Sunday, January 14, 2018

Reli ya ‘Standard Gauge” Sasa Dar Mpaka Rwanda

Na. Judith Mhina 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuunganisha Reli ya Kisasa (Standard Gauge) kutoka Isaka mkoani Shinyanga mpaka Kigali nchini Rwanda, ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizi mbili.

Rais Magufuli ameeleza hayo leo Ikulu Jijini Daar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame aliyekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.“Mimi na Rais Kagame kumeongea mambo mengi ya ushirikiano na kwa pamoja tumekubaliana kuanza ujenzi wa Reli ya Standard Gauge kutoka Isaka mpaka Kigali,” ameeleza Rais Magufuli.

Ameeleza kuwa ili kuharakisha ujenzi wa reli hiyo, kwa pamoja wamewaagiza Mawaziri wanaohusika na sekta ya ujenzi na wale wale wa Mambo ya Nje wa nchi hizi mbili kukutana haraka wiki ijayo kusughulikia masuala kadhaa yanayohusu ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni pamoja na kujadili namna ya upatikanaji wa fedha za ujenzi.

Akielezea umuhimu wa kukuza uchumi na biashara baina nchi hizi mbili, Rais Magufuli amesema mpaka sasa mwenendo wa biashara kati ya nchi hizi umekuwa wa kusuasua na kwamba reli hiyo itasaidia kuimarisha biashara na ushirikiano wa Tanzania na Rwanda.

“Tunataka ikifika mwezi Desemba mwaka huu, mimi na Rais Kagame tuwe tayari tumeweka mawe ya msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli hii,” alisisitiza Rais Magufuli.

Amesisitiza kuwa mbali na kuimarisha uchumi, ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa takribani kilometa 400 pia utatoa ajira kwa vijana wengi na kusaidia usafirishaji wa madini ya Nickel kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania ambapo madini hayo yanashindwa kuchimbwa kutokana na kukosekana usafiri madhubuti wa reli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kwamba Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa asilimia mia moja katika kuchukua Uenyekiti wa Umoja wa Afrika na kwamba itafanya kila linalowezekana kuzishawishi nchi marafiki pia zimuunge mkono Rais huyo wa Rwanda.

Kwa upande wake, Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli na Watanzania kwa kumuunga mkono katika nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Afrika na kwamba atafanya kila linalowezekana kuzishawishi nchi za Afrika kuongeza uwekezaji na kila nchi kuweka kikakati ya kuongeza ajira ili kuwafanya vijana waachane na dhana ya kukimbili nchi za Ulaya kutafuta maisha bora.

“Tatizo la vijaqna kukimbilia nchi za Ulaya linaweza kumalizika iwapo sisi Waafrika kwa umoja wetu tutashirikiana na kutafuta ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na nchi moja moja kuweka mikakati madhubuti ya kuwapa elimu na ujuzi sahihi ili vijana hawa waweze kumudu mazingira yao na kujiendeleza.” Ameeleza Rais Kagame.

Aidha, Rais Kagame amesifu utendaji kazi wa Rais Magufuli na kuahidi kuja mara kwa mara nchini Tanzania kwa ajili ya ushauri na kujifunza zaidi. “Naahidi kuwa nitakuwa nakujamara kwa mara kuomba ushauri kutoka kwa Rais Magufuli ili kuweza kusaidia nchi zetu na Bara la Afrika kwa ujumla. Alimalizia Kagame

Hii ni ziara ya tatu kwa Rais Kagame kuzuru Tanzania tangu Rais Magufuli aingie Madarakani mwaka 2015. Mara ya kwanza alikuja kuhudhuria sherehe za kuapishwa John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1 comment:

Unknown said...

hotuba nzuri yenye kuleta majibu kwa maendeleo ya nchi zote mbili kwa vizazi vijavyoa kama yatatekelezwa kwa wakati