Thursday, February 8, 2018

RC MNYETI AENDESHA HARAMBEE NA KUPATIKANA SHILINGI MILIONI 17 UJENZI WA MAABARA

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari Bishop Hando iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana Wilayani Mbulu, ambapo aliwapa zawadi ya shilingi milioni moja walimu wa shule hiyo na wanafunzi aliwapa chakula, magunia 100 ya mahindi baada ya kushika nafasi hiyo.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Bishop Hando ya Kata ya Masqaroda Wilayani Mbulu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alipotembelea shule hiyo ambapo aliendesha harambee ya umaliziaji wa ujenzi wa jengo maabara na kupatikana shilingi milioni 17.5.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akimsikiliza mwalimu wa shule ya sekondari Bishop Hando, ya Wilayani Mbulu Samuel Surumbu alipotembelea shule hiyo na kufanya harambee ya umaliziaji wa ujenzi wa jengo la maabara na kupatikana shilingi milioni 17.5 Wanafunzi wa shule ya sekondari
Wanafunzi wa shule ya sekondari Bishop Hando na wananchi wa Kata ya Masqaroda Wilayani Mbulu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alipotembelea shule hiyo kwenye ziara yake ya siku saba ya kutembelea wilaya ya Mbulu, ambapo anakagua miradi ya maendeleo, kuwasikiliza wananchi na kuzungumza nao.

………………….

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti ameendesha harambee iliyopatikana sh17. 5 milioni ya umaliziaji wa jengo la maabara ya shule ya sekondari Bishop Hando ya Wilayani Mbulu.

Pia, Mnyeti amewapa zawadi ya sh1 milioni walimu wa shule hiyo na wanafunzi wakapewa magunia 100 ya mahindi ya chakula kwa kushika nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017.Aliendesha zoezi hilo kwenye ziara yake ya siku saba ya kutembelea halmashauri ya wilaya ya Mbulu ambapo atakagua na kuzindua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero na kuzungumza na wananchi.

Mnyeti akizungumza kwenye shule hiyo amemuagiza mkuu wa wilaya hiyo Chelestino Mofuga kuhakikisha maabara hiyo inakamilika ndani ya muda wa miezi mitatu.“Hata mimi niliwahi kuwa mkuu wa shule ya sekondari, natambua gharama za ujenzi zilivyo, hapa panahitajika sh40 milioni, sisi tumechangia sh17. 5 milioni sasa pambaneni mlimalize jengo hili,” alisema Mnyeti.

Mkuu wa wilaya hiyo Mofuga alimuhakikishia Mnyeti kuwa atafanikisha usimamizi wa umaliziaji wa maabara hiyo ndani ya miezi mitatu kama alivyoagiza.“Kupitia nafasi hii nakuagiza mtendaji wa kata ya Masqaroda na mtendaji wa kijiji kuendesha michango kwa wananchi ili tumalize jengo hili la maabara,” alisema Mofuga.Awali, mwalimu wa shule hiyo ya sekondari Bishop Hando, Samuel Surumbu alisema kiwango cha taaluma kwa wanafunzi kinafanikiwa kutokana na ufundishaji wa walimu na kuwepo kwa chakula shuleni.

Mwalimu Surumbu alisema pia wanasaidiwa kufundisha na walimu wengine wa kujitolea wanaofundisha masomo ya sayansi.Alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wa upungufu wa majengo ikiwemo ofisi za walimu, nyumba za walimu na bwalo la kulia chakula.Diwani wa kata ya Masqaroda Peter Tarmo alimshukuru Mnyeti kwa kuendesha zoezi hilo lililofanikisha upatikanaji wa fedha hizo zitakazosaidia umaliziaji wa jengo hilo la maabara.

Huu mzigo hivi sasa utakuwa mwepesi tofauti na hapo awali, tutajipanga na wananchi wangu na wilaya yetu kuhakikisha maabara hii inakamilika,” alisema Tarmo.

No comments: