Wednesday, February 14, 2018

WAKULIMA WA KOROSHO PWANI WAPATA BIL.57.7 KUTOKANA NA MAUZO YA KOROSHO

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha 

Wakulima wa zao la korosho Mkoa wa Pwani wamefanikiwa kupata kiasi cha sh. bilioni 57.7 kutokana na mauzo ya zao la korosho ,msimu huu. Mafanikio hayo yametokana na mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umetumika miaka mitatu iliyopita tangu kuanzishwa kwenye Mkoani hapo. 

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC). Alisema fedha hizo zimepatikana kutokana na minada sita hadi kufikia Januari mwaka huu ambapo minada hiyo ilianza Novemba mwaka jana. 

Ndikilo alifafanua ,kilo zilizouzwa ni 20,399,325 za daraja la kwanza ni kilo 11,554,380 na daraja la pili ni kilo 8,814,945. “Kilo hizo kwa daraja la kwanza ziliingiza kiasi cha shilingi bilioni 35.8 na daraja la pili shilingi bilioni 21.4 kwa wakulima wa mkoa huo” 

“Wilaya ya Mkuranga imeweza kuongoza kwa kuuza na kupata mapato makubwa ikiwa imeingiza kiasi cha bilioni 13 ikiwa imeuza kilo milioni 4.1, Kibiti waliingiza bilioni 4 kwa kuuza kilo milioni 4,Rufiji bilioni 2.8 kwa kuuza kilo milioni 1.5,” alisema Ndikilo. Awali katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Shangwe Twamala alieleza, bei ya juu kwa korosho daraja la kwanza ilikuwa ni shilingi 3,817 kwa kilo na daraja la pili ni shilingi 2,950. 

Twamala alisema baadhi ya changamoto ni pamoja na mfumo huo umepata changamoto za malalamiko ya wanunuzi juu ya kushuka ubora na upungufu wa uzito. Alisema baadhi ya wanunuzi kushindwa kuwalipa wakulima kwa wakati, uhaba na ubora wa maghala,baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kutokuwa waaminifu. 

Pamoja na hayo, mkoa huo umetoa mapendekezo ya mpango wa bajeti wa shilingi bilioni 296.7 kwa mwaka 2018/2019. Akitoa mwelekeo wa bajeti ya mkoa katibu tawala msaidizi mipango na uratibu Edward Mwakipesile alisema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo. 

Mwakipesile alisema kuwa ili kutekeleza mpango na bajeti ya sekretarieti ya mkoa na mamlaka za serikali za mitaa kwa mwaka huo wa fedha. Alisema kuwa kati ya fedha hizo bilioni 222.4 zitatumika kwa ajili ya malipo ya mishahara ya watumishi, bilioni 32.4 kwa ajili ya miradi ya aendeleo,bilioni 23.8 ni mapato ya ndani bilioni 18 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. 

“Katika fedha za miradi ya maendeleo za ndani ni bilioni 25 na za nje bilioni 7.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali,” alisema Mwakipesile.
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na wajumbe wa kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC)kuhusiana na mipango na mkakati mbalimbali ya kuendeleza maendeleo ya kimkoa.(Picha na Mwamvua Mwinyi) 

No comments: