Thursday, February 8, 2018

JKCI yafanya semina ya afya ya moyo,magonjwa yasiyoambukiza kwa Wabunge mjini Dodoma.

Na Mwandishi wetu, Dodoma.

08/02/2018 Wazazi wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo
zote zinazotakiwa ili waweze kuepukana na magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.

Rai hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia
wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na wabunge
waliohudhuria semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza
iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo
ilifanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.

Waziri Ummy aliwaomba wabunge hao kila wanapokutana na wananchi
kupitia mikutano ya hadhara wawasisitize umuhimu wa kuwapeleka watoto
wao katika vituo cha afya ili wakapate chanjo zinazohitajika kwa
wakati.

Aidha Waziri huyo alisema kuwa matibabu ya moyo pamoja na magonjwa
mengine yasiyoambukiza ni ya gharama kubwa na kuwaomba wabunge hao
kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao
utawasaidia kupata matibabu katika Hospitali zote nchini ikiwemo JKCI
na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika hatua nyingine Mhe. Ummy aliwataka wakurugenzi wa Taasisi
zingine kuiga mfano wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Prof. Mohamed ambaye kupitia uongozi wake na jitihada zake
binafsi Taasisi hiyo imeweza kutoa huduma bora na kuwahudumia wananchi
vizuri katika matibabu ya moyo na hivyo kuokoa maisha ya watanzania
wengi.

“Katika utendaji kazi wa Taasisi hii tunaona juhudi binafsi za
kiongozi ambaye kwa jitihada zake amewatumia marafiki aliosoma nao
na kufanya nao kazi katika nchi mbalimbali kuja nchini kutoa mafunzo
kwa wataalam wetu na huduma za matibabu magumu ya moyo ambayo sisi
peke yetu tusingeweza kuyafanya kutokana na uchanga tulionao”, alisema
Waziri Ummy .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii
Mhe. Peter Serukamba aliomba katika kikao cha Bunge la Bajeti wabunge
wapewe semina kama hiyo ambayo itaenda sambamba na upimaji wa
magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo moyo, saratani za matiti na shingo ya
kizazi, tezi dume na kisukari.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi
aliwasisitiza wabunge kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara
ili kama watakutwa na matatizo waweze kupata matibabu kwa wakati,
kufanya mazoezi na kuepuka kula vyakula ambavyo vitawaepusha kupata
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Katika semina hiyo ya siku moja mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwa ni
pamoja na Shinikizo la damu na dalili zake na tiba , kiharusi, tezi
dume na wanawake kukoma kwa hedhi kwa wanawake.
 Mbunge wa Lupa Mhe. Victor Mwambalaswa akiwasisitiza wabunge wenzake umuhimu wa kupima afya zao hasa tezi dume kwa wanaume wakati wa semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo ilifanyika jana  katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
 Mbunge wa  Bunda mjini  Mhe. Ester Bulaya akieleza jinsi anavyoridhishwa  na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na JKCI ambayo ilifanyika jana  katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akielezea mpango wa Serikali kupitia Hospitali za mikoa wa kusomesha madaktari bingwa wengi ili kuweza kukabiliana na uhaba wa wataalam  hao wakati wa  semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo ilifanyika jana   katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Daktari wa Bunge Jeminian Temba mara baada ya kumalizika kwa semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo ilifanyika jana   katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma. Katikati ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Yona Gandye.
 Wabunge wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) akielezea kuhusu dalili za shinikizo la damu na tiba yake wakati wa  semina ya afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo ilifanyika jana  katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.Picha na JKCI


No comments: