Friday, February 2, 2018

WAZIRI MPINA AKAMATA MELI YA MALAYSIA , AIPA SIKU SABA KULIPA FAINI MILIONI 770/-WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amekamata meli ya uvuvi mali ya Kampuni ya Buah Naga 1 ya nchini Malaysia na kuitoza faini ya Dola za kimarekani 350,000 sawa na Sh.milioni 770 kwa kosa la kukutwa na mapezi ya samaki aina ya papa yenye uzito wa kilo 90 bila miili yake.

Ambapo hiyo ni kinyume cha Kanuni ya 66 ya kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kifungu cha18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007.

Meli hiyo ilikamatwa Januari 26 mwaka huu baada ya kufanyika ukaguzi uliosimamiwa na kikosi maalum cha kupambana na kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao yake wakati ikifanya shughuli za uvuvi katika ukanda wa Bahari Kuu kati ya Mkoa wa Lindi na Mtwara.Pamoja na kukutwa na mapezi hayo ya papa, meli hiyo ilikutwa pia na bastola aina ya Bereta ikiwa na risasi 10 bila ya kuwa na nyaraka za umiliki wake.

Akizungumza mjini Mtwara ambako meli hiyo ndiko inakoshikiliwa na Serikali Waziri Mpina ameagiza fedha hizo zilipwe ndani ya siku saba huku akitoa onyo kali kwa wamiliki wa meli waliopewa leseni za uvuvi wa Bahari kuu kufuata masharti ya vibali vyao na katika zama hizi za utawala wa Rais, Dk.John Magufuli watachukuliwa hatua kali zaidi.

"Enzi za Serikali ya Awamu Tano ya Rais Magufuli mtakaguliwa na kupekuliwa kuliko wakati wowote, hivyo ni vizuri mkatii sheria za nchi kwa mujibu wa leseni zenu,"amesema Mpina huku akisilizwa na Kapteni wa meli hiyo Han Ming Chuan  raia wa Taiwan.

Mpina amesema meli hizo zimekuwa zikitumika pia kufadhili biashara nyingine haramu ikiwemo kusafirisha dawa za kulevya ,usafirishaji haramu wa  binadamu na biashara ya silaha.Pia zinatumika kutorosha nyara za Serikali ikiwemo meno ya tembo, samaki na madini.

Aidha Waziri Mpina amesema kitendo cha wamiliki wa meli hiyo kuwakata samaki hao mapezi na kisha kutupa miili yao baharini kimeleta athari kubwa kwa Taifa kwani samaki hao wangeweza kutumika kwa matumizi mengine ya binadamu na kuchochea uchumi wa nchi.

Hivyo, ameridhia faini hiyo iliyotozwa na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Sh.milioni 770 na kuagiza kilo 90 za mapezi ya samaki na samaki wasioruhusiwa wataifishwe na kugawiwa kwa wananchi wa maeneo jirani ya Manispaa ya Mtwara. "Siku nyingine Serikali ikikamata meli iliyofanya makosa ya aina hiyo itataifishwa pamoja na vitu vyote vitakavyokuwemo kwa mujibu wa Sheria za nchi,"amesisitiza.

Waziri Mpina ameagiza wenye meli hizo kuzingatia masharti ya leseni zao zinazotaka kuwepo na asilimia 10 ya mabaharia wa kitanzania ndani ya meli zinazoingia kuvua katika Bahari kuu upande wa Tanzania.

Kwa upande wa Kamishna wa Oparesheni wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya, Luteni Kanali Fredrick Milanzi amesema meli hiyo baada ya kukaguliwa imekutwa na mapezi kilo 90 ya samaki aina ya papa na bastola yenye risasi 10 ambayo inaendelea kushikiliwa na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mtwara hadi hati za umiliki zitakapowasilishwa.

Pia mwenye meli atatakiwa kuhakikisha anawasafirisha mabaharia kurudi nchi zao kwa madai hawataki kuendelea kufanya kazi kutokana na kukiukwa kwa mikataba yao ya kazi.Aidha samaki wasioruhusiwa kuvuliwa kwa mujibu wa leseni ya uvuvi iliyopewa meli hiyo ( Bychatch) watabaki kuwa ni wa Tanzania na watauzwa kwa mnada na fedha zitakazopatikana kiasi cha sh milioni 12 zitaingizwa kwenye Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu, Hosea Mbilinyi amesema hatua zinachukuliwa kwa sasa zimelenga kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi na kwamba operesheni hizo ni endelevu na hazitambakiza mtu hata mmoja.

Wakati huohuo, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es Salaam, Wankyo Simon amesema makosa hayo adhabu yake ni kubwa na wanapaswa kuzingatia muda uliotolewa na Waziri wa kulipa faini.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina pamoja na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mtwara Francis Mkuti wakionesha baadhi ya Samaki waliovuliwa na Meli hiyo.
 Hosea Mbilonyi Kaim Mkurugenz mamlaka ya Usimamiz wa Bahari Kuu  DFSA akimuonesha waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina shehena ya Samaki  tani 4.5 wasiotakiwa kuvuliwa ambao wanatakiwa Kupigwa Mnada Siku Yoyote. 
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akilekea katika Meli Buah Naga one kukagua Samaki walivuliwa kinyume na Taratibu.. 

No comments: