Friday, March 16, 2018

TUMEJIANDAA VILIVYO TAMASHA LA PASAKA CCM KIRUMBA APRILI 1-JOHN LISSU

  Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa Tamasha la Pasaka Bw. lex Msama kushoto  akifafanua kuhusu maandalizi ya Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kanda ya ziwa Aprili 1 na 2 mwaka huu, mapema leo mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar,kulia ni mmoja wa waimbaji mahiri wa nyimbo za Kiroho (injili) John Lissu akifurahi jambo kwenye mkutano huokuhusu maandalizi ya Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kanda ya ziwa Aprili 1 na 2 mwaka huu.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa Tamasha la Pasaka Bw. lex Msama kushoto  na Mwanamuziki wa Injili John Lissu wakiimba wimbo  wakati walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kanda ya ziwa Aprili 1 na 2 mwaka huu.

 

*Awaambia wakazi wa Kanda ya Ziwa wafika kuona burudani, Msama awahakikishia usalama, maandalizi yamekamilika

Na Said Nwishehe,Globu ya jamii

MWANAMUZIKI maarufu wa nyimbo za Injili John Lissu amewaomba mashabiki wa muziki huo na Watanzani kwa ujumla hasa wakazi wa Kanda ya ziwa kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Aprili 1 mwaka huu.

Lissu ametoa kauli hiyo leo jiiini Dar es Salaam wakati akizungumzia Tamasha la Pasaka ambalo mwaka huu litafanyika Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza siku ya Aprili 1 na Aprili 2 litafanyika mkoani Simiyu katika uwanja vya Halmashauri mjini Bariadi.

Mwanamuziki huyo ameeleza kuwa wanamuziki mbalimbali maarufu wa muziki wa Injili ndani na nje ya Tanzania wataonesha vipaji vyao vya kuimba,hivyo kikubwa ni wakazi wa Kanda ya ziwa kujitokeza kwa wingi siku hiyo.

Tamasha hilo ambalo huwa linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotioni kupitia Mkurugenzi Mkuu Alex Msama ,wamehakikisha kuwa kutakuwa na  idadi kubwa ya wanamuziki wa Injili ili watu  wataofika kwenye tamasha hilo wapate burudani inayoambatana na ujumbe wenye kumpendeza Mungu

"Tunawaomba wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla tukutane uwanja vya CCM Kirumba siku ya Aprili 1 mwaka huu,wanamuziki wa Injili tumejiandaa vizuri,mashabiki karibuni muone kile ambacho tumekiandaa kwa ajili yenu.

" Siku hiyo mashabiki wa muziki wa Injili watarajie  mambo makubwa zaidi hasa kwa kuzingatia ukubwa wa Tamasha hilo nwa kwamba linafanyika wakati wa Pasaka na mwaka huu tupo Kanda ya Ziwa kwa mara ya kwanza,"amesema John Lissu.

Amefafanua kuwa kingine ambacho mashabiki watashuhudia siku hiyo ni uzinduzi wa Albam mpya ya mwanamuziki Rose Mhando inayofahamika kwa jina la Jipe moyo.John Lissu amefafanua kuwa Rose Mhando kwa muda mrefu amekuww kimya kwa kutotoa albam kwa zaidi ya miaka mitano na hatimaye mwaka huu atazindua albam hiyo.

"Watu wamemisi kumuona mwanamuziki Rose Mhando ambaye hajazindua albamu lakini kwa kutumia tamasha hilo atazindua albamu mpya ya Usife Moyo na kufanya mambo makubwa kwa kuimba nyimbo zake ambazo zimekuwa zikitamba kipindi chote," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Msama Promotion,Alex Msama amesema  maandalizi ya tamasha hilo yanakwenda vizuri na usalama upo wa kutosha ,hivyo watu wasiwe na hofu huku akiwahakikishia usalama wao na mali zao upo wa kutosha.

Pia amesema wanaangalia pia namna ya kufanya tamasha hilo katika mikoa ya Iringa na Dodoma  mara baada ya kumalizika kwa tamasha hili na kueleza lengo ni kutoa nafasi kwa mikoa mingine nayo kushuhudia namna tamasha hilo linavyovuta hisia za watanzania wengi na hasa wanaopenda muziki wa Injil.

Pia amesema ni tamasha ambalo pamoja na kuimbwa zaidi nyimbo za Injili pia linazungumzia kudumisha umoja,upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

No comments: