Thursday, February 1, 2018

HALMASHAURI MASWA YASHAURIWA KUWEKEZA KIWANDA CHA BIDHAA ZA NGOZI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akivaa viatu vilivyotengenezwa katika Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za Ngozi kilichopo Senani Wilayani Maswa wakati wa Ziara yake ya kukagua viwanda vidogo wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa tatu kushoto) akiwa pamoja na viongozi wakuu wa Wilaya ya Maswa wakielekea katika Kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa Ngozi katika Kijiji cha Senani kata ya Senani wakati wa ziara yake ya kukagua viwanda vidogo wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akifuatilia hatua mbalimbali za utengenzaji wa viatu vya ngozi kwenye kiwanda cha kutengeneza bidhaa ngozi kilichopo Kijiji cha Senani kata ya Senani wakati wa ziara yake ya kukagua viwanda vidogo wilayani Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Njiapanda wilayani Maswa, wakati alipotembelea eneo ambalo kitajengwa kiwanda kidogo cha kutengeneza ungalishe kitakachomikiwa na shule za Msingi 30 za Maswa,wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda vidogo wilayani humo.

………………….

Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu

Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeshauriwa kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu, mikoba na mikanda kinachomilikiwa na kikundi cha Usindikaji Ngozi Senani kilicho kata ya Senani wilayani Maswa, ili kuongeza thamani ya ngozi zitokanazo na mifugo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda vidogo katika wilaya MASWA.

Mtaka amesema katika kutekeleza Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya Viwanda , Halmashauri ya Maswa inapaswa kuwekeza katika viwanda vinavyoanzishwa na vikundi ili kuviwezesha katika upatikanaji wa malighafi ya kutosha, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo pamoja na kilimo ili viwanda hivyo viweze kuzalisha kwa tija.

“Tungehitaji kuwa mkoa ambao utawekeza sana katika viwanda vidogo na ndiyo maana tulianza dhana ya Wilaya moja bidhaa moja kiwanda kimoja na sasa tunakwenda kwenye Kijiji Kimoja Bidhaa Moja Kiwanda kimoja; tunataka kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ya Mkoa” alisema Mtaka.Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kuwasaidia wanakikundi kuweka mifumo mizuri ya kutengeneza soko la bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kuuza katika minada yote ya wilaya hiyo na kuimarisha soko la nje.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt.Fredrick Sagamiko amesema Halmashauri itahakikisha kiwanda hicho kinapata malighafi ya kutosha ambapo amebainisha kuwa Halmashauri imeingia mkataba na Chuo cha DIT Mwanza kuhakikisha kuwa inazalisha malighafi(ngozi) kwa wakati kwa ajili ya kiwanda hicho.

Akiwa Malampaka ambapo alitembelea Mradi wa Ghala na Mashine ya kukoboa mpunga na kupanga madaraja, Mtaka amekipongeza Chama cha Ushirika Bumala AMCOS kwa kuanzisha kiwanda, huku akiwataka wananchi wa eneo hilo kujiandaa kiushindani katika biashara, kwa kuwa hivi karibuni Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa bandari ya nchi kavu itakayoenda sambamba na ujenzi wa Reli ya Kisasa(Standard Gauge).

“Ni lazima mjiandae kiushindani katika biashara, miaka mitatu ijayo katika Mipango ya Serikali Malampaka haitakuwa kama ilivyo, hapa ni mahali ambapo Standard Gauge ikianza bidhaa zitakuwa zikisafirishwa kwa wingi; nimeshaongea na Mkurugenzi kuwa eneo hili lipimwe na Halmashauri imiliki eneo la uwekezaji” alisisitiza Mtaka.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka alitembelea eneo la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza ungalishe katika Kijiji cha Njiapanda, ambacho kitamilikiwa na shule 30 za Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, kinachoanzishwa kwa lengo la kuongeza kipato cha shule na halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na kuboresha lishe za watu.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Maswa, Mwl. Mabeyo Bujimu amesema shule za msingi 30 wilayani humo zitanufaika kwa kulima viazi lishe na kukiuzia kiwanda hicho kama malighafi pamoja na kuuza bidhaa zitakazozalishwa na kiwanda.

Huu ni mwanzo wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ambayo amepanga kutembelea viwanda vidogo vilivyopo katika wilaya zote za mkoa huo.

No comments: