Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Ujumbe wa Mawaziri wawili
kutoka Malawi na kuzungumza kuhusu uwezekano wa Malawi kupata Gesi
Asilia kutoka Tanzania na Uendelezaji wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe
kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji umeme.
Ujumbe
wa Malawi uliongozwa na Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey
Masi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa ambao
waliambatana na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe na wataalam kutoka
Taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara zao.
Waziri
Kalemani alikutana na ujumbe huo Februari 12, 2018 katika Ofisi za
Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam ambapo alielezwa dhumuni la ziara
hiyo ya Mawaziri hao wawili kutoka nchini Malawi.
Akizungumza
katika mkutano huo, Waziri wa Nishati wa Malawi, Aggrey Masi alisema
kuwa Malawi inaupungufu mkubwa wa nishati ya umeme na kwamba jitihada
mbalimbali zinafanyika kuhakikisha kiwango cha uzalishaji umeme
kinaongezeka.
Alisema
umeme unaozalishwa nchini humo kwa sasa ni Megawati 140 pekee huku
idadi ya watu ikiwa ni milioni 17 kiasi ambacho alisema kimeshindwa
kukidhi mahitaji.
“Sasa
hivi tumebaki na megawati 140 peke yake, hali siyo shwari; suluhisho la
haraka linahitajika ili kuweka mambo sawa. Imani yetu ni kwa Tanzania
kutazama namna ya kusaidia katika hili,” alisema.
Alibainisha
kwamba chanzo kikuuu cha uzalishaji wa umeme nchini humo ni maporomoko
ya maji na kwamba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, chanzo hicho
kimeshindwa kuzalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.
Aliongeza
kwamba Serikali ya Malawi imeamua kuwa na vyanzo mbadala vya kuzalishia
umeme ikiwemo Gesi Asilia hata hivyo alisema hakuna Gesi Asilia
inayozalishwa nchini humo na kwamba matarajio yao ni kupata Gesi Asilia
kutoka nchini Tanzania.
“Tumefarijika,
tumepokelewa vizuri, lengo la ujio wetu ni kubaini uwezekano wa kupata
Gesi Asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme,” alisema Masi.
Alisema
kwamba baada ya tathmini waliyoifanya wamebaini kwamba chanzo cha
haraka kinachoweza kuwasaidia kuvuka kwenye upungufu mkubwa wa umeme
uliyoikumba nchi hiyo kwa sasa ni Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania.
Aliongeza
kuwa tayari mwekezaji amepatikana ambaye atazalisha umeme kwa kutumia
Gesi Asilia na kwamba atajenga mitambo yake kwenye eneo la Kalonga
mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Kwa
upande wake Waziri Kalemani alisema suala hilo linaweza kujadiliwa
baada ya wataalam wa Tanzania kujiridhisha uwezekano wake.
“Tupo
tayari kushirikiana, kinachohitajika hapa ni majadiliano ya kitaalam na
wataalam wetu waliopo hapa ili kuelewa mwelekeo,” alisema Waziri
Kalemani.
Dkt.
Kalemani aliwasisitiza wataalam hao kabla hawajafanya majadiliano
wanapaswa kuelewa mambo makuu matatu ambayo wingi wa Gesi Asilia iliyopo
kwa sasa, matakwa ya Sera ya Nishati na namna ambavyo Gesi hiyo inaweza
kusafirishwa hadi huko Kalonga.
“Je
tunayo gesi ya kutosha kugawana ama ni ya kutosha kwa matumizi yetu tu?
Je Sera inaruhusu suala hilo? Na kama masuala hayo yanakubalika, Je ni
vipi tutaifikisha hiyo Gesi huko mpakani?” alihoji Dkt. Kalemani.
Aliueleza
ujumbe huo kuandaa mpango wa ombi lao kimaandishi pamoja na kuandika
ombi rasmi na kuwasilisha katika utaratibu maalum wa Kiserikali ili
majadiliano yafanyike.
Aidha,
suala la Uendelezaji wa pamoja wa Bonde la Mto Songwe, Mawaziri hao kwa
pamoja walikubaliana kupitia taarifa ya Tume ya Uendelezaji wa Bonde
hilo ambayo inaundwa na nchi hizo mbili ili kubaini hatua za kuchukua
kwenye kipengele cha kuzalisha umeme.
Miradi
inayotarajiwa kutekelezwa katika bonde hilo ni pamoja na ujenzi wa
Bwawa la kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 180 ambazo zitagawanya sawa
kwa nchi hizo, kilimo cha umwagiliaji, (hekta 6,200) usambazaji wa maji
kwa wananchi, ujenzi wa miundombinu ya jamii (bararabara, shule, na
vituo vya afya).
Miradi
mingine ni uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati, uvuvi, utalii na
uboreshaji wa mazingira, hususan kuimarisha kingo za mto ambao ni mpaka
wa Tanzania na Malawi.
Mawaziri
kutoka Malawi mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya majadiliano kuhusu masuala ya Nishati
na mwenyeji wao Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Medard Kalemani
(hayupo pichani). Kushoto ni Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini,
Aggrey Masi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa.
Waziri
wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) wakati wa
mkutano wa kujadili masuala ya Nishati na Mawaziri kutoka Malawi (hawapo
pichani).
Ujumbe
wa Mawaziri kutoka Malawi ukiendelea na majadiliano wakati wa mkutano
na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani). Kutoka
kulia ni Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi, Waziri wa
Viwanda, Biashara na Utalii, Henry Mussa na Balozi wa Malawi nchini,
Hawa Ndilowe.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza jambo wakati wa
mkutano na Mawaziri kutoka Malawi. Kulia ni Waziri wa Maliasili, Nishati
na Madini wa Malawi, Aggrey Masi.
Viongozi
kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake wakiendelea na
majadiliano. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.
Hamis Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli,
Mhandisi Innocent Luoga, Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Ally Ubwa, Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba na Kamishna Msaidizi
anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) katika picha ya pamoja na
Ujumbe wa Mawaziri kutoka Malawi. Kutoka kulia ni Balozi wa Malawi
nchini, Hawa Ndilowe, Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Henry
Mussa. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Tanzania, Dkt.
Hamis Mwinyimvua na Waziri wa Maliasili, Nishati na Madini, Aggrey Masi
mara baada ya kumalizika kwa majadiliano ya masuala ya Nishati.
Ujumbe
kutoka Malawi ukiendelea na majadiliano wakati wa mkutano wa kujadili
masuala ya Nishati na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo
pichani).
No comments:
Post a Comment