Tuesday, February 6, 2018

SHEHENA YA MAGOGO 297 YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI MIL.26.3 YATAIFISHWA MANYONI

Na,Jumbe Ismailly ITIGI 

SHEHENA nyingine ya magogo 297 yenye thamani ya shilingi milioni 26,370,000/= yaliyokuwa yakimilikiwa na Kampuni ya ARIZONA ENTERPRISES iliyopo katika Mji mdogo wa Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida yametaifishwa na serikali wilayani Manyoni na hivyo kufanya jumla ya magogo 720 yaliyotaifishwa na serikali baada ya kubainika kwamba mmiliki wa kampuni hiyo alikiuka taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu.

Mapema mwezi Oktoba,2017 serikali wilayani Manyoni ilitaifisha shehena ya magogo 423 yenye thamani ya shilingi milioni 283,022,000/= yaliyokuwa yamefichwa kwenye mashamba ya Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi,Yahaya Masare katika Kijiji cha Damwelu,kata ya Ipande,wilayani Manyoni,baada ya mmiliki wa mashamba hayo kuyakana kuwa siyo mali yake,licha ya kwamba mmoja wa watu waliokuwa wakishikiliwa na polisi wilayani Manyoni,Hassani Masare ni ndugu yake.

Akithibitisha shehena hiyo ya mazao ya misitu kutaifishwa,Afisa Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Itigi,Rodney Ngalamba alisema baada ya kukamilisha taratibu za kisheria,mtuhumiwa au mshukiwa wa magogo hayo aliweza kulipa serikalini faini ya shilingi milioni 46.

Kwa mujibu wa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya ardhi na Maliasili aliweka bayana pia kwamba katika upekuzi iligundulika kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria kwa maana baadhi ya shehena katika kiwanda ARIZONA ENTERPRISES kilichopo mjini Itigi kulikuwa na mzigo zidifu wa magogo 297.

“Kwa hiyo baada ya hapo mzigo huu wa magogo 297 pamoja na mzigo ule uliokamatwa awali shambani vimewekwa chini ya uangalizi wa serikali kwa ajili ya kupigwa mnada hapo baadaye kama taratibu za sheria za misitu namba 14 ya mwaka 2002 inavyoeleza.”alisisitiza Ngalamba.
Hata hivyo Ngalamba alithibitisha pia kwamba kimsingi magogo hayo yanaonekana ni ya HARIMU ENTERPRISES ambaye ni mshirika mkubwa wa kiwanda cha ARIZONA ENTERPRISES kinachomilikiwa na Yahaya Omari Masare kilichopo Itigi mjini.

Akizungumzia kuhusu hatua itakayofuata baada ya mtuhumiwa kutozwa adhabau ya faini,Ngalamba aliweka bayana kuwa shehena hiyo ambayo imetaifishwa na serikali itauzwa kwa njia ya mnada na baada ya kupatikana kwa nyaraka zinazohalalisha mzigo uliopo kiwandani,mmiliki wa Arzona Enterprises ataweza kurudishiwa ili aweze kuendelea na shughui zake za uchakataji wa magogo hayo.

Kuhusu shehena nyingine ya magogo iliyogundulika kwenye kituo cha reli Itigi,afisa huyo alibainisha kuwa magogo hayo bado yapo kituoni hapo na kwamba baada ya kupatiwa nyaraka halali ikiwemo TP,ndipo ataendelea na utaratibu wake ikiwepo kupeleka kwenye soko la kuuzia mazao hayo.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Halmashauri hiyo,Gilbert Modesti Kalanda aliyekuwa mmoja wa wajumbe sita wa tume iliyokwenda Kaliua,alisema akiwa mmoja wa wajumbe wa Tume hiyo walikwenda Mkoani Tabora,na wilayani Kaliua kwenye eneo ulikotoka mzigo huo la Mpandaline mpakani mwa Kaliua na Katavi.

Kwa mujibu wa Kalanda baadhi ya mapendekezo ya tume hiyo yalikuwa ni pamoja na kuainisha makosa ya kukutwa na mazao ya misitu bila kufuata sheria na walimtaka mtuhumiwa kulipa shilingi milioni 26,370,000/= ambazo ni gharama za mzigo wote

“Lakini sheria inaenda mbali zaidi kwamba baada ya kulipa hizo gharama tajwa faini tajwa nini kinatakiwa kifanyike kwenye mzigo ambao unahusika kwenye ufanyikaji wa makosa hayo ya kisheria,tunaelekezwa pia na kifungu namba 95 kinachohusiana na masuala ya Compound tunatakiwa kutaifisha mzigo husika wa mazao ya misitu na kuwa mali ya serikali ambao utauzwa kwa taratibu za kimnada”alisisitiza.
 Mwanasheria wa Halmashauri ya Itigi,Gilbert Modesti Kalanda akitoa maelezo ya sababu zilizofanya magogo 297 kutaifishwa na kusubiri kuuzwa kwa njia ya mnada na serikali ya wilaya ya Manyoni.(Picha zote Na Jumbe Ismailly) 
baadhi ya magogo yaliyotaifishwa na serikali yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 26.3 kutokana na kukiuka taratibu za kisheria zinazosimamia misitu.

No comments: