Monday, February 12, 2018

ATHARI YA UTANDAWAZI NA SIASA YA TANZANIA NA MAENDELEO YAKE


Na Saleh Jabir
Nikiwa kama mwanafunzi ninayesomea sayansi ya kijamii, naandika makala hii kwa msukumo wa hisia ya uzalendo kwa nchi yangu na kwa kutumia maono yangu na akademia ya kisayansi kuhusu mambo ya kijamii yanayohusu jamii yetu kwa faida ya Watanzania wote. Uchambuzi wa moja kwa moja unaohusu jamii katika dunia hii ya leo ya utandawazi, utakuwa ni wa makosa iwapo hatujachambua siasa na uchumi kwa ujumla wake. 
Na uchambuzi wa moja kwa moja unaohusu siasa katika dunia hii ya leo ya utandawazi, utakuwa ni wa makossa iwapo hatujachambua uchumi na jamii kwa ujumla wake, na hali kadhalika. Kisayansi, utafiti na uchambuzi wa pamoja wa mambo yanayohusu jamii, siasa na uchumi ndiyo suluhisho la manufaa ya jamii ya karne ya 21 (21st century) na si vinginevyo.
Malengo ya makala hii ni kuangaza nchini kwetu Tanzania na kutolea mifano baadhi ya mataifa mengine ya jirani na ya mbali ambayo ni rafiki na Tanzania. Siyo kwasababu nyingine yoyote, ila ni kwasababu ya kuimarisha urafiki wa kweli na iwe ndiyo chachu ya maendeleo kwetu sisi kama Watanzania, kwa Afrika, na hata dunia nzima.
Tupo karne ya 21, na miaka 56 tangu tupate uhuru kutoka kwa mkoloni. Nchi yetu Tanzania inaelekea kubugikwa na utandawazi. Kipato cha mtu wa hali ya chini kimezidi kudidimia na kipato cha mtu wa hali ya juu kimezidi kuongezeka. Maadili kwa ujumla wake katika jamii yamezidi kuporomoka, na maadili katika utumishi wa umma kiasi fulani yameshuka. Tumeona baadhi ya wanasiasa, wanaharakati, na baadhi ya taasisi za kijamii zinatetea uovu na zinakemea yanayoonekana ni mema kwa faida ya jamii. Migongano ya kijamii yanayohusu ndoa za utotoni, ukeketaji na jinsia. Pia nitaelezea tofauti kati ya siasa na dini kisayansi. Yote haya ni changamoto za karne ya 21.
Makala hii ni makala yenye kuangalia athari ya utandawazi na siasa ya nchini kwetu Tanzania ili iwe ni kioo cha kuangalia wapi tunatoka, na iwe ni mizani ya kuangalia wapi tulipo, ili kwa umoja wetu, makala hii iwe ni moja ya mishale ya mwanga itakayoangaza mustakbali wa taifa letu na tunapoelekea. Ushauri wangu, mbali na kuisoma makala hii mpaka mwisho wake, makala hii iwe ni makala yenye kutusaidia kufikiri na kuzingatia yaliyomo ndani yake, kwasababu bila ya kujua wapi tunatoka, tutakuwa hatujui wapi tunaenda.
HISTORIA YA UKOLONI AFRIKA MASHARIKI NA MABADILIKO YA DUNIA
Ukoloni (Colonialism) ni nini? Ukoloni ni hali ya mkusanyiko wa mambo yenye maslahi ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, na kijamii, ambayo nchi moja yenye nguvu inatumia maslahi hayo ya nchi dhaifu kuitawala na kuinyonya rasilimali zake, na maslahi yake, ama kwa nguvu au kwa utunzi wa sheria.
Kutokana na ufafanuzi wa Pountney & Maric (2015, Uk. 213), Ukoloni ni hali ya nchi dhaifu kunyonywa na nchi yenye nguvu ili nchi yenye nguvu ijiongezee nguvu zake na utajiri wake kutokana na rasilimali za nchi dhaifu.
Afrika ilikuwa inatawaliwa na Wafalme wa Kiafrika ambao kiasili ndiyo wakuu wa kimila; na hata kwenye vitabu vitakatifu Mwenyezi Mungu kataja uwepo wa wafalme duniani kwa njia moja au nyingine, na bila ya shaka Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye Mfalme wa Ulimwengu wote. Wafalme wa Kiafrika, hususan nchi zetu za Afrika Mashariki, walikuwa wakiishi na watu wao katika maisha ya furaha, ya kijamaa, na ya amani.
Walipokuja wakoloni, waliwakuta Wafalme wa Kiafrika wana siasa zao za kujiongoza na watu wao, wanajua thamani ya dhahabu, thamani ya vipusa, thamani ya pembe za ndovu, na hata thamani ya ngozi za wanyama, mbinu za ujenzi wa nyumba, na kadhalika. Walikuwa wameendelea kimaisha, na walikuwa wana mila zao na desturi zao ambazo ndizo zilizokuwa zikiwaweka kwa amani na usalama. Mila na desturi hizo nyingi bado tunazitumia katika jamii zetu za Kiafrika mpaka hii leo na ndiyo zinatuweka katika hali ya kuwa wastaarabu katika kuingiliana katika maisha yetu ya kila siku na kuishi kwa furaha na amani. Chifu ni jina la Kizungu, ambalo wakoloni waliwapa wafalme wa Kiafrika. Lakini kila kabila, Machifu waliitwa kwa jina la kimila. Kwa mfano ‘Mndewa’‘Mwene’, na kadhalika. Kwahiyo, Waafrika walikuwa wakiishi maisha ya kijamaa, na Machifu walikuwa wakiangalia maslahi yao ya kuishi kwa pamoja na amani (Social order).
Kabla ya wakoloni kuingia Afrika, Wazungu wa Hispania na wazungu wa kutoka Ureno waliingia Marekani ya Kusini kutawala kikoloni kwenye karne ya 15 (miaka ya 1400s) na karne ya 16 (miaka ya 1500s) kwa malengo ya kutafuta rasilimali za kuwajengea nguvu za kiuchumi na za kiutawala nchini mwao. Bara la Marekani ya Kusini lilikuwa ndiyo bara la kwanza kutawaliwa na Wazungu. Kisha likafuatia bara la Asia na baadaye bara letu la Afrika ambalo lilitawaliwa na wimbi kubwa la wakoloni kutoka nchi mbalimbali za Ulaya mwishoni mwa miongo mitatu ya mwisho ya karne ya 19 (1800s).
Bara la Asia kabla ya kutawaliwa kwake na wakoloni, lilikuwa ndiyo bara kubwa la kibiashara wakati huo ambapo Wazungu walikuwa wakienda kufanya biashara (Trade) ya kuuza madini ya fedha na madini ya dhahabu yaliyotoka Marekani ya Kusini, na wao walinunua bidhaa kutoka bara la Asia kwa mfano viungo vya chakula na hariri kwenye nchi za China, India na Arabuni, kwa madhumuni ya kuuza bidhaa hizo nchi za Ulaya kwa faida kubwa.
Kipindi hicho hicho cha karne ya 15 na karne ya 16, Mreno aliyeitwa kwa jina la Vasco da Gama aliingia kwenye fukwe za bahari ya Afrika Mashariki na akafika mpaka Tanganyika katika safari zake za kuizunguka na kuichunguza dunia, na kuanza kuweka makazi ya Kireno. Baadaye, Wazungu wa Ureno waliingia Afrika kwenye karne ya 15 (1400s) kwa malengo waliyowadhihirishia mababu zetu wa Afrika mara tu walipoikanyaga ardhi ya Afrika kwa mara ya kwanza na baadaye ikapelekea kuwa ndiyo chanzo cha Ukoloni wa Afrika […]. Waliingia Kongo mwaka 1482 wakati huo Kongo ilikuwa chini ya Mfalme Nzinga a Nkuwu ambaye aliwapokea kwa upendo na ukarimu kama wageni. Mfalme alipofariki, mtoto wake Nzinga Mbemba, kwa jina lingine Mwene Kongo akarithi ufalme. Wareno walimshawishi Nzinga Mbemba kuwa wana nia naye nzuri, na yeye akashawishika. Kwasababu alitaka nchi yake ifanikiwe kimaendeleo, alipata fursa ya kuwapeleka baadhi ya watu wake pamoja na baadhi ya watoto wake wakasome Ulaya. Mwene Kongo aliwaomba Wareno wamuuzie meli ili aanze kufanya biashara ya kupeleka bidhaa zake nje ya nchi, mfano dhahabu, ili akauze nchi za Ulaya na Asia ili ailetee maendeleo nchi yake. Wareno wakamgomea na ndipo kipolepole wakaanza mikakati ya kumuangusha mfalme ili Kongo iwe koloni la Wareno na wafaidike na rasilimali na maliasili zake. Kipindi hicho, Wareno walikuwa washatanda Kongo na idadi yao ilikuwa ishaongezeka na huku wakiwa na silaha za moto.
Nzinga Mbemba, aliamua kukata ushirikiano na Wareno mwaka 1543 baada ya kutakiwa watu wake kufanywa kuwa watumwa wa Wareno. Yote hayo yakapelekea vita baina ya Wakongo na Wareno kwa kipindi cha zaidi ya miaka mia na mwishowe Wareno wakashindwa. Kipindi hicho hicho, mwaka 1503-1505, Wareno waliingia Zanzibar, Kilwa na Msumbiji. Msumbiji, ilikuwa chin ya mfalme Mwene Mutapa, ambaye pia aliwakaribisha Wareno kwa ukunjufu na ukarimu lakini yakatokea yale yale yaliyotokea Kongo. Mpaka kufikia mwaka 1629 mfalme wa Msumbiji kipindi hiki alikuwa anaitwa Mamvuru Mutapa naye akapigana vita na Wareno kutetea maslahi ya nchi yake na hatimaye kulikuwa hakuna budi bali akalazimika kuwapatia madaraka Wareno kuwa wakoloni wa Msumbiji. Ilipofika mwaka 1680 na mwaka 1690 vita nyingine ilifumka, mfalme wa kipindi hiki alikuwa anaitwa Mutapa Mukombwe akafanikiwa kuwashinda Wareno na kuikomboa Msumbiji.
Wakati huo huo, wa karne ya 17 na karne ya 18, Wazungu waliendelea na ukoloni wao Marekani ya Kusini na Marekani ya Kaskazini hasa kwenye uchumi wa kilimo cha tumbaku, pamba, sukari, kahawa, na chai ndiyo yalikuwa mazao makubwa yakisafirishwa kutoka Marekani kwenda Ulaya kwa madhumuni ya kuuza na kupata faida. Kuanzia karne ya 17 hadi karne ya 18, kipolepole dola za Ulaya zilianza kuwakilishwa na makampuni ya wafanyabiashara wao kuendesha biashara hizo katika koloni zao badala ya kuendeshwa na wawakilishi wa dola zao. Na ndipo ubepari ulikuwa unaanza kushika kasi na kusimamiwa na dola zao kwa kuweka sheria za kisiasa, za kijeshi, na za kiuchumi, kwa mfano, sheria za soko huru.
Karne ya 19, wimbi la wakoloni wa kutoka Ulaya wakaingia Afrika kwa madhumuni ya kutafuta na kuchukua rasilimali, malighafi, na maliasili. Kipindi hiki cha karne ya 19, ubepari na ushindani wa kiuchumi ulikuwa umezidi kupamba moto nchi za Ulaya, na zilikuwa zimeshaanza mapinduzi ya viwanda kutokana na kukidhi ukubwa wa mahitaji ya uzalishaji wa bidhaa nchini mwao. Mpaka ilipofika mwaka 1876, Afrika ilikuwa imo mikononi mwa wakoloni wa Kizungu kwa asilima 10%, na ilipofika mwaka 1900, Afrika ilikuwa mikononi mwa wakoloni wa Kizungu kwa asilima 90% ya ardhi yake.
Karne hiyo hiyo ya 19, mwaka 1884-1885 wakoloni wa Kizungu waliamua kuigawa Afrika katika nchi mbalimbali kutokana na umiliki wa rasilimali na maliasili zao za kikoloni zilipo (The Scramble for Africa). Kisha wakawekeza viwanda vya kikoloni vya kuzalisha bidhaa na kusafirishwa nje ya nchi kushindana na masoko ya Ulaya.
Mpaka kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, mfumo wa dunia wa uchumi ukawa umetengenezwa na sheria za kikoloni ya kwamba nchi zinazotawaliwa kikoloni ni nchi zenye kutoa rasilimali za aina yote, na nchi zilizotawala makoloni hayo ndiyo nchi zenye kufaidika na rasilimali hizo. Huu ndiyo ulikuwa mwanzo wa utandawazi (Katundu, S., 2017Globalisation lakini ulikuwa upo kwenye jina lingine na sura nyingine. Mfumo huu wa uchumi kwa wakati huo, wengine wameuita Ubeberu (Imperialism) ambao umezaliwa na Ubepari (Capitalism)wa kikoloni. Tofauti za ‘usawa wa kibinadamu’ barani Afrika zikaanza kujitokeza na kukuwa kwa kasi, kiuchumi pamoja na kijamii, siyo tu kwa mtu mmoja mmoja bali hata tofauti kati ya nchi za Kaskazini mwa dunia na nchi za Kusini mwa dunia.
Ilipofika miaka ya mwanzo ya karne ya 20 (1900s) nchi za Ulaya zilikuwa zinazalisha bidhaa kwa wingi kiasi kwamba usambazaji wa bidhaa ulizidi mahitaji ya ndani ya nchi zao na ikabidi watafute soko la nje katika nchi zao za jirani na katika koloni zao. Ili waendelee kukua kiuchumi na kushindana katika soko la dunia, wakoloni iliwabidi walishe viwanda vyao kutokana na malighafi zilizotoka kwenye makoloni yao. Waliamua kujenga miundombinu ya barabara, bandari na reli ya kuwawezesha kusafirisha rasilimali, malighafi, na maliasili kwa njia nyepesi na njia rahisi kutoka nchi za makoloni yao ikiwemo Tanganyika.
Ningependa kuchukua fursa hii, kupeleka pongezi kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa ari na uzalendo aliokuwa nao kwa nchi yake Tanzania kwa kuamua kujenga miundombinu ya kisasa yetu wenyewe ya barabara, madaraja, na reli zitakazowasaidia Watanzania kujikomboa kiuchumi siyo mtu mmoja mmoja tu, bali kwa taifa lote kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Tusijihadae kisiasa. Tupende au tusipende, miundombinu ya nchi hii, kuanzia miundombinu ya usafiri na miundombinu ya umeme ilikuwa ni ndoto ya Watanzania wengi kwa muda mrefu tangu uhuru wa nchi yetu.
Ndani ya miaka miwili, Mheshimiwa Rais Magufuli amefanya mengi ikiwemo uthubutu wa kutoa elimu bure, madawati ya shule nchi nzima, na mbali na miundombinu yake ambayo TAMISEMI na Wizara ya Elimu zinafanya kazi kubwa ya kuishughulikia, na tunataraji huu ni mwanzo na miundombinu ya kitaaluma itafuatia. Yote haya siyo ya kusikia, bali ni yanayoonekana na anastahili kuungwa mkono kwa kila njia ili tuzidi kumtia nguvu kuendelea kufanya mengine makubwa zaidi kwa maslahi ya Watanzania. Kwasababu anayoyafanya hajifanyii yeye, bali anafanya kwa maslahi ya Watanzania wote bila ya itikadi ya chama, dini, au ukabila. Ni ishara tosha kwamba Rais Magufuli ni Rais anayethubutu kuibadilisha nchi yetu kwa maslahi ya Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo, ni Rais anayewakilisha hasa maana ya nchi huru na nchi ya kujitegemea na ni mfano wa kuigwa barani Afrika. Na ni Rais anayetimiza yale yaliyoahidiwa katika ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, CCM, ya mwaka (2015, Uk. 46-72) iliyodhamiria kuendeleza miuondombinu kwa kuuwezesha uchumi wa Tanzania uwe ni uchumi unaojitegemea kama taifa huru.
Tukirudi enzi za ukoloni, kipindi cha mwaka 1880 mpaka mwaka 1914, takriban nchi zote za Afrika zilikuwa zimo mikononi mwa wakoloni. Watanganyika hawakujitolea kwa hiyari yao kukoloniwa na kuachwa kuwa nchi maskini, bali ni hali iliyotengenezwa kwa ubeberu wa kikoloni. Kipindi cha mwaka 1914 mpaka mwaka 1939, nchi za Ulaya zilipitia vita kuu mbili za dunia na zilikuwa zimo kwenye hali mbaya kiuchumi. Kipindi hicho, baadhi ya nchi za Ulaya ziliamka na mtazamo tofauti wa kisiasa kuona mambo yanavyoenda na kuamua kuzilinda nchi zao kutokana na kuingiliwa mambo yao ya kisiasa na ya kiuchumi na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya. Urusi ikafanya mapinduzi yake mwaka 1917, na nchi zingine zikaanza kuamka kulinda maslahi ya nchi zao kwa mfano China na Uturuki ziliamka kwa msimamo wa ‘principles’ za ‘rights of nations to self-determination’ (Lenin, V., 1916).
Baada ya vita ya kwanza ya dunia mwaka 1914, nchi za Ulaya ziliamua kuanzisha umoja wa nchi zilizoathirika na vita hiyo. Umoja huo uliundwa mwaka 1920 ambao uliitwa League of Nations kwa madhumuni ya kuunganisha pamoja nchi zilizoathirika kivita na kutazama maslahi yao kwa upana zaidi ili yale yaliyotokea ya vita kuu ya kwanza ya dunia yasijirudie tena. Marekani, Urusi, na Ujerumani hazikuwemo kwenye umoja huo. Baadae nchi nyingine zilijiunga na umoja huo lakini ilipofika mwaka 1932-1933 umoja huo ulivunjika.
Mwaka 1945 uliundwa Umoja wa Mataifa (United Nations) baada ya vita kuu ya pili ya dunia kwa madhumuni yale yale ya kuunganisha pamoja nchi zilizoathirika kivita na kutazama maslahi yao kwa upana zaidi ili yale yaliyotokea kwenye vita kuu ya pili ya dunia yasijirudie tena. Mwaka 1947 nchi hizo ziliamua kuanzisha umoja wa kibiashara GATT (General Agreement on Tariffs and Trade) ili waweze kufanya biashara bila ya kunyonyana. Umoja wa kibiashara huo ulianzishwa na nchi 23 ambazo zilisaini umoja huo wa kibiashara. Baadae mataifa mbalimbali yaliendelea kujiunga na umoja huo. Mwaka 1995 GATT ikabidilishwa jina ikaitwa WTO (World Trade Organisation).
Baada ya vita ya pili ya dunia, wakoloni walikuwa tayari washaweka mfumo kamili wa kisiasa na wa kiuchumi katika nchi za makoloni yao, ili ziwe zinaongea lugha moja na nchi zao katika mfumo mpya wa ubeberu ambao utasimamiwa ndani ya makoloni yao na watu wa asili ya nchi za makoloni yao, kwa mfano nchi yetu Tanganyika, ili kuepusha gharama za kusimamia koloni zao. Wakati huo huo, mfumo wa makampuni makubwa kwenye nchi za wakoloni ulikuwa umeshaandaliwa tayari kwa kupokea malighafi za kutoka nchi zilizokoloniwa.
Kwahiyo, mfumo wa kuchukua malighafi na rasilimali kwa bei ya chini na bei rahisi uliendelea kwenye nchi za kikoloni kufaidisha wakoloni na watu wachache waliowatumikia na kupelekea Tanganyika kubaki kuitwa nchi maskini na nchi iliyopo dunia ya tatu (Third World).
Wakati huo huo, baada ya vita ya pili ya dunia, mwaka 1949 yakatokea mapinduzi ya China yaliyoongozwa na Mheshimiwa Mao Zedong kwa kuona nchi yao imeshikiliwa na watu wachache ambao walikuwa wanajifaidisha wao wenyewe bila ya maslahi ya wananchi wengine wa hali ya chini nchini mwao. Baada ya mapinduzi ya China, Mheshimiwa Mao Zedong akafunga milango ya China upande wa bara palipotokea mapinduzi hayo kwa malengo ya kuzuia na kulinda malighafi na rasilimali za nchi yake na watu wake, ili kwanza wapate kuimarisha misingi ya nchi yake kisiasa na kiuchumi chini ya chama cha Kikomunisti (Kijamaa) cha watu wa China. Kwasababu hizo, baadhi ya nchi za magharibi, kwa mfano Marekani, ilikata mahusiano ya kidiplomasia na China.
Kuanzia miaka ya 40 (1940s) nchi mbalimbali zikaanza kupewa uhuru wao kutoka kwa wakoloni. Na mwisho wa miaka ya 40 kuingia miaka ya 50 na kuendelea, iliitwa miaka ya ‘Modernisation’ na ‘Secularisation’.
Nadharia ya Modernisation ilikuwa ni nadharia ya nchi za magharibi kuandaa mkakati ambao utakaoleta maendeleo kwa nchi maskini. Nadharia ya maendeleo iliyokusudiwa na watu wa magharibi kwa nchi maskini (Third World countries) ni (Social Change) mabadiliko ya kiutamaduni, kimila, kidini na kijamii kwa ujumla ili nchi maskini ziendane na utamaduni, mila, na jamii za watu wa magharibi kwa imani ya Sayansi na Teknolojia kuliko imani ya utamaduni wa mtu, au utamaduni wa taifa lake, au mila yake, na itikadi nyinginezo, kwa imani kwamba mabadiliko haya ndiyo yanaleta maendeleo ya uchumi katika nchi kwa mtazamo wao na siyo kwa mitazamo ya nchi maskini ambao wana mila zao na utamaduni wao na itikadi zao nyingine. Kwa kifupi, ni kuhamisha fikira za watu badala ya kuamini itikadi zao kwa vile wanavyoviamini na badala yake kuamini vinavoshawishiwa na Sayansi na Teknolojia na hatimaye kuleta mabadiliko katika jamii (Social Change).
Kutokana na ufafanuzi wa Bwana Wilbert Moore (1963), Social Change (Mabadiliko ya Kijamii) ni:
“The alteration of social structures with respect not only to institutions and actions but also to changes in cultural elements, such as norms, beliefs, and values.” (na Alexander, J., Thompson, K. & Edles, L., 2012, Uk. 591).
Maana yake, Bwana Moore (1963) anaelezea maana ya Social Change(Mabadiliko ya Kijamii) maana yake ni “Kuibadilisha jamii jinsi ilivyokuzwa kutokana na utamaduni wake, na vitu vyote wanavyoviona ni vya kawaida kwao, na badala yake kuingiziwa vitu vipya ndiyo viwe kwao vinaonekana vitu vya kawaida kuliko vile vitu vyao wenyewe, kwa mfano imani za kimila na za kidini, na itikadi na maadili, siyo tu kwa jamii bali hata na kwa taasisi zake.”
Mifano mingi ya mabadiliko ambayo yanaenda kutokea nchini kwetu Tanzania ni kutokana na nadharia hii. Kwa mfano, sheria zinazoitwa ndoa za utotoni na sheria za jinsia (gender), hizo ni chache kuzitaja kwenye muktadha mzima wa masuala yanayohusu jamii ambayo kwa mtazamo wa mbali yana athari kubwa katika jamii. Ukiangalia athari za kumuacha mtoto ambaye ameshabaleghe na ana matamanio ya kimwili hasa sehemu za vijijini ambapo maisha ya wazee wetu ni magumu kuitazama familia, na kwa nchi yetu changa bado hatujafikia maendeleo ya kijamii, mtoto anaishia kutiwa mimba huku akiwa anasoma. Na jinsi tunavyoshawishiwa na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali, kila wanapofanya kampeni za ndoa ya utotoni utaona wameinasabisha na ukeketaji iwe ni kama kiini macho.
Ukeketaji ni suala la kimila na siyo makabila yote yanayofanya zoezi hilo nchini kwetu Tanzania. Zoezi la kupinga ukeketaji naliunga mkono, lakini lazima lichukuliwe kiheshima kutokana na mila wanaotumia ukeketaji. Ukeketaji unaweza ukatolewa elimu na watu wetu wenyewe wa ndani kwa viongozi wa kimila kwa makabila wanayofanya zoezi hilo na mpaka waridhie, kwa upole na kwa heshima za mila zetu, na siyo tugeuke vibaraka. Ukeketaji na ndoa za utotoni ni vitu viwili tofauti kabisa na vyote vina athari zake mbalimbali. Ni cha ajabu kwamba ukeketwaji upigwe vita, na ndoa ya utotoni ipigwe vita, jibu lake linapatikana mtoto akishabaleghe na akashikwa na matamanio ya kimwili mwisho wake anaishia wapi? Je hawa wazee wetu wa kimila wa baadhi ya makabila walikuwa wana hekima kuliko sisi wajukuu zao? Mwisho wake ni yale yale, serikali yetu changa itakuja kubeba mzigo wa kumtazama huyu mtoto wa kimaskini, na mengineyo mengi yanayofungamana na hayo. Ni bora kuihalalisha ndoa na elimu kuliko mimba ya nje na elimu.
Niliwahi kusema (Katundu, S., 2016) masuala haya yaangaliwe kikanda na kitakwimu zaidi, kuliko kutumia ufagio mmoja kwa taifa zima. Kwa maslahi mapana ya kijamii na taifa, msimamo wangu upo palepale, ndoa za utotoni kupigwa vita vijijini na hata mijini, nchi yetu bado haijawa tayari. Huu ni kwa mtazamo wa mbali bila ya kutegemea misaada ya kutoka nje yanayohusu suala hili. Mfano mwingine ni haki za binadamu ambazo zina mitazamo ya kimagharibi na zinazogongana na imani na itikadi zetu za Kiafrika au za kidini, kwa mfano kutetea ushoga, na mfano mwingine ni kuwapa uhuru na nguvu watoto kwa dhana ya kuwalinda na adhabu za kinidhamu na wazazi wao au walezi wao. Kuwalinda watoto kwa kutopewa adhabu za nidhamu na wazazi wao au walezi wao, kunapelekea watoto wajikulie huru na waamue wanachotaka kufanya katika maisha yao bila ya kujali muongozo wa wazazi wao, au athari kwa wazazi wao au kwa jamii yao, bali wawe wenye kuogopa sheria za mitazamo ya kimagharibi, na hayo ni machache kuyataja.
Mfano mwingine ambao tumeanza kuuona wenye nadharia za Modernisationni kuondoa maadili yanayotokana na itikadi, mfano mmoja wapo ni kusimama kwenye majukwaa na kudharau mitazamo na misingi ya taifa ya baba wa taifa Mwalimu Nyerere na hatimaye kudharau itikadi, maadili, na misingi ya taifa na faida zake kwa taifa na kuyaita ni mambo yaliyopitwa na wakati. Hiyo ni mifano michache katika baadhi ya mambo yanayohusu jamii na siasa ya nchi.
Vilevile, malengo mengine ya nadharia ya Modernisation miaka ya 50 yalikuwa ni ya kiuchumi, kuanzisha viwanda vya kikoloni katika nchi maskini zenye malighafi na zenye rasilimali kwa madhumuni ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa sheria na kanuni za soko huru. Kwa kifupi, ni nadharia za nchi zenye nguvu kuziambia nchi maskini kama Tanganyika nini cha kufanya bila ya kuangalia maslahi mapana ya kijamii na maendeleo ya watu wa nchi kiuchumi na taifa kwa ujumla. Haimaanishi kwamba tusikaribishe viwanda kuekezwa kutoka nchi za nje katika karne hii ya 21, lakini ni kuangalia vipi viwanda hivyo vitavisaidia Tanzania na watu wake kiuchumi na bila ya kupoteza misingi yake ya kisiasa na ya kijamii.
Pongezi ziende kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua za kulinda viwanda vya ndani na kuanza kuweka sheria mbalimbali za kulinda madini, malighafi na rasilimali za taifa kwa kutekeleza ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, CCM, ilani ya mwaka (2015, Uk. 34). Kwa mfano kuundwa kwa kamati za uchunguzi wa makinikia, na kamati ya uchunguzi wa madini ya Tanzanite, na madini ya Almasi, na kuweka sheria mpya za kulinda maslahi na rasilimali za taifa kwa manufaa ya Watanzania.
Vilevile, pongezi zingine kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua mahsusi za kuanza kulinda maadili na utamaduni wa Kitanzania kwenye nyanja zote za taasisi za taifa kuanzia taasisi za Sanaa mpaka taasisi za Utumishi wa umma. Kama ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, CCM, ilani ya mwaka (2015, Uk. 234) ilivyoahidi kutekeleza kuhusu masuala ya maadili ya Watumishi wa Umma. Na kuhusu masuala ya maadili ya Sanaa kama ilivyoainishwa na ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, CCM, ilani ya mwaka (2015, Uk. 182) iliyodhamiria kuweka maadili ya Sanaa kwa manufaa ya wananchi kwa kuzingatia maadili ya jamii na manufaa kwa wasanii wenyewe katika jamii yao na mustakbali wao. Yote haya, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli anayatekeleza ili kulinda na kurudisha maadili na utamaduni wa taifa kwenye mstari.
Nadharia nyingine ni nadharia ya Secularisation ni nadharia inayoendana na nadharia ya Modernisation. Nadharia ya Secularisation ni nadharia inayotenganisha dola mbali na dini, ni nadharia ya kilimwengu. Ni nadharia inayoamini vinavyoonekana na vile vya taasisi zake ambavyo havihusiani na imani za kidini, hiyo ndiyo maana halisi ya Secularisation.
Mfano wa vitu vinavyoonekana vya Secularisation visivyohusiana na taasisi za dini ni mfano vyuo vikuu visivyo vya kidini, taasisi zisizo za kidini, na vyombo vya habari. Mfano wa vitu vinavyoonekana vya Secularisation vinavyohusiana na sayansi ni mafuriko, vimbunga, na mitetemeko ya ardhi. Mfano wa vitu vinavyoonekana vya Secularisation vinavyohusiana na maisha ya kila siku ya mwanadamu ni haki za binadamu (kama zilivyotafsiriwa na watu wa magharibi), na usawa wa kibinadamu (kama ulivyotafsiriwa na watu wa magharibi).
Sisi Watanzania, utamaduni wetu ndiyo ilikuwa ngao yetu na bado inaendelea kuwa ngao yetu madamu tutaweza kubainisha nini kinatufaa katika jamii yetu na nini chenye madhara katika jamii yetu kama nchi. Suala la maadili na utamaduni wa Tanzania siyo suala la dini moja au nyingine, ni suala la taifa na sote tumo kwenye jahazi moja, likizama tunazama wote na vizazi vijavyo. Tanzania mpaka hapa ilipofikia leo kuwa nchi ya amani na watu wake kupendana na wenye kuwa na umoja na mshikamano ukilinganisha na baadhi ya nchi nyingine duniani, ni kutokana na misingi ya desturi zetu kutoka kwa mababu zetu, na misingi ya kidini iliyojengeka ndani ya watu wake tangu karne ya 8 kuingia kwa dini kwenye nchi zetu za Afrika Mashariki na mpaka kupindukia karne ya 20. Ni misingi ya utamaduni wa Watanzania ambao umechukua kina kipana katika sehemu kubwa ya maisha yao ya kila siku, ambayo inatokana na mila na desturi, na dini zetu mbili, Uislamu na Ukristo, zinazoingiliana kijamii katika maisha mapana ya kila siku kutokana na mafundisho ya maandiko ya vitabu vitakatifu.
Misingi ambayo, inayosimamiwa chini ya usimamizi wa dola yetu tukufu iliyoasisiwa na baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wasaidizi wake, ambapo makabila yote yaliyomo ndani yake yaweze kuishi kwa umoja na amani bila ya kubaguana kikabila, kidini, au rangi zao, au kanda zao, na bila ya kudharau au kutenga heshima ya uhuru wa kuabudu wa dini zingine kama katiba ya nchi yetu inavyoeleza. Ni misingi ya utamaduni ambayo umetujengea amani na umoja wa kitaifa.
Kuna baadhi ya watu wamehoji kuhusu msimamo wangu wa kusema nchi yetu ya Tanzania ni nchi ya dini mbili, kivipi? Nitajibu suali hili kiakademia zaidi kuliko kutumia hisia zangu kibinafsi. Jibu lake ni kwamba nimefikia msimamo huo baada ya kuangalia nchi yetu ilipotoka na historia ya watu wake kuwa ni watu wa kupenda amani, umoja na mshikamano. Haimaanishi kwamba dini zingine si za amani, hapana! Dini zote ni dini zenye kuhubiri amani, na binafsi naziheshimu dini zote. Lakini Uislamu na Ukristo ndiyo utamaduni wa Tanzania ambao utamaduni huo ulianza pale ulipoingia Uislamu Afrika Mashariki kwenye karne ya 8, na kuingia kwa Ukristo Afrika Mashariki kwenye karne ya 15. Ni utamaduni wa zaidi ya miaka 1000 iliyopita ya Uislamu, na zaidi ya miaka 500 iliyopita ya Ukristo. Kwa umoja wake ndiyo utamaduni wa nchi yetu. Pale mila zetu za asili zilipoingiliana na dini zetu hizi mbili kwa upana wa ardhi ya nchi yetu. Utamaduni huu, umehimili vipindi mbalimbali vya kila zama katika karne 12 zilizopita kuanzia zama za Uchifu wa mababu zetu, zama za ukoloni, na zama za baada ya kupata uhuru wetu. Katiba yetu adhimu inatoa uhuru wa kuabudu, lakini kila nchi lazima iwe na utamaduni wake. na utamaduni wa Watanzania umeanza pale mila za kiasili zilipokutana na dini. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi inayotokana na uchambuzi wangu wa kisayansi.
Utamaduni (Culture) ni nini? Utamaduni ni mkusanyiko wa vitu mbalimbali vinavyoonekana vya kawaida katika maisha ya kila siku ya jamii husika kutokana na mafunzo mbalimbali ya mtu au watu waliyokulia nayo ndani ya jamii hiyo.
Hii ndiyo maana ya utamaduni wa mtu au watu katika ngazi ya jamii. Kitu chochote ambacho kinajitokeza katika jamii ambacho siyo cha kawaida huwa ni kinyume na utamaduni wao. Narudia tena, simaanishi kwamba dini zingine siyo dini zisizo na amani au kwa hisia yoyote inayofanana na hiyo, lakini maana yake tutakuja kuona zaidi huko mbeleni kwenye makala hii ambayo yanaendana pamoja na yale niliyoyaainisha hapo juu.
Kutokana na ufafanuzi wa Bwana Edward Tylor (1871, Uk. 1), Culture (Utamaduni) ni:
“Culture… is that complex whole which includes knowledge, beliefs, arts, morals, law, customs, and any other capabilities and habits acquired by man as a member of society.” (Tylor, E., 1871)
Maana yake, Bwana Edward Tylor (1871) anaelezea maana ya Culture (Utamaduni) maana yake ni mchanganyiko [mkusanyiko] wa mambo yote ikiwemo maarifa, itikadi, sanaa, uadilifu, sheria, desturi, na uwezo na tabia anayoipata mtu katika jamii yake inayomzunguka.”
Kwa hiyo, utamaduni wa jamii unajengwa kutokana na mkusanyiko wa mambo yanayomzunguka mtu au yanayoizunguka jamii ambayo hupelekea kutohoa na kuambukizana kwa mtu mmoja mmoja na kufikia ngazi ya jamii nzima na hatimaye taifa zima. Kutokana na utafiti wa akademia ambao tumeshauona, je ni nini utamaduni wa taifa letu?
Kwa muda mrefu sasa Tanzania tumekuwa tukijiuliza utamaduni wa Tanzania ni upi? Kutokana na mila na desturi mbalimbali za makabila mbalimbali ya asili yaliyomo nchini mwetu, utamaduni wa Tanzania ulizaliwa pale mila zetu zilipokutana na dini zetu kuu mbili za Uislamu na Ukristo kuanzia karne ya 8 mpaka karne ya 19. Ndipo utamaduni wa taifa ulizaliwa. Baada ya dini kuingia katika mila zetu za Kiafrika, baadhi ya mababu zetu wa Afrika walitohoa baadhi ya mila zao lilipowajia neno la Mungu na maamrisho yake ya haki ndipo wakaupokea Uislamu na baadaye baadhi ya mila zingine zikaupokea Ukristo.
Kutokana na hivyo, na kwa kulinda utamaduni wa Tanzania huko tunapoenda kabla hatujafikia utandawazi wa kiza, ningependekeza serikali na wazalendo wa nchi yetu kuingiza kifungu kwenye katiba yetu ya nchi kinachosema Tanzania ni nchi ya dini mbili zitakazosimamiwa chini ya serikali ambayo inawapa dini zote zilizopo nchini uhuru wa kuabudu bila ya kuvunja sheria na utamaduni wa watu wa taifa la Tanzania, iwepo kikatiba. Pendekezo hili ni njia moja wapo la kuimarisha na kuukinga utamaduni wa Tanzania kuendelea kuwa wa amani kwa vizazi vijavyo na kuendelea kuwa ni nchi yenye kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa dini zingine. Ni muhimu kila zama kufikiria mikakati mipya ya kulinda wananchi na utamaduni wao kama taifa ili kuweza kulinda misingi ya taifa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Hii ni nadharia yangu ya kisayansi, ninavyoiona nchi yetu ilipo na inapoelekea. Lakini hatimaye, dola na mihimili yake ndiyo yenye uamuzi wa mwisho.
Lazima ieleweke kwamba nadharia yangu hii ni uchambuzi wangu kama mwanasayansi wa kijamii na isieleweke kama ni hisia binafsi au maslahi binafsi. Ni uchambuzi wa kisayansi ambao unaheshimu dini zote na watu wote wa kutoka sehemu mbalimbali ambao wanaishi nchini Tanzania. Mfano nchini mwetu tunao watu wa dini ya Kihindu ambao asili yao ni kutoka India, na ninao marafiki ambao wengine nilisoma nao ambao wapo hapo hapo Tanzania. Lakini pia wapo Waislamu wa kutoka India ambao pia wapo hapo hapo Tanzania na ni Watanzania kama Watanzania wengine. Kwa hiyo, nadharia yangu haiangalii dini fulani au watu wa kutoka sehemu fulani kivingine, bali ni nadharia yenye ukweli wa kisayansi ambao naamini ndiyo utamaduni wetu wa Tanzania. Tukisema Tanzania ni nchi ya Waafrika, hatumaanishi kwamba Wachina, Wazungu, Wahindi na Waarabu hawapo.
Elimu, maarifa, au taarifa anayoipata mtu inaweza ikamsaidia kuijenga nchi yake. Elimu, maarifa, na taarifa hiyo hiyo anayoipata mtu anaweza akaichukua na akaigeuza kuwa ndiyo sababu ya kuiangamiza nchi yake ama kwa kiburi alichokuwa nacho mtu, au kwa chuki na choyo binafsi kwa watu anaowatumikia au watu waliomzunguka katika jamii. Sisi Watanzania wote, kwa utamaduni tuliojengewa nao, ni watu wenye utamaduni wa kupenda umoja, upendo, mshikamano, na heshima kwa watu wote.
Tukirudi tena kwenye suala la Secularisation, kutokana na maelezo ya Bwana Alexander, J., Thompson, K. & Edles, L. (2012, Uk. 489), ameielezea Secularisation kama ni:
“The declining significance of religion in social institutions, culture, and individual experience.”
Maana yake, Bwana Alexander, J., Thompson, K. & Edles, L. (2012) anaelezea athari ya Secularisation ni “Kuporomoka kwa dini kwenye taasisi za kijamii, kitamaduni, na kwa mtu mmoja mmoja.“
Kwa sisi Watanzania, Secularisation ni mfumo ambao upo katika mfumo wetu wa taifa kwa kipindi kirefu kwenye ngazi ya viongozi wa kikoloni kabla ya uhuru, na baada ya uhuru. Pamoja na rehema za Mwenyezi Mungu, mfumo huu umetusaidia kutulinda kama taifa kwababu ya mchanganyiko wa watu wa dini mbalimbali nchini mwetu, hususan Waislamu na Wakristo ambao waliokuwa wakiingiliana sana kwenye harakati zao za kijamii za kila siku, na umesaidia kudhibiti amani na kulinda maslahi ya nchi kwa mfano elimu. Na kwa upande mwingine, Modernisation, ni kitu ambacho kinaweza kutuletea athari kubwa mbaya kijamii katika nchi yetu na ni kitu ambacho wanasiasa na wawakilishi wa wananchi walioaminiwa na watu wao wanahitaji kuangalia upya yanayofaa na yasiyofaa kiuchumi na kijamii siyo tu kwa kuangalia maslahi na makatazo ya dini moja au nyingine, bali ni kwa maslahi mapana ya taifa lakini pia bila ya kupuuza dini.
SIASA NA DINI
Hivi karibuni, baadhi ya watu wamekuwa wakihoji tofauti baina ya dola (siasa) na dini nchini kwetu Tanzania. Hoja na sintofahamu ya suala hili mara nyingi hujitokeza pale kiongozi wa dini anapoongelea jambo linalohusu siasa, au pale mwanasiasa anapoongelea jambo linalohusu dini, au pale hoja za kidini na hoja za kisiasa zinapogongana na kusababisha kiwingu katika jamii. Mara chache sintofahamu hii inapotokea, hutupelekea kupata changamoto za kupambanua tofauti baina ya dini na siasa. Kwahiyo, badala ya kuwa tunazima moto mara kwa mara, nataraji uchambuzi huu utatusaidia kwa kiasi fulani kufahamu na kuelewa tofauti kati ya dola (siasa) na dini.
Matarajio ya sehemu ya makala hii ni kwamba uchambuzi huu usaidie na uweze kujibu masuali kwa mwananchi wa kawaida ili mwananchi wa kawaida aweze kujua, kupambanua, na kuitambua sehemu ya dola yake katika taifa, na sehemu ya dini yake katika taifa na katika jamii. Iwe ni lenzi ya kujenga udugu na umoja wa kitaifa. Niweke wazi kwamba utafiti na uchambuzi wangu huu, ni uchambuzi wa kisayansi unaogusa moja kwa moja katika taifa kama la kwetu la watu wa dini mbalimbali.
Kila Muumini wa dini nchini mwetu Tanzania, anafafanua maana ya dini kutokana na mafunzo ya dini yake ambayo yanatokana na kitabu kitakatifu cha dini yake. Na fafanuzi hizi lazima ziheshimike katika jamii ili watu waishi kwa pamoja na kwa amani. Katika jamii, kuna wanaoamini kwamba dini ipo na wanafuata maamrisho yake, na kuna ambao wanaoamini kwamba dini ipo lakini hawafuati maamrisho yake, na kuna wachache ambao ama ujumbe wa dini haujawafikia au hawaamini kabisa kama dini ipo. Kwa upande mwingine, dola au serikali, mbali na dini, ndiyo chombo kinachotumia siasa zake za ndani na nje ili kuwasilisha maslahi ya watu wake inayowawakilisha katika ngazi ya taifa. Hii inatupelekea tujiulize je, tofauti kati ya dola (siasa) na dini ni nini?
Kama nilivyoainisha hapo awali kwamba kila dini ina ufafanuzi wake wa maana ya neno dini kutokana na kitabu chake kitakatifu. Kwa hivyo, sitofafanua maana ya dini kutokana na ufafanuzi wa kila dini iliyopo nchini mwetu, bali nitafafanua maana ya dini kisayansi ili ilete uwelewa wa pamoja wa kufahamu nini tofauti kati ya dini na siasa katika ngazi ya kitaifa.
Kutokana na wanachuoni wa kisayansi, dini wanaifafanua katika makundi mawili: Substantive na Functional.
Kutokana na Bwana Alexander, J. (2012, Uk. 484) anafafanua upande wa kwanza kuwa dini kama Substantive ni kwamba dini ni mfumo uliojengwa juu ya misingi ya imani na matendo ambayo yana maana ndani yake. Bwana Max Weber (1905) ameenda mbali zaidi na akafafanua zaidi juu ya maana ya dini kuwa Substantive ni kwamba dini ni (Supernatural) ni kuamini nguvu zisizoonekana ambazo haziwezi kuelezewa kisayansi [kwa mfano kuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu]. Hiyo ndiyo maana ya dini kama inavyofafanuliwa na Bwana Max Weber.
Kwa upande mwingine, kutokana na Bwana Alexander, J. (2012, Uk. 485) anafafanua upande wa pili wa dini inavyofafanuliwa na wanasayansi wengine kuwa dini ni Functional ni kwamba dini ni kuamini vitu vinavyoonekana (Natural), kwa mfano, matukio na mikutano ya hadhara isiyohusiana na maudhui ya kumjua Mwenyezi Mungu, lakini kwao wao wanakutana kubadilishana fikra na mawazo yanayowafanya kuwa pamoja kwa vitu wanavyoviamini na wanavyoviona kwao ni vitu vitakatifu (Sacred).
Bwana Alexander, J. (2012, Uk. 70) anaendelea kuelezea maana ya vitu vitakatifu (Sacred things) maana yake ni vitu vyenye alama na ishara (Symbols) vinavyoiwakilisha jamii, ambavyo vina mahusiano ya kihisia (au ya kihistoria) yanayowagusa jamii husika. Bwana Alexander, J. anaelezea mfano wa alama na ishara (Symbols) hizo ni kama bendera ya taifa.
Anaelezea kwa mfano baada ya mashambulizi ya kihalifu yaliyotokea New York, Marekani, tarehe 11 Septemba 2001 (9/11), Wamarekani wengi walikasirishwa kwamba bendera ya Marekani ilikuwa ikipeperushwa kiholela kila kona, mchana kutwa na usiku kucha bila ya kuwashiwa taa iwe bendera yao inaonekana au iwe inang’aa unapoingia usiku. Kwasababu bendera kitaifa ni moja wapo ya vitu vitakatifu, na kwa hivyo, ni imani ya vitu vinavyoonekana.
Kila taifa lina alama zake na ishara zake takatifu ambazo zinawakilisha na zinaashiria hisia na historia ya taifa. Alama na viashiria hivyo vinaweza kuwepo kwenye bendera ya taifa, au bendera za dola (serikali), au bendera ya chama cha siasa, au bungeni, au mahakamani. Kwa mfano nchini kwetu Tanzania, tuna bendera, mwenge, wimbo wa taifa, na hata utaratibu wote wa kuapishwa kwa viongozi wa taifa, gwaride la jeshi, sikukuu ya mashujaa, na sikukuu ya uhuru. Zote hizi ni ishara na alama za vitu vitakatifu kwa taifa.
Kinyume cha kitu kuwa kitakatifu (Sacred) ni uovu (Profane). Kutokana na maelezo ya Bwana Alexander, J. (2012, Uk. 70) anaelezea maana ya Profanemaana yake ni vitu vinavyoashiria na vinavyofungamana na ubaya na uovu. Kwa mfano, shetani au ibilisi ni mifano ya vitu vyenye maana ya kuwa Profanekutokana na dini ya Kiislamu na dini ya Kikristo. Kitaifa, mfano mmoja wapo unaoashiria kitu kuwa Profane (kiovu) ni kuikanyaga bendera au kuichoma bendera ya taifa au ya chama, au kuitupa, au kuikanyaga kofia ya jeshi na vitu vyote vinavyohusiana na alama za taifa ikiwemo nembo ya serikali.
Kutokana na ufafanuzi huo, mwanachuoni mwingine, Bwana Ėmile Durkheim (1915) yeye kaenda mbali zaidi na akafafanua zaidi juu ya maana ya dini kuwa Functional (kuamini vitu vinavyoonekana) ni kwamba dini ni mfumo wa imani na matendo ambayo yanawaleta watu pamoja kwa vitu wanavyoviona kwao ni vitu vitakatifu […]. Hiyo ndiyo maana ya dini kwa mwanachuoni Bwana Ėmile Durkheim (1915, Uk. 47).
Tumeona kwamba maana ya dini imefafanuliwa katika makundi mawili kutokana na wanazuoni wa kisayansi. Maana ya kwanza ni kuamini vitu vinavyoonekana (alama na ishara), na maana ya pili ni kuamini vitu au nguvu zisizoonekana (Mwenyezi Mungu). Katika ufafanuzi wa vitu ambavyo vinavyoonekana, kisayansi, ndiyo inaingia nafasi ya dola (siasa). Kivipi?
Nchi moja wapo ya kutolea mfano huu wa alama na ishara zinazonasabishwa na taifa, ni Marekani (USA). Kutokana na uchambuzi wa kisayansi wa Bwana Robert Bellah (1967, Uk. 1) anadai kwamba taifa la Marekani lenyewe lina dini yake ambayo inaitwa Civil Religion (Dini ya kutumikia watu).
Sina shaka kwamba mtazamo wa Bwana Robert Bellah, umetokana na uchambuzi wa Bwana Ėmile Durkheim (1915) kwamba dini ni kuamini vitu vinavyoonekana, na ni mfumo wa imani na matendo ambayo yanawaleta watu pamoja kwa vitu wanavyoviona kwao ni vitu vitakatifu […]. Kwa mfano bendera, au mkusanyiko wa kuapishwa kwa viongozi wa taifa.
Bwana Robert Bellah ameendelea kusema kwamba Civil Religion (Dini inayowatumikia watu kitaifa) ipo nchini Marekani, lakini watu hawaitambui kama ipo katika maisha yao ya kila siku. Kwa kumaanisha maana ya dini kutokana na ufafanuzi wa kisayansi.
Civil Religion (Dini ya kutumikia watu) inatambulikana kuwa ni nguvu ya dola ambayo inaongozwa na kiongozi (Rais) ambaye ana imani na Mwenyezi Mungu, kwa kuwaongoza watu ambao pia wengi wao wana imani na Mwenyezi Mungu. Watu hao wanaoongozwa ni watu ambao siyo wa dini moja, lakini wapo kwenye mfumo maalum wa kuendesha maisha yao ya kila siku ya kijamii katika taifa. Sababu kubwa ya kuifanya nchi iende na mfumo huu, ni kuitenganisha dola (siasa) na dini. Kutenganisha dola (siasa) mbali na dini kwa kuipa dini uhuru katika jamii, ambacho ni kitu binafsi kwa kila mtu akiwemo rais wa nchi, na kuipa dola nafasi ya kuwaongoza watu wa dini mbalimbali.
Kwa mfano, marais wote wa Marekani, na marais wengi duniani wakiapishwa kuwa rais, lazima wamtaje Mungu (God) au sifa zake kwenye viapo vyao, na wengine humtaja Mungu au sifa zake kwenye hotuba zao za kwanza au za pili au zote, za kuapishwa kuwa rais wa nchi. Kwa mfano, Rais wa kwanza wa Marekani, Mheshimiwa Rais George Washington, kwenye hotuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa rais, alimtaja Mungu kwa sifa zake tu na hakutumia neno Mungu. Alimtaja kwa sifa yake na akasema:
“The Almighty Being who rules over the Universe”
Maana yake, “Mwenye nguvu (Mwenye Rehema) anayetawala Ulimwengu wote”
Kuanzia Rais wa kwanza wa Marekani, Mheshimiwa George Washington mpaka Rais wa nne wa Marekani wote walikuwa wakimtaja Mungu kwa sifa zake kwenye hotuba zao na hawakutumia neno Mungu (God). Na kwenye hotuba ya pili ya Mheshimiwa George Washington, hakumtaja Mungu na wala hakutaja sifa zake. Ilikuwa hotuba fupi sana yenye mistari michache (paragraph 2). Neno God lilianza kutajwa na Rais wa tano wa Marekani, Mheshimiwa James Monroe, ndiye kwa mara ya kwanza alilitaja neno Mungu (God) kwenye hotuba yake ya kuapishwa baada ya kuchaguliwa tena kwa mara ya pili kuwa rais wa Marekani, tarehe 05 Machi 1821. Na marais wengine waliyofuata waliendelea hivyo hivyo ama kumtaja Mungu kwa sifa zake, au kutaja neno Mungu (God) kwenye hotuba zao za kuapishwa kuwa rais (Bellah, 1967, Uk. 13).
Mfano mwingine wa rais wa nchi kutambua uwepo wa Mungu na kumtaja kwenye hotuba yake ni rais wa thelathini na tano wa Marekani, Mheshimiwa John F. Kennedy (1961) katika hotuba yake maarufu alisema:
“…the rights of man come not from the generosity of the state but from the hand of God.”
Maana yake, “haki ya mtu haiji (au haipatikani) kutokana na mkono wa dola, bali inapatikana kutokana na Ufalme wa Mwenyezi Mungu.”
Pamoja na kuwa ni rais wa dola, dola ambayo ina miongozo yake, lakini Rais John F. Kennedy anaamini kuwa dola na watu wake, imo mikononi mwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu. Kwa rais kuchagua neno Mungu kwenye hotuba, ni kutamalaki nchi na watu anaowaongoza kwa niaba ya Mwenyezi Mungu.
Mfano mwingine, ni rais wa arubaini na tano wa Marekani Mheshimiwa Donald J. Trump (Mungu amsaidie), katika hotuba yake ya kuapishwa kuwa rais (2017) naye pia alimtaja Mungu kwa kusema:
“…how good and pleasant it is when God’s people live together in unity.”
Maana yake, “…uzuri na raha ilioje, watu wa Mwenyezi Mungu wanapoishi pamoja kwa umoja wao.”
Kwa nchini mwetu mfano, Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli, ambaye ni muumini mzuri wa dini ya Kikristo na ni mwenye kuamini uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kwa mfano, tarehe 04 Februari 2018, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alihudhuria sherehe za kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa tano, wa kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam. Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais alisema:
“Sisi viongozi wa serikali, mara nyingi huwa tunawategemea viongozi wa makanisa na viongozi wa misikiti kutuongoza. Nafahamu serikali haina dini, lakini inaheshimu sana dini. Inaheshimu na kuthamini sana mawaidha na mafundisho yanayotolewa na dini, wawe Waislamu, wawe Wakristo, wawe Wahindu, tunayaheshimu sana. Na siku zote sisi viongozi ndani ya serikali huwa tunafurahi sana unapoona makanisa na misikiti imetulia. Unaposikia mahali fulani fulani kuna migogoro, sisi viongozi na hasa mimi huwa ninajiuliza, ninapopata matatizo nitakimbilia wapi? Kwasababu makanisa na misikiti ni mahali pa uponyaji wa roho zetu.” (Magufuli, 2018).
Hotuba hii, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa hekima zake, amefafanua kifalsafa tofauti baina ya dola (siasa) na dini kwa wananchi wa Tanzania. Na sote tunajua kwamba Mheshimiwa Rais binafsi yake ni muumini mzuri sana wa Mungu, na katika nasaha zake mara nyingi huwa anasema “Mtangulize Mungu”, “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu”, na kadhalika. Na mara moja moja hutumia aya mbalimbali za Biblia katika kupeleka ujumbe wake, lakini pia mara nyingine anapoona kofia ya dola inatakiwa kuvaliwa kwa maslahi mapana ya taifa, kwa hekima zake huwa anatuma ujumbe wake kwa lugha inayomtambulisha yeye akiwa kama ni rais wa dola nzima ya watu anaowaongoza.
Hivyo hivyo, Bungeni kwetu, kuanzia utaratibu wa kuingia kwa Spika wa Bunge au Naibu Spika wa Bunge bungeni, na dua ya kuliombea taifa ambayo husomwa na Spika au Naibu wake yote haya ni mfano wa alama na ishara za Civil Religion (Dini ya kuwatumikia watu) kama anavyoichambua Bwana Robert Bella (1967). Dua ya kwenye bunge inasema:
“Ewe Mwenyezi Mungu mtukufu, muumba mbingu na dunia. Umeweka katika dunia serikali za Wanadamu na Mabunge ya mataifa ili haki yako itendeke. Twakuomba uibariki nchi yetu idumishe uhuru, umoja, haki, na amani. Umjaalie Rais wetu hekima, afya njema, na maisha marefu ili pamoja na wanaomshauri wadumishe utawala bora. Utuongezee hekima na busara sisi Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na utupe uwezo wa kujadili kwa dhati mambo yatakayoletwa mbele yetu leo ili tufanye maamuzi sahihi yenye manufaa kwa watu wote na ustawi wa nchi yetu. Amin.”
Kwahiyo, kutokana na nadharia ya ufafanuzi wa dini wa Bwana Max Weber (1905), na nadharia ya Bwana Ėmile Durkheim (1915), na nadharia ya Bwana Robert Bellah (1967), kwa umoja wake, ni mfumo mzima wa kuwahudumia watu kitaifa ambao una alama zake, matendo yake, na ishara zake, na utamaduni wake. Ni mfumo unaoitwa Civil Religion (Dini ya kutumikia watu).Kwa sisi Tanzania, ama tukubali kuwa hiyo ndiyo maana yake au hiyo siyo maana yake mbali na vile Bwana Robert Bellah (1967) alivyokusudia kwa taifa la Marekani, ni juu yetu kutafakari, na kuchambua zaidi. Tanzania tuna utamaduni wetu katika ngazi ya taifa, iwe ni mikutano ya serikali, au hotuba zinazowakilishwa na serikali. Utamaduni huo umetuweka kwa amani na usalama.
Nchi nyingi zimejaribu kuweka mambo ya siasa na dini mbali kwasababu ya hofu ya maingiliano ya dini na siasa zinaweza kuleta machafuko ndani ya nchi, au pengine wameshindwa kuchambua tofauti zake, au pengine kwa sababu zao za kisiasa tu (Secularism?). Tanzania tumeweza kuziweka siasa na dini bega kwa bega na tumedumisha amani mpaka hivi sasa. Siyo kwasababu tuna umahiri kuliko nchi nyingine, au yaliyotokea nchi nyingine hayawezi kutokea nchini kwetu, ila ni kwasababu ya dola (siasa) na dini kuheshimiana na kutumika pamoja kwa faida ya wananchi wanaowaongoza ambao wamekua na misingi hiyo ya kuheshimiana.
Siku pale dola itakapoamua kuitenga dini moja kwa kuitengenezea picha kwa jamii kuwa ni dini hatarishi katika maisha yao ya kila siku, au kuinasabisha dini moja wapo na uhalifu kwasababu zinazotokana na utandawazi wa kisiasa au sababu nyingine zozote. Hapo ndiyo itakuwa mwanzo wa sisi wenyewe kujichimbia shimo iwapo kama bado hatujafikia huko. Kwasababu sisi Watanzania tunajijua utamaduni wetu pamoja na kuwa na dini zetu mbalimbali. Kama viashiria hivyo vipo hivi sasa au vitajitokeza baadaye, ni bora tuanze kuviepuka kuanzia hivi sasa na mapema. Kwasababu nguvu za dola na nguvu za watu zinapokutana hakuna mshindi. Lakin sote tunajua kwamba Serikali siku zote ina nguvu!
Kuna baadhi ya watu nchini kwetu huona kuwa anapoingia rais Muislamu, basi nchi yote ishakuwa ni nchi ya Kiislamu, na kuna baadhi ya watu huona kuwa anapoingia rais Mkristo, basi nchi yote ishakuwa ya Kikristo. Nadharia hii na majigambo haya yanaleta mipasuko katika jamii, chuki, na kutoana Imani katika taifa lenye kuamini uhuru na umoja. Tanzania, watu hawawezi wakawa wanaishi kwa mitego mitego kwenye ngazi zote zinazohusu maslahi ya taifa kwa kutoaminiana kutokana na sababu za kidini. Hakuna dini yoyote ndiyo mlinzi wa nchi ya Tanzania. Dini zote zinawakilishwa na Watanzania. Hofu zisizotuhusu zinazojengewa miongoni mwetu kama Watanzania, ni kuchotwa akili ili shetani apite na yake. Uzalendo wa kila mmoja wetu ndiyo utakaolifanya taifa hili kuendelea kuwa taifa la imani. Kwa wenye kufikiri!
Muwakilishi wa chombo cha dola au mwanasiasa ambaye ni Muislamu ni lazima kuheshimu wanasiasa wenzake na kuheshimu anaowawakikilisha ambao ni wa dini nyingine tofauti na Uislamu na kulinda na kuyatetea maslahi yao. Na muwakilishi wa chombo cha dola au mwanasiasa ambaye ni Mkristo ni lazima kuheshimu wanasiasa wenzake na kuheshimu anaowawakilisha ambao ni wa dini nyingine tofauti na Ukristo na kulinda na kuyatetea maslahi yao. Viongozi wa dini kutoa nasaha za hekima na kuheshimu viongozi wa dola, na viongozi wa dola wanapoongea na viongozi wa dini vilevile kutoa nasaha za hekima na kuheshimu viongozi wa dini pale wanapotuma ujumbe wao kwa viongozi wa dini. Bila ya kutoka kwenye misingi yetu ya kisiasa dola isisite kumchukulia hatua za haraka kwa kiongozi yeyote aliyepewa mamlaka ya kiserikali kisha akatumia nafasi yake kuidhalilisha dini nyingine, ili tuweze kulinda amani kabla ya watu kuanza kupaza sauti zao.
Kazi yangu katika sehemu ya makala hii, ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa kisayansi ili kutaka kuisaidia nchi yangu kuleta maana ya wazi, na maana tofuati baina ya dola (siasa) na dini nchini kwetu Tanzania. Uwazi huu matarajio yake ni kuleta tanabahi ya ufahamu wa tofauti baina ya dola (siasa) na dini uweleweke zaidi, na jinsi dola (siasa) na dini zinavyochukua nafasi zao katika jamii ya Watanzania ili nchi yetu iendelee kuwa ni nchi ya amani.
Kwa ujumla niseme kwamba, zaidi ya miaka elfu saba iliyopita, historia ya mwanadamu inaonyesha, maendeleo ya kila jamii iliopo sehemu yake, huchukua muda mrefu mpaka kufikia maendeleo ya kiteknolojia. Kutokana na mtiririko wa historia tuliyoiona hapo juu, utafiti wangu unaonyesha kwamba iwapo wakoloni wasingekuja Afrika, Afrika tungepiga hatua kidogo kidogo sisi wenyewe na mpaka kufikia maendeleo ya teknolojia ambayo yangetokana na ustadi, utamaduni, desturi na mila zetu wenyewe hata kama ingechukua miaka 1000 mingine ijayo. Afrika tumeharakishwa sana na maendeleo, wakati sisi wenyewe tulikuwa bado hatupo tayari kujifinyanga kwenye yale yanayoitwa maendeleo ya mtazamo wa watu wa magharibi.
Kwa upande mwingine, Afrika ingekuwa ndiyo bara linaloongoza kwa maendeleo kuliko bara lolote duniani kutokana na nguvu walizokuwa nazo Ufalme wa Kandake uliotawala Afrika ya Nubi miaka ya 40 B.C. (miaka 4000 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo), yaani takriban miaka 6000 iliyopita. Lakini tulipo hapa tulipo si vingine, bali ni mapenzi na rehema za Mwenyezi Mungu kwa kuwapenda waja wake wote, Wana wa Adam wa Mungu mmoja, Mungu wa ulimwengu wote.
Baada ya miaka ya 50 (1950s) ya kipindi cha mkoloni ambayo nadharia ya Modernisation na Secularisation imeanza kusambazwa duniani, na mpaka ikaingia miaka ya 60 (1960s), baba yetu wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ameshajiandaa katika harakati za kutukomboa kutoka kwenye makucha ya wakoloni kwa kuunda chama cha TANU (sasa CCM) na mpaka kufikia uhuru wetu mwaka 1961. Miaka 56 imepita tangu tupate uhuru hatuna budi bali ni kuangalia nyuma, kuangalia kulia, na kuangalia kushoto kisha kupiga hatua moja nyuma, na kutafakari wapi tulipo na wapi tunataka kuelekea katika hii njia panda. Hatutaki kuendelea au kurudi kwenye ukoloni, na hatutaki kurudi kwenye uchifu na ukabila. Umoja wa kitaifa ndiyo suluhisho kwenda mbele.
Mbali na hayo, ningependa kuongezea ushauri kuhusu historia za kimila na desturi zake na za Kichifu, serikali iwekeze kwenye kulinda, na kuhifadhi mila na desturi za nchi na historia zake kwa kila makabila, na kuhifadhi makazi ya machifu na hazina zao za kiasili katika maeneo yao ya asili kwa vizazi vijavyo ili wajue wapi wanatoka. Siyo uamuzi wa mtu mmoja mmoja binafsi anavyojisikia yeye, au anavyohisi yeye, bali ni kwa hazina ya taifa. Nchi nyingi zimefanya hivyo kulinda historia yao na kuboresha maeneo yao ya kimila. Kwa mfano nchi zilizoendelea kama (Uingereza) na hata baadhi ya nchi za Afrika (Afrika Kusini) walivyohifadhi sehemu za historia zao na mila zao na sehemu hizo zimekuwa ni sehemu mojawapo kubwa kwa vivutio vya watalii. Mwalimu Nyerere alisema: “Taifa lisilokuwa na utamaduni wake ni taifa mfu”. Na Chifu wa Kabila la Wasafwa, Mbeya, Mwene Mwashinga (2017) alipohojiwa na Michuzi TV, wasia wake mkubwa alisema: “Tunasema nyinyi watoto, mkumbuke mlikotoka”. Kulinda mila (zinazofaa), kulinda desturi, na kulinda utamaduni wa taifa ni tunu na hazina ya kila taifa. Dini imekuja kuleta muongozo sahihi wa watu ili iwe rehema kwao kuelekea kwenye mfumo wa dunia kuwa kijiji.
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ameanza kutuonesha njia kuwa tukikusudia tunaweza. Na mambo mengi yamefanyika ndani ya miaka miwili ya uongozi wake kuliko miaka 56 ya uhuru iliyopita. Kiongozi wa kila awamu iliyopita, kafanya kila alichokiweza kukifanya kwa mustakbali wa taifa, na kuna mengi yanatakiwa kufanywa iwapo tutakuwa na umoja na kuwacha tamaa za mpito na tamaa binafsi za kuliangamiza taifa au kuiangamiza jamii. Haijalishi jamii hiyo udogo wake vipi. Mustakbali wa Watanzania, umo mikononi mwa Watanzania. Tuna mengi yanayotufanya tuwe wamoja kuliko yale yanayotufanya tutengane. Lakini angalau wengine miongoni mwetu tutaweza kukiambia kizazi kijacho, nimefanya nilichoweza kukifanya, nimesema nilichoweza kukisema kile kilicho ndani ya uwezo wangu kwa kuisemea nchi yangu Tanzania. Kifua changu cheupe, na moyo wangu upo furahani kwa matarajio ya kujua ya kwamba kizazi kijacho kwao ‘Sina deni’.
Mwisho wa sehemu ya kwanza.
Imeandikwa na:
Saleh J. Katundu
11/02/2018
Itaendelea…
MAREJEO:
Alexander, J., Thompson, K. & Edles, L. (2012) A Contemporary Introduction to Sociology. 2nd ed. Colorado, USA: Paradigm Publishers.
Bellah, R. (1967). ‘Civil Religion in America.’ Daedalus, 96(1), pp. 1-21.
Chama Cha Mapinduzi (2015) Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 – Umoja na Ushindi. Tanzania: Chama Cha Mapinduzi.
Durkheim, Ė. (1915) The Elementary Forms of the Religious Life. London: Hollen Street Press Ltd.
Jefferies, J. (2005) Focus on People and Migration. 1st edition: Palgrave Macmillan UK.
Katundu, S. (2017) Utandawazi wa Uchumi Nchini Tanzania. [Online] Available at: https://sjposters.wordpress.com/2017/03/07/utandawazi-wa-uchumi-nchini-tanzania/ [Accessed: 11 February 2018].
Katundu, S. (2016) Shule ya Sekondari Tegeta Waandamana Baada ya Kupoteza Mwaka Mzima Bila ya Elimu. [Online] Available at: https://sjposters.wordpress.com/2016/10/11/shule-ya-sekondari-tegeta-waandamana-baada-ya-kupoteza-mwaka-mzima-bila-ya-elimu/ [Accessed: 11 February 2018].
Kennedy, J. (1961) President Kennedy 1961 Inaugural Address. [Online] YouTube. Available at: https://youtu.be/BLmiOEk59n8 [Accessed 11 February 2018].
Lenin, V. (1916) ‘The Socialist Revolution and the Right of Nations to Self-determination’. Vorbote, No. 2.
Magufuli, J. (2018) Hotuba ya Rais Dkt. Magufuli Baada ya Kusimikwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dsm. [Online] YouTube. Available at: https://youtu.be/36i0eEwGuGg [Accessed 11 February 2018].
Mwashinga, C. (2017) Huyu Ndiye Chifu wa Kabila la Wasafwa Mbeya, Chifu Mwashinga. [Online] YouTube. Available at: https://youtu.be/z5zcDxqnOwo[Accessed 11 February 2018].
Pountney, L. & Maric, T. (2015) Introducting Anthropology. 1st ed. Cambridge: Polity Press.
Tylor, E. B. (1871) Primitive Culture: Researches into the Development of Mythology, Philosophy, Religion, Art and Custom. London: John Murray.

No comments: