Na Lorietha Laurence-Dodoma
Serikali imeeleza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kama zilivyo taasisi nyingine kimefuata taratibu za ujenzi na umiliki wa viwanja vya michezo kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe .Juliana Shonza leo Mkoani Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupa Victor Mwambalaswa, lililohoji kuhusu viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na Chama hicho.
“Ni vizuri ikafahamika kwamba mpaka sasa viwanja hivyo vinaendelea kutumika na umma wa watanzania kwa shughuli mbalimbali za kimichezo, kijamii na kiserikali sawa kabisa na Mipango ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995, Sura ya 4 (i)-(ii)”
“kwa hiyo kuhusu suala la uporaji wa viwanja hivyo, CCM hakijafanya uporaji wowote kwa kuwa kinamiliki viwanja hivyo kihalali kwa mujibu wa sheria zilizopo hivyo ushiriki wa wananchi wenye mapenzi mema katika ujenzi wa viwanja hivyo hauondoi uhalali wa Chama cha Mapinduzi kumiliki viwanja hivyo”amefafanua Shonza.
Aidha Naibu Waziri Shonza amesema kuwa, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1955, sura ya 7(vi) inaeleza wajibu wa Mamlaka ya Serikali za mitaa kushirikiana na wadau kujenga, kulinda na kutunza miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja.
Akizungumzia kuhusu mpango wa serikali katika kusaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja wa chunya Shonza amesema kuwa, ujenzi wa viwanja vya michezo ni jukumu jumuishi ambalo linawapa fursa wadau na wananchi kujenga na kuendeleza miundombinu ya michezo katika maeneo yao kwa manufaa ya jamii.
Hata hivyo, Mhe. Shonza amepongeza juhudi za wananchi wa Chunya kwa jitihada za kuanza ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye thamani ya bilioni 8 huku Halmashauri ya Chunya ikiwa imetenga kiasi cha shilling Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mhe. Shonza amezidi kufafanua kuwa Serikali katika awamu zote tokea kupatikana kwa uhuru imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza watu binafsi, mashirika na Taasisi kuchangia katika kujenga na kuendeleza viwanja vya michezo nchini.
No comments:
Post a Comment