Monday, April 16, 2018

MITI YA ASILI IPANDWE NA KUTUNZWA KWA FAIDA YA VIZAZI VIJAVYO-LUAMBA

Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya upandaji miti la SAHO,(wa kwanza kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wenzake baada ya kupanda moja ya mche wa mti wa asili ,katika shule ya msingi Visiga wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti ya asili inayofanywa na shirika hilo
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kibaha, Fokas Bundala(wa kushoto) akipanda mche wa mti wa asili aina ya mninga ,katika shule ya msingi Visiga wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti ya asili inayofanywa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya upandaji miti la SAHO,(wa kulia) ni diwani kata ya Visiga Mbegu Kambi Legeza.Picha na Mwamvua Mwinyi


Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

JAMII imehimizwa kupanda miti hasa ya asili ambayo ipo hatarini kutoweka pamoja na kulinda mazingira kwa faida na manufaa ya kizazi kijacho.

Aidha wananchi wameaswa kuacha kukata miti na misitu ovyo kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha kuondoa uoto wa asili.

Rai hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la – SAHO-linalojishughulisha na masuala ya upandaji miti na kuhimiza kutunza mazingira , Emmanuel Luamba wakati wa uzinduzi wao wa kampeni ya upandaji miti kata ya Visiga ,Kibaha Mkoani Pwani.

Alisema wananchi wanahimizwa kupanda miti lakini isisahaulike miti ya asili ikiwemo mninga,mkwaju,mkongo ambayo ina faida zake katika kukuza uchumi ,kuleta hewa safi na kuwa na nchi ya kijani.

Luamba alieleza wameotesha miche ya miti ya asili ipatayo 10,000 ambayo wanaisambaza iweze kupandwa taasisi za umma ikiwemo mashuleni ,kwa wananchi kata ya Visiga, kisha ngazi ya halmashauri na baadae Mkoa.

“Tumeanzia taasisi za umma ikiwemo shule mbalimbali na jamii ili kuwa na uelewa wa kujua faida za miti hii kwa manufaa ya sasa na vizazi vinavyokuja” alielezea Luamba.Akizungumzia ujio wa shirika hilo ,mwenyekiti huyo alibainisha wanatarajia kuwa na matawi nchi nzima .

Luamba alielezea kwamba lengo lao ni kurejesha miti asili kwa kiasi kikubwa kwamaana imekuwa ikivunwa kwa kasi na kuwa na hatari ya kutoweka .Nae diwani wa kata ya Visiga Mbegu Kambi Legeza aliwataka wananchi kushirikiana na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kupanda miti na kuitunza.

“Ni jukumu letu sote kuunga mkono kampeni hii ili kuwa na maeneo na nchi ya kijani pamoja na hewa safi ” alisema Legeza.Legeza alikemea ukataji miti kiholela na kuchoma moto miti kwa ajili ya mkaa kusiko kwa utaratibu maalumu hali inayosababisha kupoteza miti .

Aliishukuru SAHO kwa kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kunarejeshwa uoto wa asili na kutunza na kupanda miti kwenye mazingira yanayotuzunguka.Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ,makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Fokas Bundala aliwataka wananchi kuilinda miche ya miti wanayopewa kupanda badala ya kuitelekeza .

Kwa upande wake ,mwanafunzi wa shule ya msingi Visiga ,anaesoma darasa la saba ,Abdul Faraji alieleza wamepanda miche ya miti shuleni hapo na alilishukuru Shirika hilo kwa kuona umuhimu kuanza na kampeni hiyo katika shule mabalimbali ili kupata ufahamu wa miti hiyo.

Alisema wamekuwa wakisikia miti ya asili bila kujua ni ipi na faida zake lakini sasa atakuwa balozi mzuri kuwaelimisha watoto wengine juu ya suala hilo .

No comments: