Sunday, February 4, 2018

KAMISHNA MKUU WA TRA AMSIMAMISHA KAZI MENEJA WA TRA MKOA WA MARA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyekaa mbele) akiongea na kutoa maagizo kwa Meneja wa TRA Wilaya ya Bunda Mkoani Mara pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali mara alipotembelea ofisi ya TRA Wilayani hapo ili kujionea namna ukusanyaji mapato unavyofanyika mapema 3 Februari, 2018.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia) akimsisitizia jambo Mfanyabiashara wa duka la nguo Wilayani Bunda Mkoani Mara kuhusu suala la umuhimu wa kutumia mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti (EFD) mara alipofanya ukaguzi wa mashine hizo katika baadhi ya maduka Wilayani hapo 3 Februari, 2018.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia) akikagua taarifa ya mauzo ya siku ya Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti (EFD) toka kwa Wafanyabiashara wa duka la vifaa vya nyumbani Wilayani Bunda Mkoani Mara mara alipofanya ukaguzi wa mashine hizo katika baadhi ya maduka Wilayani hapo 3 Februari, 2018.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa TRA Wilaya ya Bunda Mkoani Mara pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo mara alipotembelea ofisi ya TRA Wilayani hapo ili kujionea namna ukusanyaji mapato unavyofanyika mapema 3 Februari, 2018.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA).Na: Veronica Kazimoto-Bunda, 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere amemsimamisha kazi Meneja wa TRA Mkoa wa Mara Ndg. Nicodemus Mwakilembe kutokana na uzembe wa kutosimamia vizuri matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwa wafanyabiashara wa mkoani kwake. 

Uamuzi huo umetokana na ziara ya kushtukiza ya kukagua matumizi ya EFD aliyoifanya Kamshina Mkuu wa TRA kwenye baadhi ya maduka ya biashara Wilayani Bunda Mkoa wa Mara. Akizungumza mara baada ya ziara yake, Kamishna Mkuu Kichere alisema Meneja huyo ameonyesha uzembe wa hali ya juu kwani kuna wafanyabishara wengi mkoani kwake ambao walishalipa fedha kwa ajili ya kupata mashine za EFD lakini mpaka sasa hawajapatiwa mashine hizo. 

"Katika ziara yangu nimegundua kwamba, wapo wafanyabiashara ambao walikwisha kulipia mashine tangu mwaka 2013, 2014 na 2015 lakini mpaka sasa bado hawajapatiwa mashine za EFD na wamekuwa wakitumia mwanya huo kama kinga ya kutochukuliwa adhabu na TRA wakati Meneja wa Mkoa yupo na hachukui hatua zozote. Huu ni uzembe uliopitiliza na kamwe siwezi kuuvumilia," alisema Kichere. 

Kutokana na uzembe huo, Kamishna Mkuu Kichere amewaagiza Mameneja wote wa TRA nchi nzima pamoja na majukumu mengine, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu matumizi ya mashine za EFD katika mikoa yao na amesema hatasita kumuwajibisha Meneja yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. 

Ziara hiyo ya kushtukiza imewawezesha wafanyabiashara waliokuwa wamelipia mashine za EFD miaka ya nyuma, kupata mashine hizo na kufundishwa jinsi ya kuzitumia ambapo wengine wamejitokeza kununua mashine hizo kwa ajili ya biashara zao. Kamishna Mkuu aliongeza kuwa, mashine za EFD zina umuhimu sio tu kwa Serikali kupata mapato bali kwa wafanyabiashara husika kwani huwawezesha kutunza kumbukumbu, kujua mwenendo halisi wa biashara zao na hatimaye kulipa kodi stahiki. 

Sambamba na hayo, Kichere amewataka wananchi wasiishie tu kudai risiti bali wakishachukua risiti hizo wazikague ili kuthibitisha uhalali wake na usahihi wa kiasi cha pesa walicholipa. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku 5 ambapo amepata nafasi ya kutembelea Vituo vya Forodha mipakani na ofisi mbalimbali za mamlaka hiyo pamoja na baadhi ya wafanyabiashara akikagua matumizi ya mashine za EFD.

No comments: