Sunday, February 4, 2018

MAADHIMISHO YA 19 YA KUMBIKIZI YA PROF. HUBERT KAIRUKI

Marehemu Prof. Hubert Clemence Mwombeki Kairuki na mkewe Mama Kushubila Kairuki
Utangulizi: 
Hospital ya Kairuki (KH), Shule ya Uuguzi Kairuki (KSN) na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), kwa pamoja vitashiriki katika maadhimisho ya 19 ya kumbukizi ya Marehemu Prof. Hubert Clemence Mwombeki Kairuki, muasisi wa taasisi mama inayosimamia taasisi hizo yaani Shirika la Afya na Elimu la Kairuki (KHEN). 
Kumbukizi hiyo itafanyika kwa juma moja kuanzia tarehe 1 Februari 2018 na kufika kilele chake tarehe 6 Februari 2018, kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kama ifuatavyo: 
* Kuweka jiwe la Msingi kwenye kituo cha kusaidia watu wenye matatizo ya kupata ujauzito kwa njia ya kawaida Bunju. 
 *Kuanzisha kliniki ya mama, baba na mtoto. 
 *Kutoa huduma za afya bila malipo kwa wananchi. 
 *Uchangiaji Damu/Blood Donation.
 *Mhadhara wa Tisa wa Kitaaluma wa kumbukizi ya Prof. Hubert Kairuki. 
 *Mashindano ya kitaaluma baina ya wanafunzi wa HKMU na KSN. 

 1.Uwekaji jiwe la Msingi kituo cha Bunju: 
 Hospitali ya Kairuki itaweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha kusaidia watu wenye matatizo ya kupata ujauzito kwa njia ya kawaida katika tawi lao jipya huko Bunju. Jiwe la msingi la kliniki hiyo litawekwa na Mheshimiwa Ally Salum Hapi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, tarehe 5 Februari 2018, saa tano asubuhi. 
 Ujenzi wa kituo hiki utakapokamilika inatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa familia ambazo hazijabahatika kupata mtoto kwa njia ya kawaida. Michoro kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki ipo katika hatua za mwisho kwenye taasisi husika kwa jili ya kupata idhini ya ujenzi. Kairuki Hospitali tayari inayo wataalamu wa kuweza kuendesha kituo cha hicho pale ujenzi wake utakapokamilika.

 2. Utoaji wa Huduma za Afya bila Malipo: 
 Sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi la kituo hicho, Kairuki Hospitali itafanya zoezi la utoaji wa huduma za afya za msingi pamoja na ushauri bila malipo. Zoezi hili litafanyika huko huko Bunju kuanzia tarehe 4 hadi 6 Februari 2018. Baadhi ya huduma za msingi zitakazotolewa ni pamoja na kupima shinikizo la damu, Body Mass Index (BMI) yaani uwiano wa urefu na unene wa mtu na kutoa ushauri. Utoaji wa huduma za afya utaanza saa 3 kamili asubuhi hadi saa 10 jioni, kwa siku zote tatu mfululizo. 

 3. Uchangiaji Damu/Blood Donation: 
 Pamoja na upimaji wa afya bila malipo pia kutafanyika zoezi la uchangiaji damu. Zoezi hili litafanywa kwa kushirikiana kati ya Kairuki Hospitali na Taasisi ya Damu Salama. Wananchi wa maeneo ya Bunju, wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Kairuki Hospitali na Shule ya Uuguzi Kairuki watashiriki katika zoezi la uchangiaji damu. Zoezi hili litafanyika kwa siku tatu mfululiza kuanzia tarehe 4 hadi 6 Februari 2018. Utoaji wa huduma ya uchangiaji damu utaanza saa 3 kamili asubuhi hadi saa 10 jioni. 

 4. Mashindano ya Kitaaluma (Academic Competition): 
 Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki watashiriki katika shindano la kupima ujuzi wao juu ya mambo ya msingi katika taaluma ya Afya, maswali ya ufahamu kuhusu Tanzania, maisha ya Prof. Hubert Kairuki, Jiografia na jamii kwa ujumla. 

 5. Mhadhara wa Tisa wa Kitaaluma wa Kumbukizi ya Profesa Hubert Kairuki (The Ninth Hubert Kairuki Memorial Lecture): 
 Hili ni tukio la mwisho katika kilele cha wiki ya kumbukizi ya muasisi. Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki kitasimamia shughuli ya uendeshaji wa mhadhara utakaofanyika tarehe 6 Februari 2018, kuanzia saa 8 kamili mchana. Mhadhara utafanyika katika ukumbi wa Chuo wa mihadhara. 
 Mada ya mhadhara itakuwa Maono ya Prof. Hubert Kairuki yanayotumu: Umuhimu wake katika utoaji wa Huduma za Afya Barani Afrika yaani Hubert Kairuki's Enduring Vision: Its Impact to the provision of heath care services in Africa.  Mtoa mada atakuwa ni Prof. Malise Kaisi. Kabla ya uwasilishwaji wa mhadhara huo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo ndugu John Ulanga, atawasilisha taarifa juu ya mipango ya uendelezwaji wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki iliyoko Boko na Mfuko wa Elimu (Endowment Fund). 

 Maisha ya Prof. Hubert Kairuki 
 Profesa Hubert Clemence Mwombeki Kairuki alizaliwa Juni 24, 1940 huko Bukoba, mkoani Kagera. Alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kigarama na ya Kati (middle school) katika shule ya Mugeza. Alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Kahororo, Ilboru na Old Moshi, kati ya mwaka 1947 na 1962. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere mwaka wa 1963, kwa ajili ya mafunzo ya Udaktari na kuhitimu mwaka 1968. 
 Mwaka 1974, alihitimu shahada ya uzamili ya udaktari yaani Master of Medicine (M.Med) katika magonjwa ya akina mama (Obstestrics na Gynecology) katika Chuo Kikuu cha Makerere. Baadae alijiunga na Royal College huko London Uingereza na kufanikiwa kuwa mjumbe katika jumuiya ya madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama (MRCOG na baadea FRCOG). 
 Kazi: 
 Mwaka wa 1968/69, Profesa Kairuki alifanya kazi kama Daktari wa Matibabu wa Ndani katika Hospitali ya Ocean Road, na tangu 1969 hadi 1975, alikuwa Daktari katika Hospitali ya Ndolage huko Bukoba. Mnamo mwaka wa 1975; alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Mhadhiri katika Kitivo cha Tiba na Mshauri/consultant katika Hospitali ya Muhimbili. Pia alikuwa mshauri katika hospitali zifuatazo:- Hindu Mandal, Aga Khan, na Burhan zilizopo katika jiji la Dar es Salaam. Ujasiriamali Mwaka 1982 Prof. Kairuki aliacha kazi Muhimbili Hospitali na kuanza kufanya kazi za matibabu binafsi Mikocheni jijini Dar es Salaam, chini ya mwavuli wa taasisi ya Assemblies of God (TAG). 
 Mnamo tarehe 17 Machi 1987, Prof. Kairuki alianzisha Hospitali ya TAG Mikocheni (yenye vitanda 30 na wafanyakazi 60). Mnamo 1992 Hospitali ya TAG Mikocheni ilibadilisha jina na kuitwa Mission Mikocheni hospital, ambayo sasa inaitwa Kairuki Hospitali. Mnamo mwaka 1997 Prof. Kairuki alianzisha Mikocheni International University kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari na wauuguzi nchini Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla. Miaka miwili (2) baada ya chuo kuanzishwa Prof. Kairuki alifariki dunia (6.2.1999) jina la chuo lilibadilishwa na kuwa Hubert Kairuki Memorial University. 

 Miaka 19 tangu Prof. Kairuki alipofariki dunia: 
 Wakati hospitali inaanzishwa ilikuwa na uwezo wa kupokea wagonjwa wa nje 200 na wagonjwa wa ndani 30 kwa siku, kwa sasa hospitali ina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje zaidi ya 700 kwa siku na wagonjwa wa ndani 150 kwa siku. Wakati muasisi alipofariki, Chuo kilikua kinapokea wanafunzi 5 hadi 30 katika fani ya udaktari na uuguzi kwa sasa:- 
 KSN - uuguzi ngazi ya astashahada 290 
 HKMU - Daktari wa binadamu 1965 - 
Wauguzi ngazi ya astashahada 224 - 
Masomo ya uzamili 30
 Hivyo jumla ya wanafunzi waliopo HKMU wanafikia 1509. 

Chuo kimeweza kutoa wahitimi wenye taalima ya Tibabu na Uuguzi na wameweza kupata ajiri kwenye taasisi mbalimbali ndani ya nchi na nje ya nchi.

No comments: