Waziri wa Kilimo, Eng. Charles Tizeba, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiongea na mkulima wa pamba wilayani Igunga.
Waziri wa Kilimo, Eng. Charles Tizeba na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga wakikagua zao la pamba wilayani Igunga.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri wakikagua shamba la pamba wilayani Kwimba
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akipulizia dawa shamba la pamba wilayani Kwimba. Uzalishaji wa pamba nchini unatarajiwa kuongezeka mara tano msimu huu wa kilimo 2017/2018 kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Bodi ya Pamba kuhamasisha wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kuzingatia kanuni za kilimo bora cha pamba, kuimarika kwa mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, ubora wa mbegu za kupanda zilizosambazwa kwa wakulima na kuongezeka kwa eneo la uzalishaji wa pamba.
Akiongea katika ziara ya kukagua maendeleo ya uzalishaji wa mbegu bora wilayani Igunga, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Bwana Marco Mtunga amesema, uzalishaji unatarajiwa kuongezeka kwa takriban asilimia 400 kutoka tani 133,000 zilizozalishwa msimu wa 2016/17 hadi kufikia zaidi ya tani 600,000 msimu huu wa 2017/18.
Aliendelea kueleza kwamba, eneo la uzalishaji wa pamba limeongezeka kutoka ekari 659,000 hadi ekari 3,000,000 ambapo jumla ya tani 26,500 za mbegu zimepandwa zikiwemo tani 8,000 za mbegu za msimu uliopita zilizokuwa kwa wakulima. Kuongezeka kwa eneo la uzalishaji wa pamba kumetokana na uhamasishaji uliofanywa katika maeneo inakolimwa pamba, kuongezeka kwa mikoa mipya ya Dodoma na Katavi katika uzalishaji wa pamba na bei nzuri ya pamba waliyolipwa wakulima msimu uliopita.
“Juhudi za serikali na wadau wengine ndani ya tasnia zimeanza kuzaa matunda; eneo la uzalishaji limeongezeka mara dufu, asilimia 60 ya wakulima wamepanda pamba kwa mistari na kwa nafasi inayopendekezwa hali itakayowafanya kuwa na mimea ya kutosha kwa eneo hivyo kuongeza tija. Upandaji wa pamba kwa mistari hauongezi mimea kwa eneo tu bali pia unarahisisha kazi ya kuhudumia shamba wakati wa palizi, kupunguza miche iliyozidi na kunyunyizia viuadudu” alisema Mtunga.
Amesema, Bodi ya Pamba imejipanga vizuri huhakikisha pamba yote iliyolimwa inapata viuadudu kwa wakati. Kutokana na kuongezeka kwa eneo la kilimo, makisio ya chupa milioni 4.5 ya viuadudu za awali hazitatosheleza. Makisio mapya ya viuadudu ni chupa milioni 9 kwa wastani wa minyunyizo mitatu kwa kila ekari moja ambapo jumla ya shilingi bilioni 36 zinahitajika. “Kama hatua za awali kunusuru jahazi, Wizara ya Fedha kupitia Hazina na Benki ya Kilimo wametoa kiasi cha shilingi bilioni 10 kama malipo ya awali ya chupa 6,500,000 za viuadudu.
“Serikali inafahamu mahitaji makubwa ya viuadudu vya pamba msimu huu na inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wakulima wanapata viuadudu vya kutosha kuhudumia pamba yao” alisema Mtunga na kuongeza kuwa “tarehe 5/2/2018 bodi imeanza kupokea viuadudu na kwamba mwezi Februari tumepanga kusambaza chupa 2,000,000 na mwezi Machi chupa nyingine 2,000,000”.
Aliendelea kusema kwamba, pamoja na mahitaji ya viuadudu kuwa makubwa na usambazaji wa viuadudu kuanza katika maeneo yote inakolimwa pamba Kanda ya Magharibi, yamejitokeza malalamiko ya viuadudu kutofanyakazi vizuri katika wilaya ya Kwimba, hali ambayo ililazimu kuundwa kwa timu ya wataalam tarehe 11/1/2018 iliyojumuisha Watafiti, TPRI na Bodi ya Pamba. Timu hii kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba na viongozi wengine walitembelea mashamba ya wakulima na kujiridhisha kwamba viuadudu vinafanya kazi vizuri.
Pamoja na jitihada hizi, malalamiko yaliendelea ambapo timu hii ilirudi tena tarehe 27/1/2018, walikagua mashamba na kuongea na wakulima; ilionekana kuwa viuadudu ambavyo vimesambazwa aina ya duduba na duduall vinafanyakazi vizuri. “Izingatiwe kwamba viua dudu hivi ndivyo vilivyosambazwa katika wilaya zote zinazolima pamba na wakulima wanasema vinafanya kazi.”
“Timu ya wataalam ilibaini kwamba, wakulima wengi wanatumia viuadudu vya pamba kudhibiti wadudu kwenye mahindi na choroko na kuacha pamba ikishambuliwa na wadudu huku wakilalamika kuwa viuadudu haviui wadudu” Alisema Mtunga na kuongeza kuwa, Bodi ya Pamba kama msimamizi wa Tasnia ya Pamba haina uwezo wa kuzuia wananchi kutumia viuadudu vya pamba kunyunyizia kwenye mahindi au choroko pamoja na ukweli kwamba hali hii inasababisha upungufu wa viududu kwenye zao la pamba. Akiwa katika wilaya ya Igunga, Mtunga amewaondoa wakulima wasiwasi wa kutofikiwa kwa lengo la kuzalisha kilo 1000 kwa ekari kutokana na kutofahamu namna bora ya kutumia viuadudu.
Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti Ukiriguri na Halmashauri za wilaya watapeleka wataalam katika maeneo ya uzalishaji wa pamba kusimamia kwa karibu zoezi la unyunyiziaji wa viuadudu kwenye pamba. alisema Mtunga na kuongeza kwamba ili mkulima wa pamba aweze kupata kilo 1,000 kwa ekari anahitaji kuwa na mimea zaidi ya 20,000 kwa ekari; iwapo kila mmea wa pamba utazaa matunda 20 tu mkulima anapata kilo 1,000 au zaidi katika ekari moja.
Hili linaweza kufikiwa kwa sababu wakulima asilimia zaidi ya 80 katika wilaya ya Igunga wamepanda pamba kwa mistari na kwa nafasi inayopendekezwa. Mtunga alisema kwamba, Juhudi kubwa zimefanyika kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya pamba msimu huu, na kutoa rai kwa wadau wote kuunga mkono juhudi hizi ili kurejesha sifa ya zao la pamba katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Kwa juhudi zilizokwishafanyika ni dhahiri kipato cha mkulima kitaongezeka, wachambuaji watapata pamba bora itakayouzwa kwa bei nzuri katika masoko ya kimataifa na pato la taifa litaongezeka.
No comments:
Post a Comment