Saturday, March 17, 2018

WIZARA SABA KUKUTANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI MPAKANI MWA TANZANIA NA ZAMBIA

Mkuu wa mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu, Chiku Galawa akiteta jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango wa maboresho ya Mazingira ya biashara na uwekezaji mkoani Songwe, tarehe 17 Machi, 2018.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora akiendesha kikao kilicho jumuisha watendaji wa serikali na sekta binafsi wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango wa maboresho ya Mazingira ya biashara na uwekezaji mkoani Songwe, tarehe 17 Machi, 2018.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora akiongozwa na Meneja wa Kituo cha Forodha cha Pamoja Tunduma, Jomimosa Nsindo wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa maboresho ya Mazingira ya biashara na uwekezaji , mpakani mwa Tanzania na Zambia, tarehe 17 Machi, 2018.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora akifuatilia maelezo ya wateja wa Kituo cha Forodha cha Pamoja Tunduma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa maboresho ya Mazingira ya biashara na uwekezaji , mpakani mwa Tanzania na Zambia, tarehe 17 Machi, 2018. 
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU


…………….


Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini, imeamua kuzikutanisha wizara saba zinazohusika moja kwa moja na changamoto zinazopunguza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na Wawekezaji mpakani mwa Tanzania na Zambia.


Akiongea wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango wa maboresho ya Mazingira ya biashara na uwekezaji katika mkoa wa Songwe na maeneo yaliyopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora amesema mara baada ya kuhitimisha ziara yake tarehe 17 Machi, 2018, atakutana na makatibu wakuu wa wizara zinazopaswa kutoa suluhisho la changamoto hizo.

“Nitakutana na makatibu wakuu wenzangu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) na naamini maazimio tutakayotoa katika kikao hicho yatakuwa suluhisho la kuondoa changamoto zinazojitokeza hapa mpakani mwa Tanzania na Zambia” , amesema Kamuzora.

Akibainisha changamoto za mazingira ya Biashara na uwekezaji mpakani mwa Tanzania na Zambia, Mkuu wa mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu, Chiku Galawa amesema, changamoto kubwa mpakani hapo ni usalama kwa wafanyabiashara na biashara zao, ambapo kwa mazingira ya mpaka huo imekuwa vigumu kuuimarisha.

“Mpaka wetu umejengwa kila mahali , hivyo uhalifu unakuwa mgumu kuuzuia Kuna watu wanakunywa pombe Zambia ambazo tumezizuia hapa nchini kuuzwa, na kurudi wamelewa Tunduma, suala la biashara haramu ya ubadilishaji wa fedha inayofanywa mtaani kinyume na sheria na taratibu za nchi ni changamoto , lakini wafanyabiashara wanakwepa kodi kutokana na kuwa kunabaadhi ya watanzania sehemu ya nyumba zao zipo Zambia nyingine ipo Tanzania hivyo ushuru wa forodha haukusanywi kwa madai wanapeleka bidhaa hizo kwa watanzania kwani hawapitishi bidhaa hizokwenye lango husika” alisema Galawa

Galawa amebainisha mipango ambayo Mkoa umejipanga katika kuhakikisha wanakabili changamoto hizo, kuwa ni kuliweka Daftari la wakaazi katika mfumo wa kielektroniki ambalo litajumuisha wakaazi wote wa Tunduma kuanzia umri wa mwezi mmoja na litakuwa linahuishwa kila wakati, Upimaji wa mji waTunduma nao unaendelea na kila mmiliki wa ardhi atapewa hati, pia litajengwa soko kubwa mpakani hapo ili kufanya menejimenti ya biashara mpakani.

Aidha, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu alikutana na wadau wa sekta binafsi, pamoja na wateja katika Kituo cha Forodha cha Pamoja Tunduma, ambao walishauri sekta zinazohusika na Mazingira ya Biashara na Uwekezaji mpakani hapo kwa upande wa Tanzania na Zambia zikutane ili kuharakisha kutatua changamoto zinazopunguza ufanisi wa biashara mpakani hapo.

Lengo la Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ni Kupunguza gharama za Kufanya biashara nchini kwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na Wawekezaji, mpango huo unaotekelezwa na Idara, Wizara na Wakala wa Serikali kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments: