Spika wa Bunge mstaafu, Mhe. Pius Msekwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anafanya kazi vizuri katika kuiletea nchi maendeleo hasa kwa kulinda na kusimamia rasilimali .
Msekwa alisema hayo jana katika mahojiano na shirika moja la utangazaji la kimataifa yaliyofanyika Ukerewe, mkoani Mwanza.
"Mwenye macho haambiwi tazama, yanayofanywa na Rais Magufuli yanaonekana wazi hata yanatoka kwenye vyombo vya habari badala ya kubaki kwenye kumbukumbu za serikali", alisema Msekwa.
Kuhusu demokrasia nchini, Msekwa amesema kuwa hali ya demokrasia nchini inaridhisha kwani viongozi muda wao wa kukaa madarakani ukiisha wanaondoka. Wanaominya demokrasia ni wale wanaong'ang'ania madarakani baada ya kipindi chao kuisha, jambo ambalo kwa Serikali ya Tanzania halipo. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani mambo mengi yamebadilika na kuwa bora zaidi. Mfano, nidhamu ya watumishi na uwajibikaji serikalini imeongezeka na hivyo ukiritimba na urasimu umepungua.
Huduma za Afya zimeboreshwa kwa kujenga na kukarabati hospitali, zahanati na vituo vya afya. Hii pia ni pamoja na upatikanaji wa dawa hospitalini kupitia bohari ya dawa ya serikali (MSD). Kwa kujali afya za Watanzania, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 39 hadi bilioni 268, jambo ambalo limefafanya upatikanaji wa dawa kuongezeka.
Mambo mengine ambayo Mzee Msekwa anasema kuwa yanashamirisha utendaji wa Rais Magufuli ni pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi, kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo ya barabara, madaraja, umeme , viwanja vya ndege na ujenzi wa reli ya kisasa yenye viwango vya kimataifa (Standard Gauge Railway).
Kwa kipindi kifupi ambacho Rais Magufuli ameingia madarakani, serikali imeweza kununua ndege 7 ambazo tatu kati yake zimeshawasili nchini na zinafanya kazi, nne zinatarajiwa kuingia nchini mwaka huu (2018).
Elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari inatolewa, jambo ambalo limefanya wanafunzi wengi kujiandikisha kuanza darasa la kwanza kwa mwaka juzi, jana na mwaka huu 2018. Uhamasishaji wa uchumi wa kati unaotokana na viwanda ni jambo jingine ambalo Serikali ya Awamu ya Tano imelitilia mkazo. Hili ni dhahiri kwa kuongeza umeme katika gridi ya Taifa hadi kufikia megawati 1,451 mwaka 2018 na kuzidi kuongeza umeme.
Ongezeko la umeme hadi kufikia zaidi ya megawati 5000 linatarajiwa ifikapo mwaka 2020, kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani. Ujenzi wa mradi wa umeme wa Stieglers Gorge, utaleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme kwa kuzalisha megawati 2100, ambao utachagiza ujenzi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment