Wednesday, February 14, 2018

KWANDKWA: SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA UJENZI NA UCHUKUZI MKOA WA TANGA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shighella mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya Naibu Waziri huyo ajaanza kukagua miradi ya barabara katika Wilaya za Pangani na Muheza jana Jumanne Februari 13, 2018. 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiiaino, Elias Kwandikwa akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya barabara katika Wilaya hiyo jana Jumanne Februari 13, 2018. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Bi. Zainab Issa. 
Meneja wa TANROAD Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro akitoa maelezo ya ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa (wa pili kulia)kuhusu ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa kilometa 550 linalotarajia kujengwa na Serikali katika Mto Pangani wakati wa ziara yake Wilayani humo jana Jumanne Februari 13 2018. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Zainab Issa. 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akipata maelezo kuhusu ufafanisi wa utendaji kazi wa kivuko cha MV Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya barabara na vivuko katika Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla katika ziara yake jana Jumanne Februari 13 2018. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Serikalini (TEMESA), Mhandisi Magreth Ginna. 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akishuka katika kivuko cha MV Tanga iliyopo Pangani wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya barabara na vivuko katika Wilaya za Mkoa wa Tanga jana Jumanne Februari 13, 2018. Anaongoza nao Diwani wa Kata ya Pangani Magharibi, John Semhande na Meneja wa TEMESA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Magreth Ginna na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Issa. (PICHA NA MAELEZO 

………………… 



Na Ismail Ngayonga -MAELEZO 


NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema Serikali imekusudia kuimarisha sekta ya ujenzi na uchukuzi katika Mkoa wa Tanga ikiwemo Ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa Mita 550 katika Wilaya ya Pangani, hatua inayolenga kufungua fursa na kuinua pato la kiuchumi kwa wanachi wa Mkoa huo. 

Akizungumza katika mkutano wake na Mkuu wa Mkoa huo, Martin Sheghela jana Jumanne Februari 12, 2018, Naibu Waziri Kwandikwa aliyopo katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya barabara Mkoani humo, alisema lengo la Serikali ni kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na uwanja wa ndege katika Mkoa wa Tanga. 

Kwandikwa alisema katika bajeti ya mwaka 2017/18 Serikali imekusudia kuanza ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani-Saadani-Bagamoyo yenye urefu urefu wa kilometa 242, ambapo tayari kazi ya usanifu wa barabara hiyo tayari umeaanza, ambapo wakati wowote kutoka sasa Serikali inatarajia kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo. 

“Kwa kipande cha barabara ya Tanga-Pangani ambayo imekuwa kilio cha wananchi wa Pangani kwa kipindi kirefu, tayari tumeanza hatua ya usanifu wa barabara hiyo, ambapo Serikali imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 4.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo” alisema Kwandikwa. 

Aliongeza kuwa Serikali pia imepanga kuharakikisha ujenzi wa Barabara ya Handeni-Kilindi-Nchemba-Mkoro yenye urefu wa kilometa 461 ambayo inatarajia kuunganisha Wilaya ya Kondoa na Mkoa wa Singida, hatua inayolenga kuongeza fursa ya shughuli za uzalishaji mali kwa kuzingatia fursa ya ujenzi wa bomba la mafuta linloatarajiwa kuanza ujenzi wake mwaka huu. 

Kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege na uimarishaji wa bandari ya Mkoa wa Tanga, Naibu Waziri Kwandikwa alisema uwezeshaji na utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wake upo katika miradi ya Afrika Mashariki, ambapo kukamilika kwake kutasaidia kuzalisha ajira na kuongeza mvuto wa Mkoa wa Tanga kwa wawekezaji mbalimbali. 

Kwa mujibu wa Kwandikwa alisema mbali na Mkoa wa Tanga, Serikali imekusudia kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara nchini kwa wakati hatua inayolenga kuwapunguzia gharama wananchi na kuokoa muda wa kusafirisha bidhaa na malighafi. 

“Ujenzi wa Barabara ya Handeni-Kilindi-Nchemba-Mkoro ukikamilika unatarajia kuokoa zaidi ya kilometa 150 kwa abiria wanaosafiri kutoka Dar Es Salaam hadi Singida, huu ni mradi muhimu na hivyo tutaupa kipaumbele cha pekee” alisema Kwandikwa. 

Kwa upande wake Mkuu wa MKoa wa Tanga, Martin Sheghella alisema ujenzi wa miundombinu ya uhakika ikiwemo uimarishaji wa bandari ya Tanga katika Mkoa huo utasaidia kuongeza pato la wananchi na mapato ya Serikali kwa kujenga ushawisihi wa Nchi jirani ikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutumia Bandari hiyo. 

“Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya Shehena za mizogo Milioni 28 zinasafirishwa katika nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na DRC lakini iwapo tutaimarisha bandari ya Tanga tutaweza kukifanya nchi hizi zikatumia bandari yetu” alisema Sheghella.

No comments: