Thursday, April 12, 2018

MEGHJEE ATUNUKIWA CHETI NA KANISA LA AICT BWIRU

Na Baltazar Mashaka, Mwanza

Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Bwiru la jijini Mwanza limemtunuku cheti Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TD & CF) Alhaji Sibtain Meghjee kwa kutambua huduma za jamii zinazotolewa na taasisi hiyo katika sekta za afya,elimu na maji bila kujali itikadi za dini wala kubagua.

Akizungumza kabla ya hafla hiyo Mchungaji Ephafra Zabron alisema taasisi ya TD & CF imefanya mambo mengi muhimu ya kusaidia jamii kwa kuhudumia watu wa dini na madhehebu mbalimbali bila ubaguzi katika masuala ya afya, elimu na maji lakini pia imejenga shule, nyumba za ibada (misikiti na makanisa) na kuchimba visima.

“Tusipotoshwe na watu kuwa watu wa dini ya Kiislamu wana mitizamo tofauti na wapo watu wanapotosha na kuleta lugha za kufarakanisha watu kuwa ukimwona Muislamu ni adui yako si kweli.Waislamu wanatuzidi mambo mengi na wanatimiza maandiko kwa vitendo ambapo kila Ijumaa wanatoa misaada kwa jamii ya wahitaji,” alisema Mchungaji Ephafra. 

Mchungaji huyo alieleza kuwa Kanisa la AICT Bwiru linatambua mchango mkubwa wa Sibtain Meghjee na taasisi yake kwa jamii kwani anafanya huduma aliyoifanya Yesu na kuwataka waumini wa kanisa hilo na wakazi wa eneo la Bwiru wajifunze kutokana na kazi zinazofanywa na The Desk & Chair.

Akisoma risala ya kanisa hilo Paulo Sweya alisema kanisa hilo linatoa huduma za kiroho na kijamii kwa waumini na watu mbalimbali kulingana na mahitaji ya jamii inayowazunguka hasa wazee wasiojiweza, wajane, yatima, walemavu na wagonjwa bila kujali itikadi wala kabila lakini pia limendelea na huduma kuu ya kueneza neno la Mungu kwa jamii ya watanzania wote ili kudumisha amani na upendo bila kujali itikadi za dini.

Aliongeza kuwa ili kumudu kuwahudumia wahitaji hao kanisa limebuni miradi mbalimbali ili kuweza kumudu kuwahudumia lakini kutokana na ukosefu wa fedha wameshindwa kuikamilisha na hivyo kutoa huduma duni zisizofikia kiwango cha ubora unaokusudiwa. 

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ukumbi wa mikutano na ufukwe, shule ya awali na huduma ya chakula kwa ajili ya kujiongezea kipato, kisima na matanki ya kuhifadhia maji, choo, mitambo ya umeme jua,nyumba ya mchungaji, ofisi za viongozi wa kanisa na usafiri, ili miradi hiyo ikamilike inahitaji kiasi cha shilingi milioni 28.5.

“Ndugu Mgeni rasmi kuja kwako hapa kumetuthibitishia kuwa ni mtu wa pekee, mwenye moyo wa upendo, msikivu unayejali wahitaji katika jamiii mbalimbali na tumejifunza kwako somo la upendo pasipo ubaguzi wa aina yoyote na hivyo wewe ni mfano wa kuigwa kwenye jamii na tunamwomba Mungu akupe afya njema uendelee kumtumikia.Pia jamii iendelee kujifunza kwako na matendo yako mema yawe somo kwa jamii ujio wako ni fundisho kwa wote wanaomwabudu Mungu aliyewaumba,”alisema Sweya.

Akijibu risala hiyo baada ya kutunukiwa cheti sambamba na Mkurugenzi wa Nitetee Foundation Meghjee aliahidi kusaidia ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa na Kanisa hilo la AICT Bwiru.

“Sisi kama waislamu na taasisi ya The Desk & Chair Foundation tunashukuru kwa kutualika na kutushirikisha kwenye ibada na shughuli zenu za maendeleo.Tunaahidi kusaidia ujenzi wa miradi yenu na tutaana na hili la maji tutaanza nalo mara moja lakini misaada tutakayoitoa lazima ifanye kazi iliyokusudiwa,”alisema.
Mwenyekiti wa The Desk &Chair Foundation (TD &CF) Sibtain Meghjee (kulia) akipokea cheti kutoka kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Mchungaji Philipo Majuja kutokana na kutambua mvhango wa taasisi hiyo wa kusaidia jamii.Hafla iliyofanyika kanisani hapo Jumalipili iliyopita.
Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Mchungaji Philipo Majuja (kushoto),akipokea kitabu cha Kuran tukufu kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk &Chair Foundation (TD &CF) Sibtain Meghjee. Anayeshuhudia kushoto wa kwanza ni Mchungaji wa Kanisa la Bwiru, Ephafra zabron na kulia ni Sheikh wa Bilal Muslim Mission of Tanzania Kanda ya ziwa Hashimu Ramadhan.Picha na Baltazar Mashaka

No comments: