Wednesday, February 14, 2018

Wizara ya Maji Yaanza Kutekeleza Agizo la JPM Kwa Kasi

 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akikagua mitambo ya kusukuma maji katika eneo la Mailimbili mapema leo wakati wa ziara yake yakukagua namna Wizara hiyo kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji  Taka Dodoma (DUWASA) itakavyofanikisha mradi wa kufikisha huduma ya maji katika eneo la Ihumwa unakojengwa Mji wa Serikali. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji  Taka Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo  (katikati) akifafanua  kwa Waziri wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe mikakati ya Mamlaka hiyo itakayowezesha uchimbaji wa visima virefu katika eneo la Mtumba Mjini Dodoma ambapo tayari Mamlaka hiyo imechimba sehemu ya Visima  hivyo vitakavyowezesha kufikiwa kwa kiwango cha maji kinachohitajika katika eneo unakojengwa Mji wa Serikali, Ihumwa Mjini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA), Mhandisi David Palangyo akionesha eneo utakakojengwa mfumo  wa kusukuma maji  kutoka eneo la Nzuguni mjini Dodoma  hadi eneo unakojengwa mji wa Serikali Ihumwa Mjini humo.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji  Taka Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo katika eneo lenye visima vilivyochimbwa na DUWASA ambavyo vitazalisha maji yatakayotumika katika Mji wa Serikali unaotarajiwa kujengwa Ihumwa mjini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akikagua moja ya Visima virefu vilivyochimbwa na DUWASA katika eneo la Mtumba mjini Dodoma ambapo visima zaidi vitachimbwa katika eneo hilo ili kuendana na mahitaji ya maji katika mji wa Serikali utakaojengwa Ihumwa Mjini Dodoma.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji  Taka Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo (wakwanza kulia) akimuonesha Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge eneo yakapojengwa matanki makubwa yakuhifadhia maji kabla yakusambazwa katika mji wa Serikali unaotarajiwa kujengwa Ihumwa Mjini Dodoma.
  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji  Taka Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo (wa kwanza kulia) akionesha ramani ya Mji wa Serikali na jinsi miundo mbinu ya maji itakavyojengwa kutoka katika vyanzo vya maji hadi katika mji huo .
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akionesha namna miundo mbinu ya maji itakavyojengwa kutoka katika mitambo ya maji ya Mailimbili, mjini Dodoma hadi eneo la Ihumwa utakapoojengwa mji wa Serikali. ( Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo, Dodoma)

Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
 Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaanza kutekeleza Agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kufikisha huduma ya maji katika eneo linalojengwa mji wa Serikali, Ihumwa Mjini Dodoma kwa kuanza kuchimba visima virefu vyenye uwezo wa kuzalisha mita za ukubwa 600 kwa siku.
Akizungumza wakati wa Ziara yakukagua maendeleo yautekelezaji wa Agizo hilo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa maji mengine yatachukuliwa kutoka katika matenki ya Maili mbili ambapo maji yanayozalishwa kutoka katika chanzo cha Makutopora ni lita milioni 71 wakati  mahitaji ni lita milioni 46 kwa siku.
Akifafanua Mhandisi Kamwele amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa ziada ya maji katika matenki ya Maili mbili mjini humo wataweka mtandao wa mabomba kutoka katika eneo hilo hadi Ihumwa unakojengwa mji wa Serikali ili kuharakisha shughuli za ujenzi wa mji huo .
"Kiwango cha maji kinachosukumwa ni lita milioni 61 tu kati ya milioni 71 tunazozalisha hali inayopelekea tuwe na maji ya ziada  ambayo yatasaidia upatikanaji wa maji ya uhakika hapa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya Nchi," alisisitiza Mhandisi Kamwelwe.
Aliongeza kuwa  moja ya mikakati ya Wizara yake kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) ni  kuongeza visima virefu katika eneo la Mtumba ambapo visima vingine tayari vimechimbwa tangu mwaka jana ili kukidhi mahitaji ya maji katika Mji  huo ambayo ni takribani lita milioni mbili na laki sita.
Mhandisi Kamwelwe amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu sasa.Kazi ya uchimbaji wa visima vingine katika eneo la Mtumba nje kidogo ya Mji wa Dodoma inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia leo, ikitekelezwa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amesema anaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo kupitia DUWASA katika kuhakikisha kuwa mji wa Dodoma unakuwa na maji ya uhakika yatakayochochea ujenzi wa uchumi wa viwanda na uwekezaji kwa ujumla.
Mradi wa Kufikisha maji katika mji wa Serikali ni moja ya Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa hivi karibuni kwa Wizara hiyo, pamoja na Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa miundo mbinu ya umeme inawekwa katika eneo hilo.

No comments: