WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa wa Mwanza kuachana na biashara ya dawa za kulevya.
Pia Waziri Mkuu amegiza vijana nchini waelimishwe madhara mbalimbali yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ili wajiepushe nazo.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumanne, Februari 20, 2018) alipozindua kliniki ya methadone kwa ajili ya waathirika wa dawa za kulevya.
Alizindua kliniki hiyo iliyopo kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure akiwa katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Serikali imejizatiti katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, hivyo nawataka wananchi wasijishughulishe nayo. waache kutumia, kusambaza na kuuza.”
Pia aliwaomba wananchi washirikiane na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa hizo.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga aliishukuru Serikali kwa kutambua madhara ya dawa za kulevya na kuchukua hatua.
Bw. Siyanga alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa waathirika wa dawa za kulevya kwenda katika kliniki za methadone ili wapatiwe matibabu yatakayowafanya kuachana na matumizi ya dawa hizo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella alisema kuwa, mkoa huo ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa biashara ya dawa za kulevya. Aidha, aliongeza kuwa bado kuna watu wanaoendeea kujishughulisha na biashara hiyo na kwamba Mkoa unaendelea kupambana nao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile alisema dawa za kulevya zinasababisha madhara makubwa katika sekta ya afya kwa kuwa yanachangia kusambaa kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo ukimwi na kifua kikuu.
Pia alisema kwa sasa dawa za methadone zinazotolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya wanazipata kutoka kwa wahisani mbalimbali. Hata hivyo, Serikali imepanga kuingiza suala hilo katika bajeti ijayo ili ianze kuagiza yenyewe.
Baadhi ya vijana waliokuwa wanatumia dawa za kulevya mkoani Mwanza akiwemo, Nyamizi Sospeter na Abdul Abdallah, waliishukuru Serikali kwa kuanzisha vituo vya methadone.
Nyamizi alitumia dawa za kulevya kwa muda wa miaka saba na muda wote huo alikuwa akiisumbua familia yake kutokana na matukio mbalimbali ya kihalifu aliyokuwa akiyafanya ili apate fedha za kununulia dawa hizo.
Naye Abdul Abdallah alisema alitumia dawa za kulevya aina ya heroine kwa takribani miaka 20 na muda wote huo alikuwa anakaba watu ili apate fedha za kununulia dawa hizo.
“Naishukuru Serikali kwa kuanzisha kliniki ya methadone na sasa nimeacha mimi pamoja na mke wangu. Najiona binadamu maana nilikuwa mwizi, mchafu kwani nilikuwa nakaa mwezi bila kuoga na hata kutengwa na jamii.”
Kwa pamoja waathirika hao wa dawa za kulevya waliiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi na kupata kipato kitakachowasaidia kuendesha maisha yao.
Awali, Waziri Mkuu alizindua muongozo wa uendeshaji wa nyumba za waathirika wa dawa za kulevya (Soba Houses) ambao unalenga kuwawezesha wamiliki wa nyumba hizo kuziendesha vizuri na kuwasaidia ipasavyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 21, 2018.
No comments:
Post a Comment