Saturday, January 20, 2018

KWANDIKWA: BARABARA ZA MCHEPUO KUPUNGUZA MSONGAMANO DODOMA

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, sehemu ya ujenzi wa barabara ya mchepuo kutoka Chimwaga-Ihumwa yenye urefu wa KM 10 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari yanayoingia mkoani humo.Mhandisi Mkazi anayesimamia ujenzi wa barabara ya Chimwaga-Ihumwa KM 10 kwa kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi kwa waandishi wa habari ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.4 na KM 8 zimeshakamilika kujengwa, mkoani DodomaNaibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mbande-Kongwa KM 11.7, inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani humo.Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, athari za mvua eneo la katondo katika barabara za mji huo.Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiongozana na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, wakikagua athari za mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es Salaam.Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nae wakati akikagua athari za mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es Salaam.Muonekano wa sehemu ya barabara ya mchepuo ya Chimwaga-Ihumwa yenye urefu wa KM 10 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Dodoma.

………………………………………………………………………….

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa (Km 11.7) na Chimwaga – Ihumwa (Km 10) utasaidia kupunguza msongamano kwa magari yanayoingia Dodoma mjini.

Naibu Waziri huyo ameyasema hayo wakati akikagua barabara hizo na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambapo amesisitiza kwa makandarasi wanaojenga barabara hizo kuhakikisha wanamaliza kazi hizo kwa muda uliopangwa na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba.

“Tutaendelea kujenga na kuboresha barabara hizi za mchepuo lengo ni kupunguza foleni katikati ya mji kwani Dodoma sasa inakua kutokana na uwepo wa watumishi wengi wa Serikali na ongezeko la magari, kwa hiyo sisi kama Serikali hatuna budi kuangalia namna ya kuboresha miundombinu yetu ili ikidhi haja ya ongezeko hili”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, amefafanua kuwa barabara hizo zikikamilika zitakuwa ni njia mbadala kwa watumiaji kwani sio lazima kwa magari yote kupita mjini na badala yake yatatumia njia nyingine za mchepuo kuendelea na safari zake.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua athari za mvua katika barabara za mji wa Dodoma na kuwataka wananchi na madereva kuchukua tahadhari ili kuepusha hatari zinazoweza kuwakabili wakati wakivuka ama kupitisha magari yao katika kipindi hiki ambacho baadhi ya sehemu za barabara zinajaa maji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha. 

Amewaomba viongozi mbalimbali wa Serikali kushirikiana katika kutoa ushauri kwa wananchi kuhusu utafutaji wa maeneo yanayowafaa kuishi ili kunusuru maisha yao na mafuriko ambayo yanaweza kuwakabili kutokana na kuchagua maeneo yasiyo sahihi kwa makazi ya binadamu.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amefafanua kuwa barabara ya Mbande- Kongwa yenye urefu wa KM 11.7, kwa sasa imejengwa kilometa Tano ikiwa ni awamu ya kwanza na kufikia mwezi ujao watajenga tena kilometa nyingine Tano.

Naye, Msimamizi wa ujenzi wa barabara ya Chimwaga – Ihumwa yenye urefu wa KM 10 kwa kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, amesema mradi ulianza mwaka 2013, ambapo kwa sasa umefika asilimia 92.4 na kilometa 8 tayari zimeshajengwa.

Ujenzi wa Barabara ya Chimwaga- Ihumwa (Km 10), inajengwa na mkandarasi Nyanza Road Works kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 15 ambapo ujenzi wake unaendelea na unategemewa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.

No comments: