Wataalam wa Afya moja nchini ambao ni wataalam wa sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameanza kuandaa Mpango Mkakati wa ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi utakaosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa sampuli za vimelea hivyo hatarishi kutoweza kueeneza magonjwa kwa binadamu.
Mpango huo utatoa mwongozo wa namna sekta za Afya nchini ambazo ni sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira kushirikiana katika kuvichukua vimelea kwa wanyama, binadamu na mimea au wakati wa kuvisafirisha na kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi na wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi.
Akiongea wakati wa Mkutano wa wataalamu wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini, leo tarehe 28 Februari,2018 mjini Morogoro, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu alibainisha kuwa serikali imedhamiria kuijenga jamii yenye Afya bora kwa kuikinga na majanga yatokanayo na magonjwa ya mlipuko hivyo imeamua kuandaa mpango huo ili kuboresha uratibu.
Naye mratibu wa Mkutano huo anayeshughulikia masuala ya Ulinzi na Usalama wa vimelea hatarishi katika wizara ya Afya, Jacob Lusekelo, alibainisha mpango huo ambao utatoa mwongozo wa sekta za Afya kushirikiana utasaidia kupunguza maabukizi ya vimelea hivyo kwa wanyama na binadamu.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini, ikiwemo wataalamu wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini, ambao unawajumuisha wataalamu wa kutoka katika sekta zote za afya katika masuala ya maabara.
Afya Moja ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa , kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu ,wanyamapori na mifugo. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na Shirika la Maabra SANDIA na DTRA wameandaa mkutano wataalam hao.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu akieleza jambo wakati wa Mkutano wa wataalamu wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini, uliojikita katika ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi leo tarehe 28 Februari, 2018 mjini Morogoro.
Mtaalamu Masuala ya Mpango Mkakati wa Maabara kutoka Shirika la Maabara –SANDIA, Laura Jones, akifafanua umuhimu wa Mpango huo wakati wa Mkutano wa wataalamu wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini, uliojikita katika ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi leo tarehe 28 Februari, 2018 mjini Morogoro.
Baadhi ya Wataalamu wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini, wakijadiliana namna ya kuandaa Mpango Mkakati wa ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi, leo tarehe 28 Februari, 2018 mjini Morogoro.
Wataalamu wa Afya moja wanaounda Mtandao wa Huduma za Maabara nchini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano wa kuandaa Mpango Mkakati wa ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi, leo tarehe 28 Februari, 2018 mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment