Thursday, January 18, 2018

RC NDIKILO AWAPA ONYO WARATIBU WA ELIMU KATA /AWATAKA KUJIKITA KWENYE AJIRA YAO ILI KUINUA TAALUMA MKOANI PWANI

Kaimu afisa elimu sekondari halmashauri ya Chalinze ,Irene Lubega akimkabidhi ripoti ya taarifa ya mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mashuleni hadi sasa ,mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,ambapo mahudhurio hayaridhishi kimkoa bado yakiwa chini ya asilimia 50
Kaimu afisa elimu sekondari halmashauri ya Bagamoyo ,Juma Yusuph akisoma ripoti ya taarifa ya mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mashuleni hadi sasa mbele ya mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,ambapo mahudhurio hayaridhishi kimkoa bado yakiwa chini ya asilimia 50
Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete akizungumzia masuala ya kielimu mara baada ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,kupitia shule ya sekondari Mboga ,Chalinze kuzungumzia hali ya mahudhurio ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ambapo hali ya mahudhurio mashuleni hayaridhishi kimkoa bado yakiwa chini ya asilimia 50
Mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo(aliyesimama) akizungumzia masuala ya kielimu mara baada ya kupitia shule ya sekondari Mboga ,Chalinze kuzungumzia hali ya mahudhurio ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ambapo hali ya mahudhurio mashuleni hayaridhishi kimkoa bado yakiwa chini ya asilimia 50.Picha na Mwamvua Mwinyi


Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze

MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,amewaasa waratibu wa elimu kata,kusimamia masuala ya elimu ili kuinua kiwango cha taaluma,na atakaebainika kwenda kinyume na majukumu yake ajihesabu amejifukuzisha kazi.

Aidha hajafurahishwa na hali ya mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ambapo mahudhurio yapo chini ya asilimia 50 kimkoa.Pamoja na hayo,ametoa rai kukamatwa na kufikishwa mahakamani , wazazi na walezi wote ambao watashindwa kuwapeleka watoto wao kuripoti shule kwa wakati.

Ndikilo,aliyasema hayo ,wakati akizungumza na baadhi ya waratibu wa kata, maafisa elimu wa Chalinze na Bagamoyo,walimu na wajumbe wa bodi ya shule ya sekondari Mboga,iliyopo Chalinze .Alisema mratibu wa elimu kata atakayefanya uzembe na kubainika kujishughulisha na masuala tofauti na kazi yake atamvua kazi.

Ndikilo ,aliwapa siku saba kuhakikisha hali ya mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mashuleni inakuwa nzuri tofauti na sasa.Alisema hali ya mahudhurio hairidhishi ,kwani wanafunzi waliotakiwa kuripoti shule ya sekondari Mboga hadi sasa ni asilimia 51 pekee.

Alisema tathmini iliyofanyika kwa halmashauri ya Bagamoyo wanafunzi walioripoti shule ni asilimia 43.4,Chalinze ni asilimia 50.63.Halmashauri nyingine ni Rufiji ambayo hali ya mahudhurio ni asilimia 75, Mafia wanafunzi walioripoti ni asilimia 86.73 hivyo ni lazima kulivalia njuga suala hilo.

Ndikilo alieleza ,hii ni wiki ya pili lakini inashangaza kuona mahudhurio hayaridhishi katika shule walizopangiwa watoto hao huku elimu ikiwa ni bure.Hata hivyo,alikemea tabia inayofanywa na baadhi ya wakuu wa shule na bodi za shule kuwapa masharti ya kuchangia michango wazazi wakati wakiwapeleka watoto wao kuripoti shuleni.

“Kama bado kuna mwalimu ama shule inatoza wazazi ama wanafunzi fedha za michango,la sivyo vifaa kama madawati na mambo mengine atafukuzwa kazi,’;kwa hili halina mchezo tutafukuzana kazi ,haiwezekani mh.Rais anasisitiza elimu bure nyie huku mnakandamiza wazazi”

Ndikilo,aliwataka waratibu wa elimu,watendaji,maafisa Tarafa,wakuu wa shule kushirikiana kusimamia watoto waliopo majumbani kuhakikisha wanakwenda shule ,kwani sio jambo la mzaha hata kidogo.

“Pia mzazi,mlezi ambae ana mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ,haumwi ukigundulika ni kukamatwa na kufikishwa mahakamani,ili wapate cha mtema kuni,Serikali inatoa mabilioni ya fedha ,lakini walengwa hakuna wanachokifanya,inasikitisha sana”;:

Kwa upande wao kaimu afisa elimu sekondari Bagamoyo,Juma Yusuph na kaimu afisa elimu sekondari Chalinze,Irene Lubega walipokea maagizo yaliyotolewa na kusema watayafanyia kazi.Nae ,mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alhaj Majid Mwanga,alisema alichogundua waratibu wa elimu kata wanahangaika na masuala ya TASAF badala ya kushughulika na elimu.

Aliwakemea waratibu hao kujishughulisha na mambo nje ya majukumu ya elimu,ambayo yanatia doa elimu ,inashusha taaluma wilayani humo na kuwa wa mwisho.Alhaj Mwanga,aliwaeleza kazi za TASAF wawaachie watendaji wa kata,wa vijiji ,maafisa Tarafa ili kuongeza hali ya taaluma wilayani Bagamoyo.

Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete alisema mwaka uliopita wa masomo wanafunzi wamefaulu wengi lakini changamoto iliyopo Chalinze ni kuchelewa wanafunzi kuripoti shule kutokana na maeneo waliyopangiwa ni ya mbali.

Alisema jiografia iliyopo inasababisha wanafunzi kushindwa kufikia maeneo ya shule walizopangiwa kuwa mbali.Ridhiwani alisema wapo wanafunzi waliochaguliwa kutoka shule za Chalnze na Bwilingu lakini wamepangiwa shule za Kibindu na Matipwili ambako ni umbali mrefu hali ambayo wazazi hawana uwezo wa kumudu gharama zinazotakiwa.

Alitoa wito huo na kutoa changamoto hiyo ili halmashauri zianze kujipanga na kuweka mkakati hasa wa kuongeza madarasa kwenye shule za sekondari hadi ifikapo 2020.

No comments: