Thursday, February 8, 2018

JAFO ASHUSHA NEEMA YA LAMI CHANG’OMBE, AMFAGILIA MAVUNDE KWA UCHAPAKAZI WAKE



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akiwa na viongozi mbalimbali katika uzinduzi wa Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo wa Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
jiwe la msingi la soko la Chang'ombe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akizungumza katika uzinduzi wa Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo wa Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk.Binilith Mahenge akizungumza katika uzinduzi wa Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo wa Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde akizungumza katika uzinduzi wa Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo wa Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
Baadhi ya bidhaa zilizopo soko la Chang'ombe
Soko lenyewe la Chang'ombe
Viongozi mbalimbali katika uzinduzi wa Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo wa Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
Wafanyabishara wa Soko la Chang'ombe Manispaa ya Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akitembelea soko la Chang'ombe mara baada ya kuzindua.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akisalimiana na wananchi na wafanyabiashara wa soko la Chang'ombe.




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo, amemfagilia Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo kwa wananchi wake, huku akiuagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha katika bajeti yao ya mwaka 2018/19 wanaingiza kwenye mpango ujenzi wa barabara ya lami Chang’ombe hadi Chuo cha Mipango.

Jafo ameyasema hayo leo alipokuwa anazindua soko jipya la kisasa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo kata Chang’ombe lililojengwa na Serikali kwa kusaidiana na wafanyabiashara na Mbunge Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana.

Ujenzi wa soko hilo ulianza mwaka 2017 na kukamilika mapema mwaka huu na litakuwa na wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali takribani 342 na limegharimu kiasi cha Sh.Milioni 70.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Jafo amesema katika ziara zake za miradi ya maendeleo alizotembelea katika Manispaa ya Dodoma, Mbunge Mavunde ameonekana kushiriki katika kila sekta kwa kusaidiana na wananchi.

“Katika kila taarifa ya mradi wa maendeleo inayosomwa,unaonesha Mbunge wenu Mavunde amechangia kwa kweli nimpongeze sana kwa kushiriki kuleta maendeleo kwa wananchi wake, ni mchapakazi.Nawapongeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 mlilamba dume kila eneo ninaloenda nakuta nyayo zake, Naahidi kumpa ushirikiano wa kutosha,”amesema jafo

Amesema katika ujenzi wa soko hilo Mbunge huyo amesaidiana na wananchi na kufanikisha kukamilisha ujenzi wake na kuahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya Dodoma ili iendane na hadhi ya Makao Makuu ya nchi.

Waziri Jafo amesema Serikali inawekeza miundombinu ya hali ya juu katika mkoa wa Dodoma ikiwemo mtandao wa barabara za lami katika maeneo mbalimbali pamoja na taa za barabarani ikiwa ni pamoja na ujenzi wa dampo la kisasa.“Kwa kuwa serikali inahamia Dodoma hivyo basi miundombinu mbalimbali lazima iendelee kujengwa na kurekebishwa,” Amesisitiza Mhe. Jafo

Aidha Waziri jafo amewapongeza wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa kukamilisha ujenzi wa soko la kisasa na kwamba limejengwa kwa gharama nafuu sio kama masoko mengine yanayojengwa kwa gharama kubwa.

Pia ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge na Mkurugenzi wa Manispaa Godwin Kunambi kwa jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi.

Amemuagiza Mkurugenzi Kunambi kukamilisha masoko mbalimbali pamoja na kuanza kutumika kwa machinjio ya kuku yaliyopo soko la majengo ipasavyo kwa kuwa kuna taarifa kuku wanaenda kuchinjwa maeneo mengine na kuacha machinjio ya eneo hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mavunde amesema ujenzi wa soko hilo ni ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 na kwamba yataendelea kujengwa masoko ya kisasa yanayoendana na hadhi ya Makao Makuu ya Nchi.

“Pia kipekee niwashukuru wananchi wangu hasa wafanyabiashara kwa kuchangia ujenzi wa soko hili, pia na Mbunge wa jimbo la Mbarali Mhe.Haroun alinisaidia hapa kifusi malori 70 kwa ajili ya kushindilia chini.Niliahidi kuwatumikia na sitawaangusha nitakuwa nanyi bega kwa bega nanyie nawaomba mniunge mkono,”amesema Mavunde

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amempongeza Mavunde kwa kazi anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuwataka wananchi kumuunga mkono ili aweze kuwatumikia ipasavyo.Kadhalika, Mkurugenzi Kunambi amesema Manispaa imepangwa vizuri kwa kuwa kila kata imetengewa eneo kwa ajili ya soko na kwamba Manispaa hiyo imejipanga kutengeneza masoko hayo.

Aidha amesema mwezi Machi mwaka huu utaanza ujenzi wa stendi kubwa ya kisasa ya mabasi yaendayo mikoani na soko la kisasa katika eneo la Nzuguni.

No comments: