Karama Kenyunko,Globu ya jamii.
WAKILI wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Abdul Nondo, Jebrah Kambole amesema barua inayozunguka katika mitandao ya kijamii kuhusu kusimamishwa chuo kwa mwanafunzi bado hawajaipata rasmi.
Pia amesema hata Nondo naye hajaipata barua hiyo zaidi ambapo akizungumza leo jijii Dar es Salaam Kambole amekiri kuiona barua hiyo kwenye mtandao na kama barua hiyo itakuwa ni ya kweli watakaa wao kama wanasheria, Nondo, ndugu na marafiki kujadiliana na kuangalia kusimamishwa kwake na utaratibu wa kisheria ukoje.Pia haki zake zitakuwaje.
"Kama barua hiyo hata kama itakuwa ni ya kweli tutajadiliana ni njia gani tuichukue na kama ni ya kweli itakuwa ni ukiukwaji wa haki ya mtu kwa kuwa atakuwa amesimamishwa bila ya kusikilizwa.
"Na hata mfanyakazi wa kawaida akisimamishwa anaendelea kupata mshahara wake.Kusimamishwa tu kwake ni adhabu ambapo hata kama baadaye atakuja kusafishika na kuwa itakuwa amekosa masomo kwa muda wote huo,"amesema.Amefafanua kitendo cha kusimamishwa atakuwa amepata hasara ambayo haiwezi kurudishika kwani itakuwa amepoteza masomo na hata akirudi darasani wenzake watakuwa wameishamaliza na hawezi kupata masomo ambayo angepata akiwa na wenzake.
"Hivyo haki zake nyingi zitakuwa zimepotea.Sheria za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni za muda mrefu na zimepitwa na wakati kimsingi walitakiwa kutumia busara kwa kesi yake unaendelea Iringa aachwe asome masomo yake,"amesema.
Amesema anapozuiliwa asipate masomo haki zake nyingine zinakuwa zimezuiliwa ikiwamo haki ya kupata elimu na kusikilizwa na kwamba Nondo bado anadhaniwa kuwa ametenda kosa hadi hapo kosa lake litakapothibitika, hivyo UDSM itakuwa imemuhukumu bila ya kuisikiliza na bila ya kudhani kuwa anaweza kuwa hajatenda kosa hilo.Ameongeza kumekuwa na mtindo wa wanafunzi wengine wanaoshtakiwa mahakamani wanaendelea na masomo yao na ni wanafunzi wa Chuo hicho hicho.
Kambole amesema kusimamia sheria kwa njia,za kibaguzi si nzuri kwa Taifa , kusimamia sheria kwa namna ya kukandamiza watu huyu anaadhibiwa hivi na yule anaadhibiwa hivi si vizuri kwa afya ya Taifa letu.Kambole amesema sheria ikisimamiwa kwa mtindo wa kibaguzi ni itatengeneza Taifa lenye mgawanyiko na tutakuwa na sheria ambayo inatungwa kwa mtindo wa kukomoa.
Wakili, Jebrah Kambole.
No comments:
Post a Comment