Friday, February 2, 2018

DC SHINYANGA AKABIDHI HUNDI ZA MIKOPO MIL 25 VIKUNDI VYA VIJANA,WANAWAKE

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amekabidhi hundi za mikopo shilingi milioni 25 kwa vikundi vitatu vya vijana na kimoja cha wanawake zilizotolewa na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya makusanyo kutoka katika vyanzo vya mapato ndani ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Julai 2o17 hadi Disemba 2017.

Vikundi vilivyokabidhiwa hundi ni kikundi cha Wanawake na Maendeleo kilichopo katika kijiji cha Ishololo kata ya Usule na vikundi vya vijana vya Umoja wa bodaboda, Jikwamue, Shukrani Group vilivyopo katika kijiji cha Didia kata ya Didia katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Akikabidhi hundi hizo kwa wawakilishi wa vikundi hivyo leo Ijumaa Februari katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo,Matiro aliwataka walionufaika na mikopo hiyo watumie pesa walizopata kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Kila mtu aliyepata pesa akafanye kile alichokusudia kufanya, serikali inajitahidi kuwawezesha kwa kuwapatia mikopo ili mjikwamue kiuchumi,naomba mfanye kazi kwa bidii ili kubadilisha maisha yenu”,alieleza Matiro.

Aidha aliiagiza Idara ya Maendeleo na Vijana ya halmashauri hiyo kuhakikisha inatembelea vikundi vya wajasiriamali na kufuatilia kikamilifu kama fedha zilizotolewa na serikali zinatumika kama inavyotakiwa.

Matiro alitumia fursa hiyo kuwashauri vijana na wanawake kuunda vikundi vya ujasirimali watakavyovitumia kupata mikopo huku akisisitiza kuwa serikali haiwezi kutoa pesa kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bakari Kasinyo Mohammed alisema kutolewa kwa mikopo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayotaka vijana na wanawake wapewe asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ndani ya halmashauri.

Alisema pia Mwezi Julai 2017, halmashauri hiyo ilitoa shilingi milioni 3 kwa vikundi viwili vya vijana na kimoja cha wanawake hivyo jumla ya fedha zote zilizotolewa kwa kipindi cha Mwezi Julai,2017 hadi Disemba, 2017 ni shilingi milioni 28.

Wakizungumza baada ya kupokea hundi hizo za mikopo,wawakilishi wa vikundi hivyo waliishukuru serikali kwa kuwapatia mikopo wakidai kuwa hawakuwa na mitaji hivyo watatumia fedha walizopata kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati wa kukabidhi hundi za mikopo shilingi milioni 25 kwa vikundi vitatu vya vijana na kimoja cha wanawake vilivyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga zilizotolewa na halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza vijana na wanawake waliopata mikopo kutumia fedha walizopata kwa malengo waliyokusudia. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bakari Kasinyo Mohammed. Kulia ni Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Charles Maugira.
Wawakilishi wa vikundi vya vijana na wanawake waliopata mkopo pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bakari Kasinyo Mohammed akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi hundi za shilingi milioni 25 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana ambapo aliwataka kurejesha mikopo kwa wakati. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo na Vijana halmashauri hiyo, Deus Muhoja.

Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikabidhi hundi ya shilingi 5,000,000/= kwa Joyce Charles aliyewakilisha Kikundi cha Wanawake na Maendeleo kilichopo katika kata Didia chenye wanufaika watano kinachojihusisha na utengenezaji wa sabuni.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikabidhi hundi ya shilingi 6,800,000/= kwa Majaliwa Kihangaji aliyewakilisha kikundi cha Umoja wa Bodaboda kinachojihusisha na ubebaji wa abiria kwa pikipiki kilichopo katika kijiji cha Didia kata ya Didia chenye wanufaika 60. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikabidhi hundi ya shilingi 10,250,000/= kwa Methusela Jackson kutoka kikundi cha Jikwamue kilichopo katika kijiji cha Didia kata ya Didia chenye wanufaika 20 kinachojihusha na ufyatuaji wa matofali ya saruji.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikabidhi hundi ya shilingi 2,290,000/= kwa Sham Moses kutoka kikundi cha Shukrani Group kilichopo katika kijiji cha Didia kata ya Didia chenye wanufaika 6 kinachojihusisha na uchomeleaji,uunganishaji vyuma na utengenezaji masofa. 
Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo na Vijana halmashauri ya wilaya ya Shinyanga , Deus Muhoja akiwaonesha vijana fomu ya kujaza taarifa za mikopo waliyopata.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo na Vijana halmashauri hiyo, Deus Muhoja akiwasisitiza vijana waliokabidhiwa hundi za mikopo kuhakikisha wanatumia fedha walizopata kufanya maendeleo ili wajikwamue kimaisha.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: