Thursday, January 18, 2018

WADAU WAJADILI MTAALA WA MAFUNZO KWA VYUO VYA USTAWI

Kamishna Msaidizi Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawke na Watoto Simon Panga akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku moja wa wadau wa Ustawi wa Jamii kutengeneza mtaala wa Ustawi wa jamii kwa vyuo vinavyofundisha masuala ya Ustawi katika ngazi ya Cheti na Diploma jijini Dar es Salaam.
Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Paulo Mwangozi akitoa ufafanuzi wakati wa wa mkutano wa siku moja wa wadau wa Ustawi wa Jamii kutengeneza mtaala wa Ustawi wa jamii kwa vyuo vinavyofundisha masuala ya Ustawi katika ngazi ya Cheti na Diploma jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa wadau wa Ustawi wa Jamii kutengeneza mtaala wa Ustawi wa jamii kwa vyuo vinavyofundisha masuala ya Ustawi katika ngazi ya Cheti na Diploma jijini Dar es Salaam.

……………….

Kamishna Msaidizi Ustawi wa Jamii (Mafunzo) kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bw. Simon Panga amesema utengenezaji mitaala ya taaluma ya Ustawi wa Jamii katika ngazi ya cheti na astashahada itasaidia kuboresha elimu ya ustawi wa jamii nchini.

Panga alisema hayo leo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa Ustawi wa Jamii kutengeneza mtaala wa Ustawi wa jamii kwa vyuo vinavyofundisha masuala ya Ustawi katika ngazi ya Cheti na astashahada leo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Ustawi wa Jamii (Mafunzo), mtaala utakaopendekezwa na wadau utatumika na vyuo vyote Nchini tofauti na sasa ambapo kila chuo kinajitengenezea mtaala na utakuwa umepunguza majukumu na gharama kwa vyuo katika kutengeneza na kuandaa mitaala yao.

Alisema, mtaala pendekezwa unaonzia ngazi ya cheti na astashahada utasaidia kuzalisha maafisa ustawi wa jamii wenye sifa stahiki zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi hasa ikizingatiwa kumekuwa na changamoto nyingi katika masuala ya kiuchumi na kijamii hasa katika masuala ya utumiaji dawa za kulevya, unyanyasaji wa kijinsia na kadhalika.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Paulo Mwangosi alisema lengo la kuwashirikisha wadau katika mkutano wa kukutengeneza mtaala kwa vyuo vinavyotoa elimu ya Ustawi wa jamii ni kuja na mtaala shirikishi utakaotumika na vyuo vyote vya Tanzania ambapo kwa sasa kumekuwa na vyuo vingi na kila chuo kina mtaala wake.

Kwa mujibu wa Mwangosi, kutokuwepo mtaala mmoja unaotumika na vyuo vinavyotoa elimu ya Ustawi wa jamii kunaleta mkanganyiko katika dhana nzima ya utoaji elimu hiyo kwa wanafunzi na kusisitiza kuwa elimu ya ustawi inayotolewa ni lazima ilingane na masuala ya ustawi wa jamii tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi ya vyuo hutoa elimu hiyo na kuchanganya na mafunzo mengine.

Kwa sasa nchini Tanzania kuna vyuo kumi na saba vinavyotoa mafunzo ya Ustawi wa Jamii na kati ya vyuo hivyo vyuo kumi na tano viko Tanzania bara na vyuo viwili viko Zanzibar.

No comments: