Sunday, December 10, 2017

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YAIBUKA KIDEDEA TAARIFA BORA YA HESABU KWA MWAKA 2016


Benny Mwaipaja-WFM, Dar es Salaam

Wizara ya Fedha na Mipango Fungu Hamsini (Vote 50)linalohusika na masuala ya utawala, limeibuka kinara kwa kupata tuzo ya mshindi wa kwanza katika utoaji wa Taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 katika kundi la Wizara na Idara za Serikali inayoandaliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).

Tuzo hizo zimetolewa kwa washindi na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu nchini uliofanyika katika eneo hilo.

CPA. Mwakapalila alisema kuwa taarifa bora za fedha ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi kwa kuwa walipa kodi, wawekezaji na wadau wengine hutegemea taarifa hizo katika kufanya maamuzi.

‘Kama taarifa za fedha hazitatolewa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati mwafaka kunaweza kusababisha athari katika uthabiti wa mifumo ya kifedha nchini’, alieleza CPA. Mwakapalila

Aidha Mwakapalila amewapongeza wahasibu kwa kuamua kukaa pamoja na kujadili taaluma ya uhasibu katika maendeleo ya viwanda ambayo ni ajenda ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya tano.

Amesema suala la Uchumi wa viwanda ni muhimu katika kuongeza kipato na kupata fedha za kigeni kwa njia ya kuuza bidhaa nje na pia kupata mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hivyo akatoa rai kwa wananchi kuendelea kujadili masuala ya uchumi wa viwanda na kupata namna sahihi ya kuufikia ili ndoto ya uchumi huo ziweze kuwa za kweli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA. Pius Maneno amesema kuwa tuzo zinazotolewa na NBAA zinalengo la kuhamasisha uwajibikaji na kuandaa taarifa ya fedha zilizo na viwango vya kimataifa.

Amesema kuwa washindi wa tuzo hizo wanapatikana kupitia mchakato uliosheheni weledi wa hali ya juu kutoka kwa wabobezi wa taaluma ya uhasibu nchini ambao wanaangalia vigezo kadhaa vikiwemo kuwa na hati safi na kuwasilisha Hesabu kwa wakati na pia kufikisha kiwango cha ubora wa taarifa kuanzia asilimia 75.

Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50, Bw. Christopher Nkupama, amesema kuwa tuzo hiyo inawapa morali ya kufanyakazi kwa umahili zaidi na kuwapongeza watumishi walioko katika idara yake kwa kufanyakazi kubwa na bila kuchoka kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni na taratibu za uhasibu wanapotekeleza majukumu yao.

Mshindi wa Jumla katika tuzo hizo kwa taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 ni Twiga Cement Plc na kwa upande wa Wizara na Idara za Serikali ni Wizara ya Fedha na Mipango fungu hamsini (V. 50), tuzo ambayo ilipokelewa na Mhasibu Mkuu wa fungu hilo Bw. Christopher Nkupama, ikifuatiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji fungu arobaini na nne (V.44) na Ofisi ya Waziri Mkuu fungu ishirini na tano (V. 25)

Washiriki wa Tuzo hizo ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Wizara na Idara za Serikali na Sekta Binafsi ambapo kwa mwaka huu waliojitokeza kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa walikua sita na Wizara na Idara za Serikali walikua sita.

Jumla ya washidani waliojitokeza ni 56 na waliofanikiwa kuvuka kigezo cha kuwa na zaidi ya asilimia 75 walikua washidi 36 na hao walifanikiwa kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu kulingana na makundi.

Vilevile Idadi ya Wahasibu ambao wamehudhuria katika Mkutano wa mwaka ambao hufanyika kila mwaka kabla ya kutolewa tuzo hizo imepanda kwa asilimia 60 ambapo mwaka 2016 walihudhuria wajumbe 1700 ilihali mwaka huu 2017 wamehudhuria zaidi ya wajumbe 2700.
Wahasibu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50 wakiwa katika picha ya pamoja na Mhasibu Mkuu wa Fungu hilo Bw. Christopher Nkupama (wa pili kushoto) baada ya kupokea Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 zilizotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam .
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wahasibu wa Wizara hiyo fungu 50 baada ya kuwakabidhi tuzo hiyo katika eneo la Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, aliyeshika tuzo ni Mhasibu Mkuu wa Fungu hilo Bw. Christopher Nkupama.
Washindi wa Kwanza wa makundi mbalimbali ya Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 zinazotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) wakiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu baada ya kukabidhiwa tuzo hizo eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mmoja wa wahasibu walioambatana na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango-fungu 50, Bw. Christopher Nkupama (hayupo pichani) akisalimiana na meza kuu baada ya kupokea tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 iliyotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju nje kidogo ya Jiji l Dar es Salaam.

Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (wa kwanza kulia) akimklabidhi Mhasibu wa Wizara ya Fedha na Mipango-fungu 50 (Vote 50), Bw. Christopher Nkupama (kushoto) tuzo kwa kuwa mshindi wa kwanza wa taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 kwa kundi la Wizara na Idara za Serikali iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju, Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA. Pius Maneno.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila akieleza kuwa Uhasibu ni taaluma muhimu katika maendeleo ya Viwanda kwa kuwa wawekezaji hutumia taarifa za fedha zinazoandaliwa ili kutoa maamuzi, wakati wa kuhitimisha mkutano wa mwaka wa Wahasibu na kugawa tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa washindi wa mwaka 2016, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) CPA. Pius Maneno muda mfupi kabla ya kutoa tuzo za taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango

No comments: