Tuesday, January 30, 2018

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI WA AFYA NCHINI KATIKA KUBORESHA SEKTA HIYO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.
Watumishi wa Baraza la Uuguzi na Ukunga pamoja na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye Picha) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga.
Afisa Uuguzi wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Jane Mazigo akitoa maelezo mbele ya Mgeni rasmi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga.
Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga aliyemaliza muda wake Stuart Mbelwa akipokea Cheti kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa Baraza la Uuguzi na Wakunga, Kulia ni Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Lena Mfalila
Mwenyekiti aliyeingia kuliongoza Baraza la Uuguzi na Ukunga Abner Mathube akiahidi kuchapa kazi mbele ya mgeni rasmi ambae ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga.
Picha ya Pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu wakati akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.



Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kuendelea kutatua changamoto za zinazowakabili watumishi wa Kada ya Afya nchini ikiwemo kuboresha miundombinu inayowazunguka.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) mapema leo wakati akizindua Baraza la Wauguzi na Wakunga katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.

“Asilimia 80% ya Kazi zote za kutoa huduma za Afya, zinafanywa na Wauguzi na Wakunga, kwaiyo wakati tunazungumzia kuboresha huduma za, Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuzifanyika kazi changamoto hizo ikiwemo suala la watumishi” alisema Mh. Ummy Mwalimu.

Mh. Ummy aliendelea kusema kwamba, sambamba na changamoto Wauguzi na Wakunga wanazoendelea kukumbana nazo Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kutatua changamoto hizo katika kuboresha Huduma za Afya.

Kwa upande mwingine Mh. Ummy alimwagiza Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Bw. Abner Mathube Kusimamia mabadiliko ya kanuni za maadili ya Baraza hilo ambazo zimeonekana kupitwa na wakati, hivyo kutofanya kazi kwa ufanisi unaostahili na kushindwa kuendana na wakati huu.

“Nimeelekeza zile kanuni za maadili za mwaka 2007 ni lazima zifanyiwe marekebisho, kwani zimepitwa na wakati, ili tuweze kusimamia taaluma hii vizuri ya Uuguzi na Ukunga.” Alisema Mh. Ummy Mwalimu.

Pia Mh. Ummy Mwalimu amelitaka Baraza hilo kujizatiti katika kutoa taarifa za Baraza mbele ya umma katika kueleza shughuli za kila mara za Baraza hilo, jambo litakalosaidia kuwafahamisha wananchi juu ya majukumu ya baraza hilo.

“Jamii haipati taarifa kuhusu utendaji kazi wa Baraza, tunatakiwa kuliona Baraza linakuja mbele, angalau kila robo mwaka katika kila kipindi, kukaa kimya kunafanya wananchi waone Baraza halina meno wala maamuzi” Alisema Mh. Ummy Mwalimu.

Kwa upande mwingine Mh. Ummy amelitaka Baraza hilo kuwachukulia hatua Waauguzi na Wakunga wanaenda kinyume na maadili ya kazi yao, huku akikemea matumizi ya lugha chafu yanayofanywa na baadhi ya wauguzi wachache ambao kwa kiasi kikubwa wanaitia doa kada hiyo.

Aidha, Mh. Ummy amemshukuru mwenyekiti aliyemaliza muda wake Stuart Mbelwa kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuliongoza Baraza hilo ikiwemo kusimamia wauguzi na wakunga nchini, kusimamia vyuo na vituo vya kutolea huduma za Afya na kuweza kukamilisha jengo la kuwaendeleza Wauguzi na Wakunga, huku akiwataka waamishe kazi zote za Baraza hilo katika jengo hilo lililopo Kibaha.

Mwisho Waziri Ummy aliahidi kuvifungia au kuvishusha hadhi Vituo vya Afya ambavyo havitakidhi vigezo vya kutoa huduma kwa jamii, huku akiwataka Wakurugenzi kujenga tabia ya kuvitembelea vituo hivyo ili kujionea mahitaji ya Vituo hivyo.

“Tutafungia au kuvishusha hadhi Vituo vya Afya ambavyo havikidhi vigezo, kwa hili hatutooneana aibu, wala kujali hiki ni kituo cha Afya cha serikali au chabinafsi, wakishindwa kutoa Huduma Bora hatutasita kuvifungia” alimaliza Mh. Ummy Mwalimu.

No comments: