Thursday, April 12, 2018

HALMASHAURI 182 ZAKAIDI AGIZO LA JPM

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

HALMASHAURI 182 nchini ikiwemo saba za mkoani Pwani ,zinadaiwa kutumia vibaya mabilioni ya fedha yaliyotumika kuondoa zaidi ya lita 100,000 za dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu ,zilizokosa soko katika kiwanda cha Biotech Products Limited,kilichopo Mji Wa Kibaha ,ikiwa ni agizo alilolitoa Rais Dkt.John Magufuli June 22 mwaka jana.

Aidha halmashauri ambazo zinadaiwa kiasi cha sh.bil.1.8 walizochukulia dawa hiyo zimetakiwa kulipa fedha hiyo haraka ili kiwanda kiweze kujiendesha na kulipa watumishi wake mishahara.

Akizungumza katika ufunguzi wa kampeni ya uhamasishaji wa ununuzi wa dawa ya viuadudu inayozalishwa katika kiwanda hicho ,meneja wa udhibiti wa ubora na viwango kiwandani hapo , Samwel Mziray , alisema ni halmashauri mbili pekee zilizochukua dawa hiyo kwa awamu ya pili.

Alieleza halmashauri 184 zilichukua dawa kwa awamu ya kwanza na ya pili zaidi ya lita 200,000 ambazo wameziweka stoo bila kuzitumia wakidai hawana fedha ya kununulia pampu."Wanashindwa kuzitumia kutokana na kukosa pampu ya kupulizia ,hii ni aibu ,nimesikitishwa sana na hali hii, "

"Ni ngumu na jambo la ajabu leo hii Rais atoke kuja kufuatilia agizo lake ama kuzifuatilia halmashauri hizo, serikali ina nia njema lakini watendaji tunashusha juhudi za Rais na serikali ""Ninawaomba wakuu wa mikoa mingine nchini kuiga mfano wa mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ya kuhamasisha kununua dawa hizo, ili kupambana na vita dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria." alieleza Mziray .

Mziray alieleza baada ya agizo la Rais walianza na mikoa 14 katika halmashauri 96 na awamu ya pili waligawa kwenye halmashauri za mikoa 12 na kutimiza mikoa 26 na halmashauri 184 nchini .Hata hivyo baada ya mgao wa kwanza halmashauri ya Rufiji iliongeza Lita 540 na Kibaha Vijijini waliongeza lita 520 .

Mziray alifafanua nchi ya Niger wameshawaunga mkono Kwa kununua dawa hiyo pamoja na Angola ambayo imeagiza lita 106,020 lakini cha kustaajabisha Tanzania na Kibaha Mjini bado hawajatambua umuhimu huo.Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri na jamii kujitokeza kununua dawa ya viuadudu ili kuondokana na vifo vinavyotokana na malaria.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alikitaka kiwanda hicho kijitangaze katika vyombo mbalimbali vya habari na kutoa elimu kwa jamii kuwa madawa hayo hayana madhara kwa matumizi ya binadamu .Alisema biashara bila matangazo haijiuzi hivyo ni wakati wa kujitangaza ili hali kuinua soko na kutambulika.

Pia Ndikilo alieleza halmashauri zilizofungia dawa hizo ni aibu "sijui tumelongwa nini,malaria ipo dawa ipo hatununui ,hivi tunasubiri Rais aje tena atununulie tena dawa ,haiwezekani"

"Nchi imetumia dollar milioni 22 ,wafanyakazi 127 wanakosa mishahara yao pale kiwandani,leo halmashauri hazioni hili ????ni lazima watumie dawa hizi na kupata matokeo" alisisitiza Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa alikemea tabia hiyo na kuwataka wachukue dawa na kuchukua nyingine pasipo kufungia stoo na kudai atakaerudia makosa aondoke kwenye nafasi yake mara moja.Ndikilo alisema hatomvumilia mkurugenzi anachezea mamilioni ya fedha wanayotenga kwa ajili ya kupambana na malaria ,na atakaejiona hatoshi aanze kuondoka katika nayadhifa yake kupisha wengine.

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Pwani, Yudas Ndungile ,alisema idara ya afya mkoa inahimiza matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu.

Alibainisha ,mwaka 2017 vyandarua 59,494 viligawiwa mashuleni pia vyandarua 48,120 viligawiwa kwenye kliniki na mwaka 2016 vyandarua 877,297 viligawiwa katika ngazi ya kaya na familia .

Ndungile alielezea wanakabiliana na malaria na kutoa elimu ya usafishaji wa mazingira kwa kuondoa mazalia ya mbu kwenye madimbwi ,suala lililosaidia vifo vinavyotokana na malaria kupungua na malaria kushuka kuwa ugonjwa wa pili kati ya magonjwa yanayoongoza kimkoa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Jennifer Omolo alisema wameitikia wito uliotolewa na mkuu wa mkoa na wanakwenda kuagiza lita 720 ili kuua mazalia ya mbu wa malaria.

Omolo alisema kuwa awali walichukua lita 520 ambazo walizitumia ,na wanaahidi kutoweka stoo . 
 Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (wa kulia) ,akimkabidhi dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu ,mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze ,Edes Lukoa wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uhamasishaji wa ununuzi wa dawa hiyo ,Mkoani Pwani.(picha na Mwamvua Mwinyi)
 Meneja wa udhibiti wa ubora na viwango katika kiwanda kinachozalisha dawa ya viuadudu cha Tanzania Biotech Products Ltd kilichopo Mjini Kibaha akionyesha wananchi kuwa dawa hiyo haina madhara, wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uhamasishaji wa ununuzi wa dawa hiyo,Mkoani Pwani .(picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments: