Wednesday, February 21, 2018

UJENZI WA BARABARA YA NYAHUA-CHAYA KM 85.4 KWA KIWANGO CHA LAMI WAANZA RASMI

Mkandarasi kutoka kampuni ya CHICO kutoka China, Bw. li, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuhusu hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiwaonesha Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Queen Mlozi na Mbunge wa Jimbo la Igalula ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi, eneo ambapo ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami itajengwa, mkoani Tabora.
Tingatinga likikata miti kwa ajili ya kusafisha eneo ambapo ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami utaanza, mkoani Tabora. 



Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa kampuni ya CHICO kutoka China, ili kuweza kuufungua mkoa wa Tabora na mikoa jirani ya katavi na kigoma.

Amesema hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati aliposimamishwa na wakazi wa kijiji cha Tura, wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, alipokuwa akikagua kambi ya mkandarasi na kuangalia hatua za awali za matayarisho ya ujenzi wa barabara hiyo.

Prof. Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 117.9 na utachukua miezi 24 mpaka kukamilika kwake."Serikali imeanza rasmi ujenzi wa barabara hii na sasa ni jukumu lenu kuhakikisha mnampa ushirikiano mkandarasi huyu ili mradi uwahi kukamilika mapema", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amefafanua kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu katika kukuza biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani. Ameongeza kuwa sasa Serikali imeshapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka daraja la Kikwete mpaka Uvinza, mkoani Kigoma na hivyo itasaidia wananchi wanaotumia usafiri wa mabasi kutoka mkoa wa Dar es Salaam mpaka mikoa ya katavi na Kigoma kupita kwenye lami njia nzima.

Naye Mbunge wa Jimbo la Igalula mkoani Tabora ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi, amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa yeye na timu yake watajitahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutohujumu vifaa vya mkandarasi huyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Queen Mlozi, ameishukuru Serikali kwa mradi unaoendelea katika wilaya hiyo na kumuahidi Waziri kuwa yeye na kamati ya usalama itahakikisha mkandarasi hahujumiwi.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Mhandisi DamianNdibalinze, amemueleza Waziri kuwa kazi imeanza kwani Mkandarasi ameshaanza kuleta vifaa eneo la kazi na ujenzi wa kambi unaendelea.

Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora ikiwa ni lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea mkoani humo .

No comments: