Sunday, January 21, 2018

WALIMU WAWILI KIBAHA WASHUSHWA VYEO KWA KUKAIDI AGIZO LA ELIMU BURE


Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

MKUU wa wilaya ya Kibaha,Mkoani Pwani, Assumpter Mshama ameamuru walimu wawili wa shule za msingi washushwe vyeo kutoka nafasi ya mwalimu mkuu na kuwa walimu wa kawaida ,kutokana na kosa la kuchangisha michango wazazi.

Hatua hiyo ,ameichukua siku chache baada ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,kukemea tabia inayofanywa na baadhi ya walimu wakuu na bodi za shule kuchangisha wazazi na walezi michango ambayo serikali imeizuia.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ,alisema walimu hao wamekiuka agizo la serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk .John Magufuli .

Mshama aliwataja walimu hao kuwa ni mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Miembesaba, Rashinde Kilakala ambaye alikuwa akipokea sh.1,000 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya mitihani jambo ambalo ni kinyume cha agizo la serikali.

Mwalimu mwingine ni wa shule ya msingi Jitegemee, Sapiensia Kilongozi ambae aliweka kikao na kuita wazazi na kuwataka wazazi wenye watoto watoe shilingi 2,000 kwa wiki kwa ajili ya masomo ya ziada na mitihani.

Mshama alisema,huo ni mwanzo kwani ataendelea kusimamia maagizo yanayotolewa na serikali ili iwe fundisho kwa walimu wanaokaidi mipango ya serikali hiyo.Alieleza atakaeendelea kufanya hivyo akibainika atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi .

"Nilipata malalamiko kutoka kwa wazazi kwamba kuna walimu wakuu wa shule hizo wanachangisha wazazi fedha kwa ajili ya michango mbalimbali ambayo imekatazwa na siku chache zilizopita" alisema Mshama.

“Mwalimu huyu wa shule ya Miembesaba hana kibali wala hajapeleka barua na hakuwa na sababu wala kibali cha kufanya hivyo ambapo mtihani wa mwisho wa mwaka kila mtoto hutoa 1,000 na alikuwa hatoi risiti,” 

“Lazima tumheshimu Rais kwani juzi tu kaongelea suala la elimu bure,hata kama umechangisha risiti ulitoa hivyo mpumzike nafasi hizo mbaki walimu wakawaida,” alisema Mshama.Aidha anashangaa walimu hao walipata wapi nguvu ya kuwashawishi wazazi na kupokea fedha hizo wakati Rais alishazuia mambo hayo.

Nae mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Jeniffer Omollo alisema suala la kuchangisha michango mashuleni lilipigwa marufuku na walimu waliaambiwa kuwa hawaruhusiwi kuwachangisha wazazi .Alisema kuanzia sasa watawachukulia hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Kwa upande wake mwalimu Kilakala alisema anashindwa kueleza kwani walikubaliana na wazazi lakini wakamgeuka kuwa walikuwa wakichanga kinyume cha taratibu hata hivyo hawezi kusema zaidi.

Mwalimu wa shule ya msingi Jitegemee Sapiensia Kilongozi yeye alijieleza":niliitisha kikao cha wazazi na kujadili masuala ya taaluma na wazazi wenyewe waliingiza kipengele wanahitaji watoto wao wasaidiwe kwenye masomo ya ziada na mitihani,” alisema Kilongozi.

Alisema walikubaliana baada ya hapo wakaandika muhutasari lakini baadhi ya wazazi walikuja huku kueleza lakini nia na madhumuni ilikuwa ni kufuata taratibu kwani asingeweza kutoa maamuzi ya kupitisha jambo hilo ,maamuzi lazima yapelekwe kwa ofisa elimu kata na baadaye kwa mkurugenzi.

Kutokana na hali hiyo ,Mshama alisema ni lazima wapate fundisho kwa kushushwa nafasi zao za kazi ili wabaki walimu wa kawaida.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ,Assumpter Mshama ,aliyesimama akizungumza jambo kuhusiana na masuala ya Elimu bure .(picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments: