Tuesday, March 6, 2018

HUDUMA YA TAXIFY BAJAJI YAWA NAFUU JIJINI DAR ES SALAAM

Machi 06, 2018, Dar es Salaam. Taxify imetangaza punguzo la asilimia 50 kwa bei ya bajaji zake jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuwavutia watumiaji wa huduma hiyo na kuwapa nafasi ya kutumia huduma zake.

Kampuni hiyo inayokuwa kwa kasi barani Ulaya na Afrika kupitia huduma zake mbalimbali za usafirishaji kwa kutumia teknolojia, imetangaza punguzo la asilimia 50 kuanzia Februari 28 kwa watumiaji wa Application yake ya ‘Taxify Bajaji’ ambapo wateja watalipa Shilingi 150 kwa kilometa na Shilingi 50 kwa dakika huku nauli ya kuanzia safari ikiwa Shilingi 300 kuanzia Jumatano Februari 28. Gharama ya nauli ya chini kabisa ikiwa Shilingi 1,000.

Wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo mpya ya Usafir wa Bajaji kwa kutumia teknolojia wiki mbili zilizopita Taxify ilikuwa ikitoza malipo ya Shilingi 350 kwa kilomita, Shilingi 75 kwa kila dakika inayotumiwa katika safari, pamoja nauli ya chini ya shilingi 750.

"Punguzo la asilimia 50 kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hususani kwa wale wote wanaopenda kutumia usafiri huu kwa safari fupi mjini ni hatua kubwa," alisema Remmy Eseka, Meneja Uendeshaji Taxify Tanzania.

Eseka alifafanua jinsi ambavyo watumiaji wa huduma hiyo watakavyokuwa wakilipa nauli zao pindi wanapofanya safari zao katika baadhi ya maeneo maarufu jijini Dar es Salaam baada ya kutolewa kwa ofa ya punguzo la asilimia 50. "Huduma mpya ya Taxify Bajaji itatoza Shilingi 1,400 tu kutoka Makumbusho kwenda Sinza, Shilingi 1,800 kutoka Ubungo kwenda Mwenge na Shilingi 2,500 kutoka Tangi Bovu kwenda Mlimani City" alisema Eseka.

Akijibu swali, kuhusu mabadiliko ya bei iwapo kama yatawaathiri madereva wa bajaji wanaofanya kazi hiyo jijini hapa. Eseka alisema, "Tutawafidia madereva kwa kuwapa bonasi ili kuhakikisha kipato chao kinabaki kuwa kizuri, hivyo hawataathirika na punguzo hili la bei."

Taxify imeendelea kuwa maarufu jijini Dar es Salaam ikiwa ni miezi mitatu tu sasa tangu kampuni hiyo tanzu ya Estonia izunduliwe jijini hapa, lakini hadi sasa imekwisha zindua huduma zake mbili jijini Dar es salaam ambazo zipo katika programu za usafiri za Kampuni hiyo, kitu ambacho ni kinawafanya waweze kuongoza katika ushindani na kuwa kampuni ya usafirishaji kwa mtandao inayopendwa katika soko na wateja wake. 

Pia bei za sasa za huduma ya Usafiri wa Taxi kupitia programu ya Taxify zina punguzo la asilimia 25, huku nauli kwa kilometa ikiwa ni Shilingi 560, Shilingi 110 kwa dakika na nauli ya kuanzia Safari ikiwa ni kiasi cha Shilingi 1,200 na bei ya chini ya Safari ikiwa ni Shilingi 3,000.

No comments: