Tuesday, January 30, 2018

GLOBAL FUND YATOA TRIONI MOJA KWA TANZANIA KUSAIDIA UKIMWI, TB NA MALARIA



Na Said Mwishehe, Globu ya jamii 

SERIKALI ya Tanzania na Global Fund wamewekeana saini mkataba wa Dola za Marekani milioni 525 sawa na Sh.Trilioni 1.155 kwa lengo la kufadhili shughuli za kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu,Maralia na uimarishaji wa mifumo ya afya nchini. 

Imeelezwa ushirikiano huo wa Global Fund ambao ndio waliotoa fedha hizo kwa Serikali ya Tanzania unategemewa kuongeza kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma za afya Katina magonjwa hayo. 

Wakati wa utiwaji saini wa mikataba ya fedha hizo, wadau mbalimbali walihudhuria ambao ni viongozi wa Serikali, mabalozi, asasi za kiraia za ndani na za kimataifa.Pia wajumbe wa bodi ya uratibu ya Global Fund nchini pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndiyo iliyoandaa shughuli hiyo. 

Akizungumza mapema jana jijini Dar es Salaam baada ya utiwaji saini wa mikataba ya fedha hizo, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu Global Fund wamekuwa wachingiaji muhimu katika sekta ya afya.

Amefafanua wamekuwa wachangiaji wakubwa katika kuzuia na kupambana na magonjwa hayo matatu tangu kuanzishwa kwa mfuko huo mwaka 2001."Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania napenda kutoa shukrani za dhati kwa Global Fund kwa ushirikiano wao ambao umewezesha nchi kuboresha afya za wananchi wetu pamoja na kuboresha mifumo ya afya, "amesema Mwalim. 

Ameongeza kwa kupitia uratibu wa Global Fund fedha ziliweza kutumika nchini kupitia sekta ya umma kwasbabu zimekuwa zikitumika kununua na kusambaza dawa, vitendanishi, vifaa tiba kwa magonjwa hayo matatu. Waziri Mwalimu amesema kwa ufadhili huo kwa miradi ya awali wamefanikiwa kwenye baadhi ya maeneo. Baadhi ya mafanikio ni ununuzi wa Gene -xpert 91 kwa ajili ya kupima Kifua Kikuu katika Wilaya 91.

"Aidha ufadhili huu umewezesha nchi kufikia kiwango cha juu cha ufanisi(asilimia 90) katika kutoa tiba ya Kifua Kikuu na wagonjwa kupona, "amesema Waziri Mwalimu. Kwenye malaria zaidi ya vyandarua milioni 40 vyenye viatilifu vimesambazwa nchini kupitia programu mbalimbali ambapo Waziri Mwalim anaongeza wagonjwa wanaotibiwa malaria bila kupimwa kuhakikisha uwepo wa malaria wamepungu kutoka asilimia 36 mwaka 2014 mpaka asilimia 5 mwaka 2017.

Kwa ugonjwa wa Ukimwi, Waziri amesema imeonekana kuwa hali ya maambukizi katika jamii imepungua kutoka asilimia 10 mwaka 1990 mpaka asilimia 4.7 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 mwaka 2016.

Amesema jumla ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi 935,374 walikuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi nchini mpaka kufikia mwishoni kwa Septemba mwaka 2017 huduma ambazo hutolewa katika vituo vipatavyo 5,785 nchini. 

Ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia Global Fund kuwa fedha ambazo wamezitoa zitatumika katika malengo yaliyokusudiwa na hakuna hata senti moja itakayotumika kinyume na malengo hayo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Makamu wa Rais (Sera na Uratibu), Profesa Faustine Kamuzora (kulia), na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban, wakisaini hati za makabidhiano ya sh.  trioni moja zilizotolewa na Shirika la Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano ya Ukimwi, TB na Malaria katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam leo. Wengine waliosimama katikati ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na viongozi wengine kutoka Global Fund.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya, akizungumza katika hafla hiyo.
Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania, Frederic Clavier, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mnufaika wa Global Fund, Joan akielezea jinsi alivyo nufaika na shirika hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaishi na VVU-Ukimwi, Mwinuka Juastine, akizungumza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban (kulia), akimkabidhi hati ya makabidhiano Mwakilishi wa Global Fund Tanzania, Linden Morrison.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Makamu wa Rais (Sera na Uratibu), Profesa Faustine Kamuzora, akizungumza.
Taswira ya ukumbi wa mkutano katika uzinduzi huo.

No comments: