Wednesday, February 7, 2018

PASIPOTI MPYA NI SALAMA ASILIMIA 100: UHAMIAJI


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu. IDARA ya uhamiaji nchini imewataka watanzania kupuuza habari zinazozagaa kuhusu uvumi wa pasipoti mpya kuwa zimechakachuliwa.

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala amesema wananchi wanatakiwa kupata taarifa sahihi kila mara juu ya kila jambo linalohusu maendeleo yao na mambo yanayoletea ustawi wa Taifa letu,sisi ndio wenye taarifa sahihi zinazohusu Mchakato mzima wa Pasipoti Mpya za Kielektroniki

Hivi karibuni Rais Dkt. John Magufuli wakati akizindua hati mpya za kusafiria alisema kumekuwapo na wahujumu wa mchakato huo ambao hawakufanikiwa kuiba sh. bilioni 400.Amesema kumekuwapo kwa watu waliozunguka kila kona na kutumia kila njama zote kupiga vita mchakato huo wakidhani watafanikiwa kuhujumu serikali.

Dkt. Anna Makakala amesema hatua hizo za kutoa na kueneza taarifa zisizo sahihi zinawaletea mkanganyiko wananchi na kudhoofisha mawazo na fikra chanya kwa Taifa lao.Amesema ni vyema jamii kutambua kuwa mchakato wa Pasipoti mpya ya kidigitali ni hatua kubwa kwa Taifa hili na si vyema kuutolea Taarifa zisizo sahihi, amewasihi wanahabari kupata taarifa kutoka katika vyanzo sahihi na kuzifikisha kwa walaji ambao ni Wananchi," 

Amesisitiza hatua ya mafanikio ya matumizi ya hati hizo hazitarudi nyuma kwa sababu ya kuwapo na taarifa zisizo sahihi zenye lengo la kupotosha ukweli wa mchakato huo.“Ni vyema jamii kuelewa kazi ya hati hizo ni kulinda usalama wa nchi yetu hivyo Uhamiaji tutaendelea kudhibiti mipaka ya Tanzania na kulinda usalama wa nchi kwa kuwezesha jamii na raia wa kigeni kufuata taratibu katika utokaji,ukaaji na uingiaji wa kila mmoja,” amesema Dkt. Makakala.

Amesema kila nchi yenye kuhitaji maendeleo ni muhimu kutumia hati ya kusafiria ya kielektroniki ili kufikia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.“Mabadiliko ya kidunia katika maendeleo yanatuonyesha wazi kuwa Taifa hili limefikia kuwa na hati za kisayansi na kiteknolojia hivyo katika hati mpya,mtu yeyote hataweza kutumia ujanja au kughushi na kutumika kwa matumizi yasiyo sahihi,” amesema Dkt. Makakala.

Amesema anaamini idara hiyo haitashindwa na wachache wanaokubali kutumika kuhujumu mchakato huo kwa maslahi binafsi kwakuwa kushindwa kwa mchakato huo ni kupunguza hadhi ya usalama wa nchi.

“Pasipoti ndio kitu kinachotuwezesha kudhibiti wanaoingia nchini na kutoka hiki ni kitambulisho cha raia sehemu yoyote duniani wenye Pasipoti za Tanzania ni mabalozi wa Tanzania mfumo huu utawezesha kudhibiti ujanja wote unaotumika kutakuwa na cheap na security features nyingi sifa ya Taifa letu dunia imeharibika lazima kufanya maamuzi kwa maslahi ya Taifa letu,” amesema.

Dk. Anna alisema kufanikiwa kwa mradi huo wa e-Immigration kwa gharama ya dola za Marekani milioni 57 imekuwa mwiba kwa vigogo walioondolewa Uhamiaji na sasa wanahaha kwa aibu wakidai kwamba gharama iliyotajwa ni kwa ajili ya mradi mradi mmoja tu wa e-Pasipoti.

“Ni wajibu wa kila mtanzania kuwa macho na wale wote wanaotumiwa na mafisadi kwa ajili ya kuichafua serikali kwakuwa imezuia na kupambana na uhujumu uliotaka kujitokeza,” amesema.

Amesema hati hizo zitawezesha waliopotelewa na hati zao kutumia mfumo wa kiteknolojia na kupakua app yake hata katika simu ya mkononi, hivyo kutambulika na kupewa msaada haraka kokote duniani.Amesema hati hiyo inaviwango vyote vya ubora wa kimataifa pia itatumika kama kitambulisho kwa nchi za Afrika Mashariki.

No comments: