Tuesday, January 30, 2018

SERIKALI YASISITIZA UWAZI SHUGHULI ZA MADINI

Kampuni za Madini nchini zimetakiwa kufanya shughuli zake kwa uwazi sambamba na kufuata Sheria za nchi ili kuepuka migongano.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Januari 29, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwenye mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles aliyeambatana na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson.

Ujumbe huo ulimtembelea Katibu Mkuu Msanjila kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo suala la Sheria ya Madini, masuala ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) yanayofanywa na kampuni mbalimbali zikiwemo za kutoka nchini Canada na matarajio ya Serikali kwa kampuni (wawekezaji).

Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazofanya shughuli zake nchini zinalazimika kufuata taratibu na sheria za nchi ili kujijengea mazingira rafiki ya utekelezaji wa shughuli husika.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa kwa ujumla sambamba na wawekezaji na alibainisha kwamba lengo hilo litafikiwa ikiwa kampuni husika zitatekeleza wajibu wake kwa uwazi kulingana na matakwa ya sheria.

“Kampuni zinazojihusisha na shuguli za madini zinapaswa kufanya shughuli zake kwa usahihi na uwazi,” alisisitiza Profesa Msanjila.

Aidha, Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za madini nchini, zinapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa Wataalam waliopo Serikalini ili kupata mwelekeo sahihi wa dhamira ya Serikali.

“Kampuni zinatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kufanya shughuli zake kwa usahihi,” alisisitiza Profesa Msanjila.

Profesa Msanjila vilevile alizungumzia dhamira ya Serikali ya kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa nje ili kukuza uchumi wa Taifa.

“Madini yakiongezwa thamani hapa nchini, faida ni nyingi ikiwemo ajira na pia mapato yataongezeka kwani tutakuwa tumeelewa thamani halisi ya madini husika, kabla hayajasafirishwa,” alisema.

Ili kufikia dhamira hiyo, Profesa Msanjila alisema Serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni zilizoonyesha nia ya kujenga viwanda vya kuyeyusha na kusafisha madini (smelting and refining).

Mbali na hilo, Profesa Msanjila alizungumzia suala la uwezeshaji wachimbaji wadogo wa madini ambapo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba wananufaika ipasavyo na shughuli zao sambamba na mchango wao kwenye pato la Taifa kuonekana.

Alielezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwawezesha wachimbaji wadogo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya mafunzo vya mfano (centre of excellence) ambavyo alivitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha Tanga, Geita na Mtwara.

Kwa upande wake Balozi Myles alisema ni muhimu Serikali, Wawekezaji na Jamii kwa ujumla kushirikiana na pia kuwa na lengo la wazi la namna ya kunufaika kutokana na Sekta ya Madini.

Naye Davidson aliahidi kuzungumza na kampuni za Canada kuelezea matarajio ya Serikali kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la sheria, uwajibikaji kwa jamii, mazingira na michango mbalimbali ya kampuni kwa maendeleo ya jamii.

“Nitawakumbusha kwamba wanawajibika si kwa wanahisa wao peke yake bali pia kwa jamii wanapofanyia shughuli zao,” alisema Davidson.

Mkutano wa Katibu Mkuu wa Madini na Balozi wa Canada nchini ulihudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya. 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) akizungumza jambo wakati wa mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia) na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (kushoto).
 Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Madini na Balozi wa Canada (hawapo pichani). Kushoto ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya na kulia ni Kamishna wa Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy. Wengine ni Maafisa kutoa Wizara ya Madini.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kulia) akimsikiliza Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (katikati). Kushoto ni Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia). 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (wa pili kulia) mara baada ya kumalizika kwa mkutano na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Ian Myles (katikati). Kulia ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya. Kutoka kushoto ni Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson na Kamishna wa Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy.

No comments: