Friday, February 16, 2018

MADALALI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUWA NA CHETI CHA UMADHUBUTI WA KAZI

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

MAHAKAMA nchini Tanzania, imewataka madalali wa Mahakama kuwa na cheti cha umadhubuti katika kazi hiyo toka Chuo cha Uongozi wa Mahakama ama Taasisi inayotambuliwa na kamati ya uteuzi.

Jaji kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Frerdnand Wambali amesema haya leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau mbalimbali wa Mahakama wanaoratibu na kusimamia utekelezaji wa amri za mahakama wakiwamo madalali.

Lengo la kongamano hilo ni kujadili rasimu ya mtaala maalumu wa kutolewa mafunzo kwa watu wanaofanya shughuli za udalali na usambazaji wito na amri za Mahakama.

Kongamano hilo limeratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Rushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania lengo ni kujadili rasimu ya mtaala maalum wa kutolewa mafunzo kwa watu wanaofanya shughuli za udalali na usambazaji wito na amri za Mahakama.

Akizungumza, Jaji Wambali amesema Mahakama inatambua madalali wa Mahakama na wale wanaopaswa kupelekwa hati za kuitiwa kwenye mashauri wanawajibu wa kuhakikisha amri mbalimbali zinazotolewa na mahakama hasa katika mashauri ya madai zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

Alisema kuwa mwaka 1997 zilitungwa kanuni kuhusu uteuzi, maslahi na usimamizi wa madalali wa mahakama na kwamba madalali wengi wanatekeleza majukumu yao bila ya kuwa na mafunzo rasmi ya kuwafanya wapate ujuzi wa utekelezaji wa kazi zao ukiacha ukiacha yale ya dharura yaliyofanyika mwaka 2003.

Amesema, hali hiyo imekuwa ikisababisha malalamiko kwa wadaawa na umma kuhusu mapungufu mbalimbali ikiwamo ukiukwaji wa utaratibu na ukosefu wa maadili katika utekelezaji wa Kazi zao.

Amebainisha hakuna shaka kuwa madalali wale waliopata kazi na kufanya usahili mbele ya kamati ya uteuzi, maslahi na usinamizi wa nidhamu ya maadili kwa ajili ya kutathmini sifa,uelewa na uwezo wao katika kutekeleza majukumu yao bado wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni.

Ameeleza kutokana na changamoto ambazo zilikabili wadau wa Mahakama ilionekana upo umuhimu wa kufanya marekebisho ya namna ya kuwapata madalali, kusimamia nidhamu na maadili, maslahi na jinsi ya kutekeleza majukumu yao.

" Ni kwa sababu hiyo sheria ndogo namba 363 ya 2017 ilitungwa na kuchapishwa Septemba 22,mwaka 2017 na kuwa sheria hii ilifuta sheria ya 1997, ni matumaini yangu sheria hii itakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi. "amesema Jaji Kiongozi.

Aidha Jaji Kiongozi ametoa mwito kwa washiriki wa mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku mbili, mpaka kesho, kushiriki kikamilifu na kwa dhati katika mafunzo hayo na kutoa maoni ya kuboreaha mtaala huo uliondaliwa bila kujali ngazi zao.

Amesema katika mtaala huo kutakuwa na mambo mbalimbali ikiwamo utaratibu muhimu wa uendeshaji wa mashauri ya madai, aina za amri za Mahakama zinazoweza kutolewa na matumizi ya teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama).

Pia, mahusiano kati ya madalali na maofisa wa mahakama na vyombo vingine vya dola, maadili ya kimahakama na mapambano dhidi ya rushwa pamoja na gharama zinazopaswa kutozwa kwa huduma za mahakama na watakazotoa madalali.

No comments: