Tuesday, January 30, 2018

RC MNYETI AMTUMIA MBUNGE OLE MILLYA, SALAMU ZA KUACHA JIMBO LA SIMANJIRO

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, amemtumia salamu mbunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya (Chadema) kutumia nafasi hii kuagana na wananchi wake kwani hawezi kushinda tena ubunge wake mwaka 2020.

Mnyeti aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa nyumba sita za walimu wa shule ya sekondari Emboreet kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation.

Alisema Ole Millya anapaswa kuanza kupita kwenye vijiji vya jimbo hilo kwa ajili ya kuaga wananchi wake sababu hivi sasa wanataka kuongozwa na mbunge wa CCM.

"Mfikishieni salamu zangu rafiki yangu Ole Millya kwani tulikuwa naye CCM na namuhakikishia hawezi kuwa mbunge wa jimbo la Simanjiro mwaka 2020 kwa sababu CCM italirudisha hivyo aanze kuaga kabla hajaondoka," alisema Mnyeti.

Hata hivyo, Ole Millya alisema Mnyeti ni kijana mwenzake wanayeheshimiana na waliyefahamiana kwa muda mrefu tangu wakiwa UVCCM, hivyo haamini kama maneno hayo yametoka kinywani mwake.

Alisema Simanjiro aliyoikuta wakati anachaguliwa mwaka 2015, ilikuwa imeharibiwa kwa siasa za maji taka, rushwa zinazodhalilisha utu wa watu na uuzaji wa ardhi uliokithiri.

"Kama nia yetu ni maendeleo kwa wananchi tunaowaongoza ni muhimu kushirikiana ili lengo litimie na Mungu akitufikisha mwaka 2020 wananchi waamue nani wa kumpa kura kwenye nafasi ya Udiwani, Ubunge na Urais," alisema Ole Millya.

Mnyeti alitumia nafasi hiyo kumpigia debe mkuu wa wilaya mstaafu Peter Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa shirika la ECLAT lililowekeza kwenye shule ya sekondari ya kidato cha sita Emboreet.

"Hili jimbo lipo wazi kwani linashikiliwa na upinzani, hivyo ndugu yangu Toima anza kupitapita huku na huku ili uchukue ubunge na mimi nitakuunga mkono kwa asilimia 100 kwani wewe ni mtu wa maendeleo," alisema Mnyeti na kuongeza:

"Wana Simanjiro mkiwa na mtu kama Toima ni sawa na kuwa na wabunge 20 hivyo msimuache kwani yeye hana ubalozi hata wa nyumba 10 lakini amefanya maendeleo mengi, nami nitamuunga mkono kwani siyo mbabaishaji," alisema Mnyeti.

Alisema Toima anapenda kunyanyua jamii yake kielimu kwani ipo nyuma mno ndiyo sababu anapaswa kuungwa mkono na kupongezwa kutokana na mchango mkubwa wa elimu alioutoa kwenye eneo hilo.

Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, Peter Toima alisema shirika hilo lilianza shughuli za ufadhili wilayani humo na kwenye shule ya sekondari Emboreet kwa mwaka 2015 hadi mwaka 2019 wametumia bajeti ya sh2.8 bilioni na mradi ukikamilika baada ya miaka sita zitakuwa zimetumika sh3.5 bilioni.

Toima alisema shule hiyo ya sekondari Emboreet ndiyo pekee wilayani Simanjiro yenye kidato cha sita na kwenye matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka huu shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya.

"Tuliona eneo hili la wafugaji linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu bora ndiyo sababu tukajenga shule hii ambao sasa hivi zaidi ya wanafunzi 200 wanalala kwenye mabweni ikiwemo wanafunzi 40 wa kidato cha sita," alisema.

Alisema wamepanga bajeti ya sh480 milioni, kwa ajili ya ukamilishaji wa chuo cha ufundi stadi Veta ambacho ni pekee kilichopo wilayani humo ili kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi.

Alisema hadi kufikia mwezi Octoba mwaka huu, mradi wa chuo hicho cha Veta, utakuwa tayari na utaanza kwa wanafunzi 24 watakaojihusisha na masomo ya ufundi uashi.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kwenye ziara yake ya siku saba ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kusikiliza kero zao na kuzungumza nao kwa kutoa maagizo na maelekezo mbalimbali kwa wananchi na viongozi wa eneo hilo.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizindua ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya kidato cha sita ya sekondari Emboreet, Wilaya ya Simanjiro iliyojengwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation kwa kuchimba msingi kwa kutumia jembe.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti (mwenye shati la maua) akimsikiliza Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation, Peter Kiroiya Toima, juu ya ujenzi wa chuo cha ufundi cha Veta, ambacho kimejengwa na shirika hilo.

No comments: