Tuesday, January 30, 2018

WLAC YAANZA KUTOA MAFUNZO KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA,UKEKETAJI WILAYANI IRAMBA

Na,Jumbe Ismailly IRAMBA

KITUO cha Msaada wa sheria kwa Wanawake( WLAC) kimeanza kutoa mafunzo ya kutokomeza ukatili kwa kijinsia na ukeketaji pamoja na madhara yake kwa watoto wa shule za msingi za Nguvumali,Songambele na sekondari ya Ndago wilayani Iramba,Mkoani Singida ambapo katika kipindi cha wiki moja jumla ya wanafunzi 600 kutoka katika shule za msingi na sekondari walinufaika na mafunzo hayo.

Mwanasheria kutoka Kituo cha Msaada wa sheria na Wanawake (WLAC) Abia Richard aliyasema hayo kwenye mafunzo waliyotoa kwa wananchi wa Kijiji cha Zinziligi,Tarafa ya Ndago,wilayani Iramba.

Aidha Mwanasheria huyo wa WLAC alifafanua kwamba katika kipindi hicho cha wiki moja zaidi ya watu 1000 wameshapatiwa mafunzo hayo ambayo kati ya hao wanafunzi wa darasa la tano mpaka la saba wa shule za msingi na kidato cha kwanza hadi kidato cha nne ni 600 na watu wazima ni 500.

Akizungumzia sababu za kwenda kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi,Abia amezitaja kuwa  ni kizazi na taifa la kesho,jambo ambalo endapo wakifahamu madhara yake mapema watakapokuwa wakubwa itakuwa rahisi kuepukananavyo.Kwa mujibu wa Abia kituo cha msaada wa sheria na Wanawake na watoto kikifadhiliwa na The Foundation For Civil Society kimekuwa kikiendesha mradi wake wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake pamoja na kuzuia vitendo vya ukeketaji kwa wanawake.

“Kwa hiyo tumefika katika wilaya ya Iramba,kata ya Ndago katika Kijiji cha Zinziligi kwa ajili ya kuongea na wanakijiji wa Zinziligi kujua ni aina gani ya ukatili wa kijinsia ambao unakumbana na wananchi wa Kijiji hicho pamoja na kupanga mkakati ni kwa namna gani wananchi hao wataepukana na ukatili huo”alisisitiza Mwanasheria huyo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Ndago,Abeli Philipo Shalua alithibitisha kwamba asilimia 85 ya wanawake ndiyo wanaonyanyasika sana kwa waume zao na kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka jana mpaka sasa kuna matukio ya ukatili wa kijinsia 13 waliyofanyiwa wanawake.

Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT Zinziligi,Rejina Matoke huku akinukuu maandiko matakatifu aliweka bayana kuwa kitu kinachouwa nyumba za familia nyingi na kushindwa kuendelea ni tamaa ya uzinzi kwani hivi sasa suala la uzinzi limekamata watu wengi.“Zinziligi imekamatwa na uzinzi nasema ile kweli halafu kuna magonjwa ya kutisha hapa,hata kama leo daktari ataleta kipimo watakaopona ni wachache,idadi kubwa hapa ni taabu tu,watu hawajiheshimu”alisisitiza Mchungaji huyo.
 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Zinziligi,tarafa ya Ndago,wilayani Iramba wakiwa kwenye viwanja vya mikutano ya Kijiji hicho wakipatiwa mafunzo na Kituo cha Msaada wa sharia kwa wanawake (WLAC) juu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na ukeketaji pamoja na madhara yake.
Bi Esther Kileee (aliyemshikilia mkono ni Afisa mtendaji wa kata ya Ndago) kwanza    akitoa ushuhuda wa kuacha kujishughulisha na vitendo vya ukeketaji baada ya kuokoka na kwamba kabla ya kuokoka alikuwa akinufaika na shughuli hizo kwa kumpatia kipato chake na alaikuwa akiwakeketa wanawake wasiopungua 50 kwa mwezi.
  Mwanasheria wa WLAC,  Abia Richard akiwasilisha mada kwa wananchi wa Kijiji cha Zinziligi,Kata ya Ndago,wilayani Iramba ambapo pamoja na mambo mengine alisema katika kipindi cha wiki moja zaidi ya watu 1000 walipatiwa mafunzo na kati yao,wanafunzi ni 600 na watu wazima ni 500.
 Mwanasheria wa WLAC, Abia Richard ajiteta jambo na afisa mtendaji wa kata ya Ndago, Abeli Philipo Shaluo.


Igizo linaloashiria mwanaume anayemnyanyasa mkewe kwa kumfanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia.(Picha  zote Na Jumbe Ismailly)

No comments: