WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba amesema serikali imefanikiwa kudhibiti matukio ya uvuvi haramu kwa zaidi ya asilimia 80 katika maeneo ya bahari na maziwa baada ya kuimarisha doria na ukaguzi wa samaki wanaovuliwa.
Aliyasema hayo wakati wa upandaji wa mikoko katika Pwani ya Bahari ya Hindi ambayo ilipandwa eneo la Mwambani Jijini Tanga chini ya Udhamini wa Mfuko wa Vodacom (Vodacom Faundation).
Alisema kuimarika kwa doria hizo kumesaidia wananachi kuwa na uelewa mpana kuhusu madhara ya uvuvi haramu na hivyo kuanz kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo ikiwemo ulinzi wa mazingira ya bahari ya hindi na rasilimali zake.
Waziri huyo alisema pamoja na jitihada za wizara katika kudhibiti fukwe za bahari zinasiendelee kuathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini bado kuna maeneo mengi ambayo yanahitaji kuhifadhiwa kwa kupandwa miti ya mikoko.
Pamoja na hayo Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Vodacom Foundation kwa kuja na kampeni ya upandaji wa mikoko ili kuhifadhi mazingira ya bahari kwa kile alichosema kuwa kutasaidia kuboresha mazingira hayo.
Naye kwa upande wake Mwakilishi wa Vodacom Foundation Rosalynn Mworia alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na chama cha skauti Tanzania waliamua kuja na kampeni hiyo upandaji wa mikoko ili kuhifadhi mazingira ya Fukwe.
Alisema kwamba kwa kuanzia kampeni hiyo wameanzia kwa mkoa wa Tanga na wanatarajia kuipeleka nchi nzima ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
No comments:
Post a Comment