Monday, February 5, 2018

WADAU HAKI JINAI WAHIMIZWA KUSHIRIKIANA KUTOA HAKI KWA WAKATIJaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akifunga Kongamano la Wadau wa Haki Jinai lililofanyika katika Kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, katika maneno yake ya kufunga, Mhe. Jaji Wambali amewataka Wadau kuendeleza ushirikiano ili kuiwezesha Mahakama kutoa haki kwa wakati.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto (IJA) (aliyesimama mwenye tai akitoa maelezo mafupi kwa Mgeni rasmi juu ya Mafunzohayo kabla ya kufunga rasmi Kongamano hilo.
Mgeni rasmi, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akikabidhi cheti cha Ushiriki kwa mmoja wa Washiriki wa Kongamano hilo, Mhe. Jaji Firmin Nyanda Matogolo.
Mgeni rasmi, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu na baadhi ya Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika Kongamano.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Washiriki wa Kongamano. (Picha na Ibrahim Mdachi, IJA)

Na Mary Gwera, Mahakama

WADAU wa Haki Jinai nchini wameazimia kwa pamoja kukuza ushirikiano baina yao katika kushughulikia uhalifu wa makosa yanayovuka mipaka kuanzia eneo la Ukusanyaji wa taarifa, Upelelezi, Uendeshaji wa Mashtaka pamoja na Mashauri ya namna hiyo.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita Februari 02, 2018 na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo katika mahojiano maalum mara baada ya kuhitimishwa kwa Kongamano la Wadau wa Haki Jinai lililofanyika katika Kituo kipya cha kisasa cha Mafunzo na Habari kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

“Katika Kongamalo hilo ambalo lilihusisha Wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali, Jeshi la Magereza, Wizara ya Katiba na Sheria na wengineo tumeazimia pia mamlaka zinazofanya upelelezi ziwe na Maabara za kufanyia Upelelezi wa Kisayansi ‘Forensic Science’ ili kuharakisha uendeshaji wa kesi na hatimaye haki iweze kupatikana kwa wakati,” alisema Mkuu wa Chuo huo ambaye pia alikuwa Mwezeshaji katika Mafunzo hayo.

Mhe. Kihwelo anasema kuwa kwa sasa wenye Maabara hizo ni Polisi pamoja na TAKUKURU, lakini wengine wote wanategemea Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na kuongeza kuwa Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ipo kwenye mchakato wa kuanzisha Maabara yao ya uchunguzi.

Aidha; Wadau wa Kongamano hilo waliazimia kwa pamoja kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iendelee kutoa majibu kwa wakati ili kuharakakisha haki kupatikana kwa wakati.

Mafunzo hayo ya Siku tano yalifanyika kwa mara ya kwanza katika Kituo Kipya cha Mafunzo na Habari za Kimahakama yalijikita katika Mada ya ‘Sheria za Uhalifu wa Makosa yanayovuka Mipaka’ ambapo katika Mada hii Sheria zilizoangaliwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Kimtandao ‘Cybercrime’, Makosa yanayohusu miamala ya fedha kwa njia ya Kimtandao pamoja na Sheria ya Madawa ya Kulevya na makosa yanayoundwa na Sheria hiyo.

Kongamano hili lililofunguliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma Januari 29, 2018 lililenga kuwakutanisha Wadau wa Haki Jinai ili kujadili changamoto zilizopo katika sheria hizokatika maeneo ya upelelezi, uendeshaji mashtaka pamoja na ubadilishanaji wa Wahalifu na kuwakutanisha kwa lengo la kujenga Mtandao wa Wadau na kukuza ushirikiano.

Aidha; Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo anaongeza kuwa Mafunzo hayo yaliyomalizika ni miongoni mwa mafunzo mengi zaidi yatakayofuatia huku yakishirikisha Wadau tofauti tofauti.

No comments: