Friday, February 16, 2018

KANALI NDAGALA AKABIDHI MABATI 280 KWA WALIMU 14 WALIOSTAAFU KAKONKO


Na Rhoda Ezekiel Kigoma,

MKUU wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amekabidhi mabati 280 kwa wastaafu 14.

Amekabidhi mabati hayo kwa niaba ya kamati tendaji ya Chama cha Waalimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Kakonko ambayo ni zawadi kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa kipindi chote cha utumishi wao.

Akikabidhi mabati hayo juzi kwa wastaafu katika ofisi za CWT wilayani Kakonko Kanali Ndagala aliwapongeza wastaafu hao na kuwasisitiza kutumia zawadi waliyopewa kukamilisha nyumba zao au kuanzisha biashara itakayowasaidia kuendeleza maisha yao.

Amesema kila mhsataafu amepewa mabati 20 kama zawadi za pongezi kutokana uadilifu.Pia pamoja na kujituma wakati wakiitumikia Serikali katika sekta ya elimu ambapo chama hicho kimetambua utendaji wao uliotukuka.

“Niwapongeze kwa kumaliza salama muda wenu, mnapoenda kuanza maisha mapya na mazuri, huu ni mwanzo mzuri kama hujamalizia kibanda kamalizie."Kama tayari ni vizuri kujenga kibanda cha biashara au kufuga ilikuweza kujikimu kwa kipindi hiki maana kuna maisha baada ya kustaafu,”, amesema Kanali Ndagala.

Aidha ametoa mwito wa kujitoa na kuwaomba watumishi wanapokuwa kazini wajiandae kustaafu kwani kustaafu si mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha mengine uraiani na fursa ni nyingi endapo watazitumia vizuri.Amewataka kutokata tamaa kutokana na changamoto zinazojitokeza kazini kwani Serikali inatatua changamoto moja hadi nyingine na kuomba ushirikiano udumishwe ndani ya chama cha walimu.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Kakonko Tumaini Daniel amewaomba walimu wastaafu kuwakumbusha walimu waliopo kazini kujituma wakati wa kazi na kuiomba halmashauri itenge bajeti ya kuwarudisha makwao wastaafu baada ya kustaafu na Halmashauri iwaingize waalimu kwenye bajeti ya 2018/19 ili wapande madaraja kwani kuna waalimu zaidi ya 400 wanaotakiwa kupanda madaraja.

Mmoja wa wastaafu Masuhuko Magwaya aliyekuwa akifundisha Shule ya Msingi Bukiriro alieleza kufurahishwa na zawadi hizo walizopewa.Amewaomba walimu waliopo kazini wafanye kazi kwa uadilifu na kujitoa kwa moyo katika kuhakikisha wanatoa elimu bora kwani wanafunzi hao ndio tegemeo la kesho.

Mninga Lameck mstaafu kutoka Shule ya Msingi Kabingo amewasisitiza walimu kufanya kazi kwa kujitoa pia watambue kazi ya ualimu ni wito na kuwataka kutotanguliza taama za kutopenda malipo kabla ya kazi ili kujengea heshima na kuweza kustaafu vizuri.
 MKUU wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikabidhi mabati 280 kwa mmoja wa wastaafu kati ya 14.Ndagaka amekabidhi mabati hayo kwa niaba ya kamati tendaji ya Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kakonko ambayo ni zawadi kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa kipindi chote cha utumishi wao.

Baadhi ya Wastaafu hao hao wakimsikiliza MKUU wa Wilaya ya Kakonko Kanali (hayupo pichani),Hosea Ndagala mara baada ya kuwakabidhi mabati 280

No comments: