Thursday, January 4, 2018

MATUKIO MAKUBWA NA MADOGO YA JINAI KATIKA MKOA WA MBEYA




 Ifuatayo ni taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha Januari hadi Disemba, 2017. Taarifa hii inaonesha matukio makubwa na madogo ya uhalifu, matukio ya usalama barabarani, matukio yaliyovuta hisia kwa jamii,  hali ya ulinzi na usalama kipindi cha sikukuu ya Kristmasi na mwaka mpya 2018, mpango mkakati wa Jeshi la Polisi Mbeya na mafanikio yaliyopatikana kutokana na operesheni, misako na doria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu kwa mwaka huu 2017.
  1. MATUKIO MAKUBWA NA MADOGO YA JINAI.
Jumla ya makosa ya jinai 26,009 yaliripotiwa kutokea mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha mwaka 2017 ikilinganishwa na matukio 32,943 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho  Mwaka 2016. [-21].
Makosa makubwa yaliyoripotiwa mwaka 2017 yalikuwa ni 2,234 ikilinganishwa na matukio 2,071  yaliyoripotiwa mwaka 2016. [+8] Makosa madogo 23,775 yaliripotiwa  mwaka 2017,  ikilinganishwa na makosa 30,872 yaliyoripotiwa mwaka 2016. [-23].
Aidha jumla ya makosa 734 yaliripotiwa mwaka 2017 kutokana na jitihada za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine kupitia misako, doria na operesheni mbalimbali ikilinganishwa na matukio 565 yaliyoripotiwa mwaka 2016. [+30].
  1. MATUKIO YA USALAMA BARABARANI.
Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani jumla ya makosa yote ya ajali pamoja na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani kwa kipindi cha mwaka 2017 yalikuwa 82,211   wakati kipindi kama hicho mwaka 2016 yalikuwa 66,172. [+24]
Matukio ya ajali kwa mwaka 2017 yalikuwa 244 ikilinganishwa na matukio 393 yaliyoripotiwa mwaka 2016.[-38].  Ajali zilizosababisha vifo mwaka 2017 zilikuwa 141, wakati  mwaka  2016 zilikuwa 182.[-22.5]. Watu waliokufa mwaka 2017 walikuwa 170, wakati mwaka 2016 walikuwa 286. [- 40.5].
Ajali za majeruhi mwaka 2017 zilikuwa 103 wakati mwaka 2016 zilikuwa 211.[-51]  Watu waliojeruhiwa mwaka 2017 walikuwa 268  wakati mwaka 2016 walikuwa 482. [-44]
Pesa zilizokusanywa kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani [notification] mwaka 2017 zilikuwa Tshs 2,380,050,000/=,  wakati kipindi cha mwaka 2016 zilikusanywa  Tshs 1,920,900,000/= [+24]
Aidha baadhi ya sababu za kutokea kwa matukio ya ajali ni kuongezeka kwa vyombo vya usafiri mkoani Mbeya hasa magari na pikipiki, baadhi ya madereva kutozingatia sheria za usalama ikiwa ni pamoja na mwendo kasi hasa usiku na ulevi licha ya jitihada za Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na baadhi ya wadau kutoa elimu hiyo mara kwa mara. Hali ya hewa hususani ukungu na utelezi katika baadhi ya maeneo ya barabara ya Mbeya / Rungwe / Kyela.
  1. MATUKIO YALIYOVUTA HISIA KWA JAMII.
Jumla ya matukio matatu makubwa yaliyovuta hisia kwa kamii yaliripotiwa kama ifuatavyo : –
  1. JALADA LA UCHUNGUZI:
Tarehe 16.01.2017 saa 12:30hrs mtaa wa Igoma [A] kata Isanga, tarafa Sisimba jiji na mkoa wa Mbeya kulitokea tukio la waombolezaji kuzika jeneza tupu na mwili wa marehemu mtoto  HARUN JAILO KYANDO [9] Mkazi wa mtaa wa Igoma [A] kusahaulika nyumbani. Hata hivyo mwili huo baadae ulizikwa upya kwa kufuata taratibu.
  1. JALADA LA UCHUNGUZI:
Tarehe 15.02.2017 BARAKA S/O MWAFUNGO, miaka 22, msafwa, mkulima, mkazi wa Pipeline alifariki dunia kwa maradhi ya kisukari. Tarehe 18.02.2017 RUTH SEGETI [57] Mkazi wa Pipeline mama mzazi wa marehemu  akiwa na vijana wawili walifukua kaburi la mtoto wake na kutoa mwili huo kisha kuupeleka nyumbani kwake na kuuhifadhi kwa  imani kuwa atafufuka.  Hata hivyo mwili wa marehemu baadae ulizikwa upya tarehe 20.02.2017 kwa usimamizi wa Halmashauri ya wilaya Mbeya Vijijini.
  1. AJALI YA MOTO KUSABABISHA UHARIBIFU.
Tarehe 15.08.2017 saa 21:30hrs eneo la SIDO Mwanjelwa katika soko la Sido, lililopo Sido, kata ya Iyela, tarafa Iyunga jiji na mkoa wa Mbeya kulitokea ajali ya moto ambapo baadhi ya maduka / vibanda  vya soko hilo liliteketea kwa moto. Hakuna madhara kwa binadamu.  Thamani ya mali iliyoteketea inakadiliwa ni zaidi ya Tshs 500,000, 000/=.
  
  1. HALI YA ULINZI NA USALAMA KIPINDI CHA SIKUKUU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA – 2018.
Katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya 2018 kwa ujumla hali ilikuwa ni shwari, ulinzi uliimarishwa maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za ibada, kumbi za starehe, barabara kuu na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Hata hivyo kuna matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani yaliripotiwa kutokea kama kawaida kama ifuatavyo:-
  • Mauaji   – 1
  • Kujeruhi – 1
  • Ajali ya kifo – 1
Upande wa misako ni kama ifuatavyo:-
  • Bhangi gram 35
  • Pombe haramu ya moshi [gongo] lita 124
  • Silaha 3 aina tofauti Riffle 1, Shortgun 1 na Gobole 1 pamoja na risasi 8 za Shortgun na 2 za Riffle.
  • Wahamiaji haramu 17 wote raia wa Ethiopia
  • Risasi 81 za aina ya Riffle / Marv IV ziliokotwa na Polisi
  • Gari 2 aina ya Fuso zenye namba T. 394 BCL na T. 399 DCC na watuhumiwa 5 wakisafirisha milipuko  bila kibali aina ya Magzan – Kubella tani 20 kutoka [W] Chunya kuelekea mkoa wa Geita.
  • Upande wa Usalama barabarani tozo Tshs 47,160,000/= zilipatikana.
  1. MKAKATI  NA  MPANGO KAZI WA KUZUIA UHALIFU
Miongoni mwa mikakati/mpango kazi wa kuzuia uhalifu Mkoani Mbeya ni pamoja na :-
  • Kufanya tathmini ili kuyatambua matishio   katika maeneo yetu na mikakati ya kupunguza uhalifu ulioongezeka zaidi mwaka 2017.  
  • Kubaini muelekeo wa uhalifu na maeneo tete uhalifu ili kuelekeza nguvu za ziada katika  maeneo hayo [Crime threat analysis].
  • Kuchukua hatua za haraka pale tukio linapotokea na kulitolea taarifa.
  • Kuendelea na jitihada za kushawishi Halmashauri za Jiji/Miji/Wilaya katika kupambana na uhalifu. Hata hivyo changamoto iliyopo ni kwa Halmashauri hizo kutotambua kuwa jukumu la kuihakikishia jamii usalama wa maisha, mali, amani na  utulivu ni moja ya majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria namba 7 ya  mwaka 1982 ya sheria za Serikali za Mitaa [Serikali za Wilaya] pamoja na sheria namba 8 ya mwaka 1982 , sheria ya Serikali za Mitaa [Mamlaka za  Miji].
  • Kuongeza jitihada kwenye doria na misako yenye tija na ufanisi
  • Kuongeza kasi ya kueneza falsafa ya ulinzi shirikishi
  • Kuendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na taasisi za Serikali na vyombo vya udhibiti kama vile JWTZ, JKT,Magereza, Uhamiaji,Usalama wa Taifa,  Zima Moto na Uokoaji Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, TRA, TFDA n.k.
  • Kudumisha ushirikiano na vyombo vya habari vilivyopo Mkoa wa Mbeya.
  • Ushirikiano na Mikoa jirani [INTER-REGION CO-OPERATION] katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu.
  • Ushirikiano na madhehebu ya dini, wazee wa mila, viongozi wa Serikali za Mitaa, Kata, Tarafa na viongozi wa Vyama vya Siasa katika kupambana na uhalifu na wahalifu.
  • Kuimarisha utendaji wa weledi
  • Kujenga na kuimarisha uaminifu na uadilifu wa askari wetu.
  • Kuimarisha utoaji huduma bora kwa wananchi [Customer Care].
  1. MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KUTOKANA NA MISAKO, DORIA NA OPERESHENI.
Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na jitihada za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine ni :-
  • Bhangi uzito wa kilo 403 na gram 394 ilikamatwa ikiwa ni pamoja na mashamba makubwa 6  tofauti yenye ukubwa wa ekari 13 ½   ilivunwa na kuharibiwa kwa kuchomwa moto.
  • Mirungi kilo 4 pamoja na shamba moja lenye ukubwa wa nusu ekari ilivunwa na kuharibiwa kwa kuchomwa moto.
  • Dawa za kulevya aina ya heroine gram 196 ilikamatwa
  • Dawa ya kulevya aina ya amphetermine gram 20 ilikamatwa.
  •    Bidhaa za magendo zenye thamani ya Tshs 81,930,000/= ikiwemo bidhaa za magendo vipodozi vya aina mbalimbali vilivyopigwa marufuku na serikali vyenye viambata vya sumu, pombe kali na mahindi tani 60 na magunia 223 yaliyokuwa yakiingizwa nchini kutoka malawi yalikamatwa.
  • Nyara za Serikali zenye thamani Tshs 379,604,000/= na USD 300 zilikamatwa.
  • Wahamiaji haramu 344 walikamatwa wakiwemo Ethiopia 240, Malawi 48, Somalia 37, Burundi 17, Botswana 1 na Zambia 1.   Pia magari 3 yalikamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu hao ambayo ni T. 347 DAJ toyota haice, T. 917 AWM aina ya fuso na T.155 AZU aina ya isuzu canter pamoja na wasafirishaji 7 watanzania wamefikishwa mahakamani pamoja na magari hayo
  • Pombe haramu ya moshi gongo ujazo wa lita 3,719 pamoja na mitambo 33 ilikamatwa.
  • Jumla ya silaha 28 zilikamatwa ikiwemo shortgun 17, risasi 202, Riffle 2 na risasi 47, gobole 8 na bastola 1.  
  • Sare za JWTZ “kombati” suruali 2, mashati 2, kofia 2 na viatu / mabuti jozi mbili zilikamatwa.
  • Pombe kali zilizopigwa marufuku na serikali zenye vifungashio vya plastiki  zenye thamani ya zaidi ya Tshs 1,023,508, 750/= zilikamatwa maeneo mbalimbali mkoani Mbeya na kuzuiliwa kusubiri maelekezo toka serikalini.
  • Noti bandia Tshs 1,245,000/= na USD 1,199 zilikamatwa.
  • Tozo [Notification] Tshs 2,380,050,000/=   zilipatikana.
WITO WA KAMANDA:
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa pongezi kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kwa ushirikiano wao wa dhati kwa Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu kupitia dhana ya ulinzi shirikishi na Polisi jamii katika kipindi chote cha Januari  hadi Desemba – 2017,  aidha anatoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kipindi chote ili kuhakikisha mkoa wetu wa Mbeya unakuwa salama.
Pia natoa shukrani zangu za dhati kwa waandishi wa habari na vyombo vyote vya habari kwa ushirikiano wetu kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha mwaka 2017, kwa nafasi hii ninaomba ushirikiano huu uendelee katika kipindi cha mwaka 2018.
Aidha anatoa wito kwa wazazi/walezi kuzingatia utoaji wa malezi bora kwa watoto/vijana ili wakue katika misingi mizuri ya maadili mema katika jamii na kujiepusha na matukio ya kihalifu na kukataa uhalifu wangali wadogo ikiwa ni pamoja na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya, kucheza kamari na ulevi uliopitiliza.
Kwa kutambua kuwa suala la ulinzi na usalama unaanzia ngazi ya familia, mtaa, kitongoji,  kijiji, kata, tarafa, wilaya hadi ngazi ya mkoa, ni vema kila mmoja wetu kutambua na kuamini usalama wa mali na maisha yetu unaanzia na mimi, wewe na sisi sote. Kwa kuimarisha ulinzi na usalama wetu na mali zetu inatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika mkoa wetu, wananchi kujiajiri na kuajiriwa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii bila kuathiri amani na utulivu.
Aidha Kamanda MPINGA anatoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi  vilivyopo katika maeneo yao.  Pia kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuheshimu sheria na alama za usalama barabarani, watembea kwa miguu kuzingatia alama za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
                 Imesainiwa na:
    [MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
  KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments: