Na John Nditi, Morogoro
MKUU wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ameunda timu maalumu inayojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama itakayoshirikiana na wataalamu wa uthamini wa Serikali na wenyeviti wa vitongoji vya vijiji vya Bwila Chini na Kiburumo , kata ya Selembala , halmashauri ya wilaya ya Morogoro ili kuhakiki upya majina ya waliolipwa fedha za fidia na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa bawawa la Kidunda.
Mkuu wa mkoa amelazimika kuunda timu hiyo baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wa vijiji hivyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bwila Chini na kuhudhiriwa na mamia ya wananchi wa vijiji hivyo.
Dk Kebwe alisema , ameiunda timu hiyo licha ya pande zote kueleza kwa udani namna zoezi la uhakiki na uthamini wa makazi ya watu wa vitongoji vinane vya vijiji hivyo kuelezwa kuwa zoezi hili lilifanyika kwa uwazi ulioshirikisha wenyeviti wao wa vitongoji na malipo kufanyika baada ya taratibu zote za kisheria kufuatwa.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliopewa furasa ya kuuliza maswali wakidai kuwa wapo baadhi ya watu wamelipwa fedha za fidia wakati zi wakazi wa vitongoji vya vijiji hivyo wakiwa hawana nyumba wala mashamba .
“ Nimelazimika niunde timu ya baadhi ya wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama itakayoshirikiana na wataalam na viongozi wa serikali za vitongoji kuhakiki majina yote kwa ajili ya kujiridhisha ili kubaini endapo madai ya wananchi yanaukweli ama laa na yakiwa na ukweli hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika” alisema Dk Kebwe.
Alisema, utekelezaji huo utawahushisha timu ya awali ya kikosi kilichofanya kazi wakati wa zoezi la uthamini siku za nyuma wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao wataungana na wengine wapya kuendesha uhakiki wa majina ya waliolipwa.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa vitongoji hivyo kuungana na timu hiyo wakati wa kupitia uhakiki wa majina ya waliothaminiwa awali hadi walipolipwa fedha za fidia ili kubaini endapo kuna majina hewa.
“ Polisi (CID) Takukuru na Usalama wa Taifa watapita kuhakiki majina ya waliolipwa fidia katika kila kitongoji “ alisema Dk Kebwe na kuongeza kuwa
“ Timu hii mpya itashirikiana na wenyeviti wa vitongoji na wananchi wote wawe kwenye maaneo yao kila siku kitongoji kimoja na kazi hii inapashwa kuanza Jumatano ijayo…( Feb 28, 2018) ili kubaini watu waliolipwa hewa na Dawasa , endapo itabainika hatua kali za kisheria kwa waliohusika zitachukuliwa“ alisema Dk Kebwe .
Mkuu wa mkoa pia , aliitaka Dawasa kutengeneza utaratibu kwa wale ambao hawakulipwa fedha za fidia awamu ya kwanza na ya pili ingawa tayari walifanyiwa uthamini lakini majina yao kukosekana kuonekana kwenye vitabu vya malipo walipwe mara moja.
Pia alitoa siku 14 kwa Dawasa na mthamini wa serikali kwa kushirikiana na watendaji wa idara ya afya kuharakisha uthamini wa makaburi ili taratuibu za malipo ziweze kuchukuliwa na wahusika kuipwa kwa mujibu wa sheria kuwezesha uhamishwaji wa makaburi eneo la mradi wa bwawa la Kidunda ufanyike kwa kushirikisha wahusika kulingana na imani zao na dini .
Naye ,Mthamini Mwandamizi wa wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Robert Lisasi akizungumza katika mkutano huo wa hadhara alisema , zoezi hilo lilifuata taratibu zote za kisheria ambapo zaidi ya watu 1,700 walihakikiwa mali zao na kufanyiwa uthamini na walilipwa fidia kulingana na bei zilizowekwa na serikali .
Hata hivyo alisema , katika zoezi hilo waliletwa wathamini wageni kutoka nje ya mkoa huo ambao walishirikiana na wenyeviti wa vitongoji katika zoezi hilo na pia serikali ya mkoa kuwaongezea maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kwenye timu hiyo ili kuondoa mianya ya rushwa na upendeleo .
Kwa upande wake, Meneja wa Miundombinu wa Dawasa , Mhandisi John Kirecha mbele ya mkutano huo alisema kuwa , Dawasa ilikuwa ni mwezeshaji na mlipaji wa fedha za fidia baada ya kuletewa vitabu vilivyopitishwa na mthamini wa serikali.
Alisema , vitabu hivyo vyenye orodha ya majina vilisainiwa na mamkala za serikali za vijiji, kata , wilaya na mkoa vikionesha majina na kiwango vya fedha kwa kila mmoja wao anayestahiki kuliipwa, isipo kuwa majina 15 hayakuweza kuonekana ndani ya vitabu igawa tayari walihakikiwa na kuthaminiwa mali zao kwa ajili ya kulipwa fedha zao.
Hata hivyo alisema , watu hao 15 tayari utaratibu wa kuandaliwa malipo unaendelea kufanywa na mamlaka hiyo .
Nao baadhi ya wakazi wanaopaswa kuhama ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda ambao walishalipwa fidia awamu ya kwanza nay a pili kwa nyakati tofauti walidai kuwa hawakulidhika na viwango hivyo na baadhi ya watu waliolipwa si wakazi wa maeneo hayo na hawana nyumba wala mashamba.
Hivyo alimwomba mkuu wa mkoa kuunda tume ya kufuatilia majina ya watu waliopitwa fedha za fidia za kuhamishwa katika vijiji hivyo wakati hawakuwa na makazi wala mashamba ili ukweli uweze kubainika na endapo watakuwepo washukuliwe hatua wao na wale walioshiriki kufanya mchezo huo.
No comments:
Post a Comment