Thursday, January 4, 2018

TRA YAJIZATITI KUONGEZA IDADI YA WALIPAKODI




Na: Veronica Kazimoto, 04 Januari, 2018, 
Dar es Salaam. 

Mwaka huu wa fedha wa 2017/18, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imedhamiria kuongeza idadi ya walipakodi kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu kupunguza kutegemea misaada kutoka kwa wahisani. 

Lengo kuu la kuongeza walipakodi ni kupanua wigo na kuongeza makusanyo ambayo hutumika katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi wa nchi. 

TRA ina mikakati mbalimbali ambayo imechukuliwa na inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa, walipakodi wanaongezeka na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. 

Mikakati hiyo ni pamoja na kusajili walipakodi ambapo Mamlaka imezindua kampeni ya usajili wa walipakodi nchi nzima ili kuhakikisha kwamba kila mfanyabiashara anasajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi  (TIN) kwa urahisi na haraka. 

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Kamishna wa Kodi za Ndani Elijah Mwandumbya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania alisema, usajili wa walipakodi ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi na mapato kwa ujumla. 

"Moja ya majukumu ya msingi ya TRA ni Usajili wa Walipakodi ambao huongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, makusanyo pamoja na kutoa taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi ili kuchangia Pato la Taifa", Alisema Mwandumbya. 

Mwandumbya alisisitiza kuwa, walipakodi wadogo wanaostahili kulipa kodi kwa njia ya makadirio, watalipa robo ya kwanza ndani ya siku tisini (90) kuanzia waliposajiliwa tofauti na utaratibu uliokuwepo kwa kulipa kodi hiyo hata kabla mfanyabishara hajaanza kufanya biashara husika. 

"Wananchi wanaostahili kusajiliwa kama walipakodi ni watu wote wanaotarajia kuanzisha biashara, kumiliki vyombo vya usafiri kama vile gari na pikipiki, wanaostahili kulipa kodi ya majengo, wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi na wanaotarajia kupata leseni za udereva", alifafanua Mwandumbya. 

Aidha, Mwandumbya aliyataja mahitaji ya usajili kuwa ni Mkataba wa pango au uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua ya mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ikiwa na muhuri na namba ya simu ya mwenyekiti wa mtaa husika, kitambulisho cha mhusika kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura na mhusika ni lazima aende mwenyewe kwenye ofisi za TRA kwa ajili ya kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole. 

Kamishna Mwandumbya, amewatahadharisha wananchi kuwa makini na vishoka kwa kuwa usajili huo hufanyika bila malipo na hufanyika katika ofisi za TRA na katika vituo maalum ambapo wananchi watatangaziwa kupitia vyombo vya habari na kwenye maeneo husika. 

"Napenda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi wote wanaostahili kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi kuwa makini na vishoka wanaoweza kutumia mwanya huo na kuharibu nia njema ya kampeni hii kwasababu hakuna wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili au hata kutoa fomu ya usajili", ametahadharisha Mwandumbya. 

Elijah Mwandumbya amesema endapo mtu atapata changamoto yoyote katika kusajili na kupata namba ya mlipakodi anashauriwa kuwasiliana na Ofisi ya TRA iliyopo karibu au kupiga simu bure katika Kituo cha Huduma kwa namba 0800 750075 au 0800 780078 au kutuma barua pepe huduma@tra.go.tz au services@tra.go.tz. 

Hatua nyingine ni uwepo wa mifumo mbalimbali ya kielektroniki ya kusajili walipakodi ambayo imerahisisha ulipaji kodi na hivyo kuongeza ulipaji kodi kwa hiari. 

Mifumo hii imepunguza muda wa usajili ambapo kabla ya kutumia mifumo hii ya kielektroniki kazi ya kusajili walipakodi mpaka kukamilika ilikuwa inachukua takribani siku 7 lakini baada ya kuanza kutumia mifumo hii, usajili hufanyika ndani ya dakika 30 tu. 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndugu Richard Kayombo akizungumza ofisini kwake alisema TRA imejiwekea lengo la kusajili walipakodi wakubwa, wa kati na wadogo wapatao milioni moja (1,000,000) kwa mwaka huu wa fedha 2017/18. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya walipakodi na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. 

Kayombo alisema kuwa, mamlaka ina mpango wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanakuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kuongeza ufanisi wa zoezi la usajili kwa kutumia Mfumo wa Vitalu - Block Management System ambao utawezesha kutambua walipakodi wanaostahili kusajiliwa na kulipa kodi. 

Aidha, ameongeza kwamba, mamlaka ina mkakati wa kuongeza idadi ya walipakodi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri au Manispaa mbalimbali ili kuhakikisha kila mfanyabiashara katika maeneo hayo anakuwa na namba ya TIN. Namba hii husaidia kumtambua kila mfanyabiashara mahali anapofanyia biashara yake na kiasi cha kodi anachotakiwa kulipa. 

"Kama mamlaka, tuna mpango wa kuwarahisishia wafanyabiashara muda wa kufanya usajili kwa kupeleka vifaa vya usajili karibu na mahali wanapofanyia biashara kwa ajili ya kuokoa muda wanaoutumia kwenda kwenye ofisi zetu kufanya usajili", amesema Kayombo. 

Kupitia mkakati huu, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itaweza kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara waliopo kwenye sekta isiyo rasmi kwa kuwapatia Kadi ya Utambulisho. Wafanyabiashara hao ni kama vile wenye maduka ya reja reja hasa wenye ma fremu, wamachinga, washereheshaji, wachimbaji wadogo wa madini n.k. 

Uwepo wa idara cha Huduma na Elimu kwa Walipakodi kilichopo ndani ya Mamlaka, ni hatua nyingine ya kuongeza idadi ya walipakodi ambapo idara hi inajishughulisha na kutoa elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi, kujibu hoja mbalimbali pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati muafaka kupitia ujumbe mfupi wa maneno. 




Mikakati na hatua zote zilizobainishwa hapo juu zitaongeza idadi ya walipakodi, uhiari wa kulipa kodi na mapato ya Serikali kwa ujumla.

No comments: