Thursday, March 8, 2018

MIRADI YA AJIRA YA MUDA INAYOTEKELEZWA NA TASAF KATIKA WILAYA YA BUKOMBE MKOANI GEITA YAWANUFAISHA WANANCH KICHUMI.


NA ESTOM SANGA-GEITA.

Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF wameipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa miradi ya Ajira ya Muda huo ambao wamesema licha ya kuinua kipato chao lakini pia unawaongezea hamasa ya kushiriki katika kazi za maendeleo kwenye maeneo yao.

Chini ya Utaratibu huo wa Ajira ya Muda,Walengwa wanaotoka katika Kaya Maskini huibua miradi,kuitekeleza na kisha kulipwa ujira ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya Serikali kupitia TASAF kuongeza kipato na ujuzi cha Kaya za Walengwa.

Kupitia utaratibu huu wa ajira ya muda,walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Wilaya ya Bukombe wametekeleza miradi kadhaa ikiwemo kilimo bora cha pamba, uchimbaji wa malambo ya maji na upandaji wa miti.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Malighasi katika halmashauri ya wilaya ya Bukombe ,Samweli Nyelu amewaambia Waandishi wa habari wanaotembelea mkoa wa Geita kujifunza namna TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusu Kaya Maskini kuwa wananchi wananufaika na huduma ya malambo ya maji yaliyochimbwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda na kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la uhaba wa maji kwao na mifugo yao lililokuwa linawakabili kabla ya kuanza kwa Mpango hu.

Aidha Walengwa wa TASAF kupitia utekelezaji wa Ajira ya Muda wamejikita katika kilimo cha pamba ambapo hupewa pembejeo, na utalaam na kisha kulipwa ujira kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kama njia mojawapo ya kuwaongezea kipato hususani katika kipindi cha hari.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe,Eliasi Kayandamila, amesema kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda, walengwa wa TASAF wilayani humo wamelima hekta 140 za zao la pamba na kupanda mbegu bora kulingana na maelekezo ya wataalam wa kilimo.

Amesema jitihada za halmashauri yake ni kuhakikisha kuwa walengwa na wananchi wengine wanafikiwa na wataalamu wa ugani mara kwa mara na kuwafikishia huduma ya madawa na mbolea kwa wakati kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa pamba katika msimu ujao wa mavuno.

Zifuatazo ni picha walengwa na baadhi ya kazi wanazozifanya wilayani Bukombe kupitia miradi ya Ajira ya Muda.
Baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Malighasi katika halmashauri ya wilaya ya Mbogwe wakiwa katika shamba la Pamba walilolilima kwa utaratibu wa Ajira ya Muda kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
Baadhi ya Walengwa wa TASAF wakitoa maelezo kwa Waandishi wa habari namna walivyoshiriki kazi ya ajira ya muda kwa kulima hekari tatu za pamba.
Mojawapo ya malambo yaliyochimbwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Waandishi wa habari wakipata maelezo kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Malighasi halmashauri ya wilaya ya Bukombe ,Samweli Nyeli kazi ya uchimbaji wa lambo ilivyofanywa na Walengwa wa TASAF na jinsi inavyowanufaisha wananchi wote kijijini hapo.
Ng’ombe wakinywa maji kwenye lambo lililochimbwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda katika moja ya vijiji vya halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

No comments: