Friday, January 19, 2018

Ajipanga Kutembea Hadi Magogoni Kuunga Mkono Juhudi za Rais Magufuli

Kijana Mzarendo,Omary Kombe akizungumzana na waandishi wa hawapo pichani juu ya kutembea kutoka Kimara hadi Kivukoni siku ya Jumamosi, Januari 20,mwaka huu ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo, Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Kutoa Elimu ya Unyonyaji kwa Watu Wenye Ualbino, Maiko Lugendo.
Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Kutoa Elimu ya Unyonyaji kwa Watu Wenye Ualbino,Maiko Lugendo akimkabdhi Kijana Mzarendo,Omary Kombe t-shirt atakayo vaakesho kwaajili ya matembezi hayo.picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Kijana mzalendo, Omary Kombe amejipanga kutembea kutoka Kimara hadi Kivukoni siku ya Jumamosi, Januari 20, 2018 ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo.

Kombe ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya nia ya matembezi yake pamoja na mpango wake wa kutoa tuzo kwa Rais Magufuli itakayojulikana kama ‘Tuzo ya Kiongozi Mzalendo’.

Kombe amesema kuwa Rais Magufuli amekuwa ni kiongozi makini, mwenye uthubutu, mwenye msimamo thabiti na mzalendo wa kweli kwani amefanya mambo mbalimbali yakiwemo ya kuimarisha mfumo wa ulipaji kodi, kubadilisha sheri kandamizi za madini, kukomesha vitendo vya ujangili katika mbuga za wanyama, rushwa na dawa za kulevya pia kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma.

“Kubwa kuliko yote, Serikali ya Awamu wa Tano kwa ujumla imekuwa ikihamasisha kwa vitendo kuhusu ujenzi wa Tanzania ya Viwanda na kupelekea nchi kuwa na uchumi wa kati hivyo kwa niaba ya vijana wazalendo napenda kumpongeza kwa kufanya matembezi, kumpa tuzo ya kiongozi mzalendo pamoja na kutoa msaada katika hospitali ya Ocean Road iliyopo jijini hapa,” alieleza Kombe.

Aidha, kijana huyo ametoa baadhi ya mapendekezo ambayo yataisaidia Serikali yakiwemo ya kuanzishwa kwa program ya kuunganisha wafanyabiashara wa zana za kilimo, Taasisi za kifedha, vikundi vya wakulima na Vyama vya Ushirika ili wakulima waweze kukopeshwa zana hizo kwa urahisi.

Ametoa rai kwa viongozi wa dini na wananchi kuzidi kumuombea Rais Magufuli ili aendelee kuwa na moyo wa uzalendo utakaoifanya Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Kutoa Elimu ya Unyonyaji kwa Watu Wenye Ualbino, Maiko Lugendo amesema kuwa Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa lakini watu wachache walikuwa wakiipeleka pabaya hivyo anamshkuru Rais Magufuli kwa kuonyesha uzalendo katika kuipeleka nchi mbele.

“Uzalendo ni kitu muhimu sana katika nchi kwani mjenga nchi na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe hivyo nampongeza sana Kombe kwa nia yake, tukiamua kuwa wazalendo tukishirikiana na Rais Magufuli hakika nchi itakuwa bora,”alisema Lugendo. 

Kijana huyo amekuwa akishiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya kuanzisha kituo cha kulelea watoto waishio katika mazingira magumu cha New Hope Family Group, Mwenyekiti Mstaafu wa Bodi ya Zahanati ya Mjimwema, Mjumbe wa Bodi ya Hospitali ya Vijibweni, Mwanzilishi wa Kombe la Amani na Upendo pamoja na kuanzisha stika yenye ujumbe maalum wa kutokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

No comments: