NA ESTOM SANGA-MBEYA
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Mkuchika amewatembelea Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuwataka kuongeza jitihada zaidi za kujitegemea kwa kutumia ruzuku wanayoipata kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili kukuza kipato chao.
Mheshimiwa Mkuchika amesema jitihada za serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF za kuhamasisha wananchi kuuchukia umasikini haziwezi kuwa endelevu ikiwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini hawatatumia fedha wanazozipata kubuni miradi ya uzalishaji mali.
“hiki mnachokipata kutoka serikalini kupitia TASAF kiwe chachu ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili hatimaye muweze kujitegemea” amesisitiza Waziri Mkuchika.
Akiwa katika eneo la Shule ya Sekondari ya Lupeta katika jiji la Mbeya , shule ambayo TASAF imejenga jengo la Utawala na Maabara,Waziri Mkuchika ameeleza kuridhishwa na matokeo ya ujenzi wa majengo hayo na kupunguza kero iliyokuwa inawakabili walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Aidha Mheshimiwa Mkuchika amekutana na vikundi vya uzalishaji mali vilivyoanzishwa na Walengwa wa TASAF kwa kutumia ruzuku ya fedha kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo walengwa hao wamekuwa wakikopeshana fedha zinazotokana na uzalishaji wa bidhaa zikiwemo mikeka,na hivyo kuwaongezea uwezo wa kuhudumia kaya zao.
Hata hivyo Waziri huyo ametoa maagizo kwa uongozi wa mkoa wa Mbeya kuhakikisha kuwa watu wanaonufaika na fedha za ruzuku kutoka TASAF ni wale wanaokidhi vigezo vya umasikini na kutaka fedha zilizolipwa kwa watu wasiostahiki zirejeshwe mara moja.
“rejesheni fedha za serikali ili ziwanufaishe walengwa wanaostahiki kupata ruzuku hiyo kama ilivyokusudiwa na serikali” ameonya Waziri Mkuchika.Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bi. Mercy Mandawa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuusimamia kikamilifu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ili uendelee kusaidia jitihada za kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.
Amesema tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ,kumekuwa na mwitikio chanya kwa walengwa kutumia ruzuku hiyo kuboresha maisha yao huku mkazo ukiwekwa katika kuboresha elimu,afya na lishe kwa watoto wanaotoka kwenye kaya za walengwa huku akisisitiza juu ya matumizi sahihi ya ruzuku inayotolewa kila baada ya miezi miwili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (aliyevaa suti nyeusi) akikagua bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa TASAFkatika mtgaa wa Inyala katika jiji la Mbeya kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
Waziri Mkuchika (aliyevaa tai) akimsikiliza mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lupeta katika jiji la Mbeya alipotoa maelezo ya maabara iliyojengwa na TASAF shuleni hapo.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akikagua jengo la maabara lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika shule ya Sekondari ya Lupeta katika halmashauri ya jiji la Mbeya.
No comments:
Post a Comment