Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha inafunga kamera katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi ili kudhibiti vitendo vya hujuma katika mifumo ya kampuni hiyo hususani kwenye Mapato.
Ametoa rai hiyo jijini Mwanza mara baada ya kuzindua mfumo mpya wa ukatishaji tiketi kwa njia ya kielektroniki katika Meli ya MV Clarias na kusisitiza kuwa matumizi ya mfumo huo mpya yaende sambamba na elimu stahiki kwa watumishi wanaoutumia mfumo huo katika kukatisha tiketi.
“Niwapongeze sana kwa hatua hii ya kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki katika utoaji huduma lakini niwatake sasa kuongeza kamera kwenye maeneo yote unapofanyika ukaguzi ili kudhibiti mianya yote inayoweza kujitokeza ya kuhujumu mapato ya kampuni” amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye shirika hilo ili liweze kupata faida na liweze kujitegemea na kuagiza kuwa kwa sasa kila fedha inayopatikana itumike vizuri sababu Shirika limeanza kupata faida.
Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), kutengeneza mfumo kama huo kwa ajili ya Shirika la Reli Nchini (TRL), ili kudhibiti uvujaji wa mapato.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabir Kuwe, amesema mfumo huo umetengenezwa na Wakala ili kuiwezesha taasisi hiyo kuthibiti mapato kwani mfumo huo utarahisisha Huduma kwani abiria ataweza kukata tiketi akiwa sehemu yoyote nchini.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL, Bw. Erick Hamis, amesema mfumo wa kielektroniki umeanza kwa meli moja ya MV Clarias inayofanya Safari zake kutoka Mwanza kuelekea kisiwa cha Ukerewe ambapo katika mpango wa baadae Kampuni inategemea kutumia mfumo huo kwenye meli zote za kampuni hiyo.
“Toka tuanze kutumia mfumo kumekuwa na ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 20, pia na kwenye matumizi ya mafuta hii inatupa ishara kuwa mfumo huu utatusaidia kidhibiti mapato mengi yaliyokuwa yakipotea kwenye tiketi”amesema Hamissi.
Ameongeza kuwa kampuni imejiwekea mpango wa miaka miwili wa kukarabati meli Tisa za kampuni hiyo ambapo mpaka sasa meli Tatu zimeshakarabatiwa na kuanza kazi wakati hatua ya kuanza ukarabati kwa meli zilizobaki uko kwenye hatua mbalimbali za manunuzi.
Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ukatishaji tiketi katika kampuni hiyo umegharimu kiasi cha shilingi takriban milioni 50.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mfumo wa ukatishaji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki katika Meli ya MV. Clarias inayotoa huduma kati ya Mwanza na Ukerewe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akikata tiketi ya kieletroniki mara baada ya kuzindua mfumo wa tiketi hizo katika Meli ya MV Clarias, mkoani Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamis, wakati akikagua ukarabati wa Meli ya MV. Clarias, mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment